Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Shangazi anapinga ndoa yetu akidai mpenzi ni mzee

April 6th, 2019 2 min read

Na SHANGAZI

SHIKAMOO shangazi! Nina mpenzi ambaye tumepanga kuoana ingawa amenizidi umri kwa miaka mitatu. Lakini shangazi yake amekuwa akipinga vikali uhusiano wetu kwa sababu ya tofauti hiyo ya umri akidai tunapotezeana wakati. Ajabu ni kwamba yeye mwenyewe hajaolewa ingawa ana watoto wawili. Nishauri tafadhali.

Kupitia SMS

Uhusiano wenu haumhusu kabisa huyo shangazi ya mpenzi wako. Kama hakuna kati yenu anayetatizwa na hiyo tofauti ya umri, fungeni masikio na muendelee na mipango yenu. Huenda huyo shangazi yake anawaonea wivu kwa sababu yeye hajaolewa.

 

Sina hisia zozote kwa mume wangu

Shangazi mimi nimeolewa kwa miaka mitatu na nina mtoto mmoja. Tatizo ni kuwa sina hisia kabisa kwa mume wangu ingawa yeye ananipenda sana. Damu yangu imemkataa kabisa. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Hiyo ni hali yenye utata sana hasa kwa sababu hamjakosana, tena unasema mumeo anakupenda. Hata hivyo, iwapo unaamini hali hiyo haitabadilka ni muhimu ufungue moyo wako kwake umwambie ukweli ili ajue la kufanya.

 

Huwa ninachukia kila ninayepakulia

Shangazi natumai wewe ni mzima. Naomba unipe ushauri kuhusu jambo moja ambalo linanisumbua. Kila nikipendana na mwanamume kisha turushe roho mimi humchukia na huwa hata sitaki kumuona tena. Ni kwa nini?

Kupitia SMS

Hizo ni dalili za mapenzi yasiyo ya dhati. Nahisi kuwa umekuwa ukiongozwa na hisia za kimwili wala si za moyoni, na ndiyo maana zikishughulikiwa huwa huna haja tena na huyo mtu. Mapenzi kutoka moyoni hudumu hata hisia za mwilini zikitoweka. Ni mapenzi ya dhati tu ambayo yatakutoa katika hali hiyo.

 

Hajui ameniteka

Vipi shangazi. Kuna mwanamume jirani yangu ambaye ameteka moyo na hisia zangu lakini hajui. Nifanye nini ili tuwe wapenzi?

Kupitia SMS

Itakuwa vigumu kwake kujua kuwa unavyohisi usipomwambia ama kuonyesha dalili hizo. Kwa sababu si rahisi kumwambia moja kwa moja, jaribu kujenga urafiki wa karibu naye ili uone kama naye anavutiwa na labda atakuomba penzi lako.

 

Nimepewa mimba na mwanamume aliyeoa

Kwako shangazi. Nina umri wa miaka 22 na nimependana na mwanamume ambaye ana mke na nimepata mimba yake. Ameahidi kunioa lakini wazazi wangu wamepinga vikali mpango huo. Nampenda sana na sijui nitafanya nini.

Kupitia SMS

Hapo umefanya makosa mara mbili. Kosa la kwanza ni kuwa na uhusiano na mwanaume ambaye ana mke. Kosa la pili ni kukubali kubeba mimba yake na bado hajakuoa. Kama wazazi wako wamekataa ukiolewa mke wa pili, itabidi uwe tayari kulea mtoto hadi utakapopata mume.

 

Demu amesema ni wake wa pili

Vipi shangazi? Kuna msichana ambaye amekuwa akinitembelea kwangu na sijui nia yake hasa. Nilimuuliza kama ananipenda akasema ana mwingine lakini eti anaweza kuwa na wawili. Nilimshauri amuache akanyamaza. Nina hakika ananipenda lakini hataki kuniambia. Nishauri.

Kupitia SMS

Inaonekana msichana huyo amekuwa akikutaka na ameamua kwamba ni lazima ujue. Huenda hata hana mwingine na anatafuta tu hakikisho kutoka kwako kuwa wewe pia unampenda. Fuatilia ujue kama ana mwingine ili upate mwelekeo.

 

Ameniambia niache masomo ili anioe

Shikamoo shangazi! Mimi ni mwanafunzi wa shule ya upili na nimependana na mwanamume anayefanya kazi. Sasa ananishauri niache shule ili anioe na ametishia kuwa nikikataa atatafuta mwingine. Sitaki kumuacha na pia nathamini masomo. Nishauri tafadhali.

Kupitia SMS

Mapenzi yanaweza kukupumbaza ukose kuona wala kusikia, na nahisi yamekufika hapo. Kumbuka kuwa anayekwambia uache shule tayari amemaliza masomo na yuko sawa maishani. Ndoa haina mikataba, anaweza kukuoa na baadaye akuache. Itakuwaje? Jenga msingi wa maisha yako kwanza, mengine baadaye.