Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Sauti tu ilinipendeza, nahofia umbo halitanivutia

August 7th, 2019 2 min read

Na SHANGAZI

SHANGAZI natumai wewe ni mzima. Kuna mwanamke tuliyejuana kupitia kwa simu nilipompigia kimakosa. Sauti yake iligusa hisia zangu na tangu hapo tumekuwa tukiwasiliana. Tumepanga kukutana na nina wasiwasi kwamba huenda nikapata kwamba maumbile yake si ya mwanamke ninayemtaka. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Siamini kuwa watu wanaweza kujuana na kupendana kupitia kwa simu. Mapenzi hutokana na watu kuonana na kuzungumza ana kwa ana. Ni vyema kwamba mmepanga kukutana. Baada ya hapo utajua iwapo anakufaa. Usiwe na hofu kwani ukigundua siye unayemtaka una haki ya kumwambia ukweli huo.

 

Nimeamua simtaki tena sababu nahisi hana nia nzuri

Kwako shangazi. Nimependana na mwanamume aliyekuwa ameoa lakini wakaachana na mke wake. Nimekuwa nikimtembelea kwake mara kwa mara na ameahidi kunioa. Nilishangaa sana juzi nilimpomtembelea kwake nikampata na aliyekuwa mke wake. Aliniomba niondoke kisha nirudi baadaye. Nilikasirika sana kwa hivyo sikurudi. Baadaye alinipigia simu kuniambia eti mke wake alimtembelea tu kumjulia hali. Sikuamini maelezo hayo na nimeamua kumuacha. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Hali uliyoshuhudia inaonyesha kuwa wawili hao wametengana tu, hawajaachana rasmi na kuna uwezekano mkubwa kwao kurudiana. Ndiyo sababu mwanamke huyo yuko huru kumtembelea mumewe wakati wowote anapotaka. Hatua ya mwanamume huyo kukutaka uondoke pia inaonyesha kuwa anamthamini mwanamke huyo kuliko wewe. Ninaunga mkono uamuzi wako.

 

Mtego wa mpenzi umenikasirisha sana, naona haniamini

Kwako shangazi. Nimekuwa katika uhusiano wa kimapenzi kwa miaka miwili sasa. Kuna mwanamume rafiki ya mpenzi wangu ambaye ameniandama sana akitaka tuwe na uhusiano wa kisiri lakini nimekataa. Nilishangaa sana juzi mpenzi wangu aliponiambia kuwa ni yeye alimtuma akitaka kujua iwapo mimi ni mwaminifu kwake. Nimekasirika sana kujua kuwa mwenzangu haniamini na nafikiria kumuacha. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Ni vibaya kwa mpenzi wako kukushuku bila sababu na pia njia aliyotumia kuthibitisha uaminifu wako kwake si nzuri. Hata hivyo, haina maana kumuacha kama unampenda kwa dhati. Sasa atakuheshimu kwa sababu uchunguzi wake huo umethibitisha kuwa wewe ni mwaminifu kwake.

 

Ataka mimba iwe siri hadi mtoto azaliwe, hiyo ni sawa kweli?

Vipi shangazi? Natumai kuwa wewe ni mzima. Nimekwua na mpenzi kwa karibu mwaka mmoja na sasa nimepata mimba yake. Wazazi wetu wanajua kuhusu uhusiano wetu. Hata hivyo, amenikataza kuwaambia kuwa nina mimba akisema tutawaambia tukipata mtoto. Hiyo ni sawa kweli?

Kupitia SMS

Ni vigumu kujua kinachoendelea katika mawazo ya mtu na mara nyingi inabidi uamini anayokwambia kama huna ushahidi wa kuonyesha kuwa anakuhadaa. Uzuri ni kwamba wazazi wenu wanajua kuhusu uhusiano wenu kwa hivyo utakapopata mtoto hatakuwa na namna ya kukukana. Ushauri wangu ni kuwa uondoe shaka na kusubiri hadi wakati huo.

 

Mpenzi amenikataza kumpigia simu au hata kumtumia SMS

Vipi shangazi? Nina umri wa miaka 23 na nina uhusiano na kijana ninayempenda kwa dhati. Hata hivyo kuna tabia yake fulani ambayo inanitia wasiwasi. Amenikataza kabisa kumpigia simu ama kumtumia SMS kwa madai eti anakuwa na shughuli nyingi. Badala yake anasisitiza kuwa ndiye atakuwa akinipigia akipata nafasi. Nishauri.

Kupitia SMS

Sijawahi kuona uhusiano ambapo mmoja wa wahusika hana haki ya kuwasiliana na mwenzake anapotaka. Haiwezekani kwamba mpenzi wako huyo huwa na shughuli usiku na mchana. Ukweli ni kuwa kuna jambo ambalo anakuficha. Inawezekana kuwa ana mwingine na hataki kugunduliwa. Ningekuwa wewe singeendelea kupoteza wakati zaidi kwake.