Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Shangazi, mpenzi wangu ana sponsa, nifanyeje?

September 19th, 2019 2 min read

Na SHANGAZI

SHIKAMOO shangazi! Natumai wewe ni mzima na ninahitaji ushauri wako katika ukumbi huu. Nimekuwa na mpenzi kwa miaka miwili sasa. Hata hivyo nimegundua kuwa ana uhusiano na mwanamume mwingine ambaye ana familia. Nimemuuliza na akaungama akisema kuwa amekuwa na uhusiano na mwanamume huyo tangu akiwa shuleni kwa sababu anamsaidia kugharamia mahitaji yake ya kifedha. Kusema kweli, sina uwezo wa kugharamia mahitaji yake ya kifedha. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Inaonekana kwamba mwanamke huyo anakupenda kwa dhati na ndiyo maana amekubali kuwa mpenzi wako ingawa huna uwezo wa kumsaidia kwa pesa. Hata hivyo, sidhani utakubali kuendelea na uhusiano huo ukijua wazi kuwa ana uhusiano wa pembeni na mwanamume mwingine kwa sababu ya pesa. Sababu ni kuwa atakapokuwa mke wako kisha ukose pesa za kumtimizia mahitaji yake atazitafuta kwa wanaume wengine.

 

Nilipokea simu ya mwanamume sasa hataki mambo nami

Hujambo shangazi? Nina mpenzi wangu ambaye nampenda kwa dhati. Hata hivyo, tulikosana hivi majuzi nilipopigiwa simu na mwanamume mwingine anayenitaka ingawa mimi sina haja naye. Nimempigia simu mpenzi wangu mara kadhaa nikitaka tuzungumze lakini anasisitiza kuwa uhusiano wetu umekwisha. Nifanyeje niweze kumsahau?

Kupitia SMS

Hiyo kamwe haiwezi kuwa sababu ya kutosha ya kukatiza uhusiano. Nahisi kama kwamba mwanamume huyo alikuwa anatafuta sababu yoyote ile ya kukutema na ndiyo maana unajaribu kumbembeleza lakini hataki. Huo sio mwisho wa maisha. Tulia na ushughulike na mambo mengine na hatimaye utamsahau.

 

Natamani turudiane

Kwako shangazi. Mwanamume ambaye tumekuwa wapenzi aliniacha majuzi bila sababu ya maana. Nampenda sana na natamani sana turudiane. Nimekuwa nikimpigia simu ananiambia bado ananipenda lakini nikimuomba tukutane anakataa. Je, ananichezea?

Kupitia SMS

Mwanamume huyo anakuchezea akili tu lakini wewe umefungwa macho na mapenzi uliyonayo kwake hutaki kuona hilo. Unasema kuwa alikuacha bila sababu na bado anakuhepa ingawa unajitahidi kumrudia. Hakuna haja ya kuendelea kuhangaika na kupoteza wakati wako kwa mtu ambaye hakutaki.

 

Penzi lilikuwa moto sasa simu hapokei na SMS pia hazijibu

Shangazi nina swali kwako. Nina mpenzi ambaye tumekuwa pamoja kwa muda wa miezi sita na amekuwa akinitimizia mahitaji yangu yote. Lakini naona amebadilika ghafla kwani nikimpigia simu hapokei na pia SMS hajibu. Sielewi kiini cha tabia yake hiyo. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Ni kawaida ya watu kubadili nia zao kuhusu mambo mbalimbali katika maisha yao. Hali kwamba mwenzako hataki tena kuwasiliana nawe ni dalili kuwa amebadili nia yake kuhusu uhusiano wenu na labda hataki kukwambia hivyo. Mpe muda usiozidi mwezi mmoja uone kama atawasiliana nawe na asipofanya hivyo ujue huo ndio mwisho wa uhusiano wenu.

 

Alimtongoza rafiki tukaachana na adai mimi ningali wake

Kwako shangazi. Niliachana na mwanamume mpenzi wangu nilipogundua alikuwa akimtongoza rafiki yangu wa karibu. Nililipata mwingine na tunapendana sana. Sasa ameanza kunipigia simu akisema mimi bado ni wake na hatakubali kunipoteza. Nahofia ataniharibia uhusiano wangu. Nishauri.

Kupitia SMS

Kama ulimuacha ilikuwa haki yako kufanya hivyo na hawezi kukulazimisha umpende. Kwa hivyo sikuelewi ukisema unahofia anaweza kuharibu uhusiano wako kwani mlikuwa wapenzi tu wala hukuwa mke wake. Akifikia hatua ya kutishia maisha yako mchukulie hatua ya kisheria.

 

Penzi gumu hili kwani hata simu hanipigii

Hujambo shangazi? Nina uhusiano na kijana fulani na ninampenda sana. Tatizo lake ni kwamba hataki kunipigia simu au kunitumia SMS. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Ni lazima mwenzako ana sababu ya kutotaka kuwasiliana nawe kwa simu. Kama hujawahi kumuuliza, ni muhimu ufanye hivyo ili ujue ni sababu gani hiyo ndipo ujue hatua ya kuchukua.