Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Sielewi ni kwa nini amekawia bila kuniomba penzi

March 13th, 2019 2 min read

Na SHANGAZI

HUJAMBO shangazi? Kuna mwanamume tunayefanya kazi pamoja ambaye ameteka moyo wangu kimapenzi. Tumekuwa marafiki wakubwa katika miaka miwili ambayo tumefanya kazi pamoja na nimekuwa nikitarajia kuwa atanidokezea hisia zake kwangu lakini bado sijaona dalili. Ninajua kwa hakika kuwa hajaoa na sielewi ni kwa nini amekawia kuniomba penzi ilhali niko tayari kwake. Nifanyeje?

Kupitia SMS

Kulingana na maelezo yako, ninaamini kwamba mwanamume huyo anakuchukulia kama rafiki mzuri tu, hana hisia kwako. Kama anakupenda angekuwa ashakwambia. Ukweli ni kwamba mwanamke na mwanamume wanaweza kuwa na uhusiano wa karibu sana lakini usio wa kimapenzi. Tafuta jinsi ya kumwelezea unavyohisi ili ujue msimamo wake.

 

Wanaosaka penzi hapa ni wa kweli?

Shikamoo shangazi. Kuna wanawake wengi ambao wamekuwa wakituma jumbe katika ukumbi huu wakisema wanatafuta wachumba. Je, unaweza kujua kwa hakika iwapo kweli huwa wanatafuta wachumba ama wanatumia ukumbi huu kuwalaghai wanaume?

Kupitia SMS

Wengi wa watu wanaotuma jumbe zao hapa huwa wana haja na ndiyo maana wanatumia wakati na pesa zao kutuma jumbe hizo. Hata hivyo, inawezekana kuna wachache wao wanaokuwa na nia mbaya. Ukweli ni kuwa siwezi kujua walio na nia njema na walio na nia mbaya. Ushauri wangu ni kuwa unafaa kuwa na tahadhari kuhusu mtu yeyote mgeni unayekutana naye kupitia safu hii na hata mahali kwingine hadi utakapoweza kumwamini.

 

Niwekeze moyo au napoteza muda tu?

Shikamoo shangazi. Mimi ni mwanafunzi wa shule ya upili na nina uhusiano na mwanafunzi mwenzangu. Nimejiunga na shule mwaka huu tu naye yuko mwaka wa mwisho. Tafadhali nishauri kuhusu iwapo tutaweza kuendelea ama ataniacha akimaliza shule.

Kupitia SMS

Ukweli ni kuwa uhusiano wenu huo ni haramu na mnafaa kuuvunja mara moja. Wazazi wenu waliwapeleka shuleni kusoma kwa maisha bora baadaye na mahusiano ya kimapenzi yanaweza kuvuruga masomo yenu. Kijana huyo anakuhadaa tu kwani hujui akimaliza shule ataenda wapi na atakuwa na nani. Zingatia masomo yako kwanza, mambo mengine baadaye.

 

Amenitema baada ya kumfungulia roho

Shikamoo shangazi. Nina umri wa miaka 23 na nimekuwa na uhusiano na mwanamume fulani kwa mwaka mmoja sasa. Hata hivyo, ameniacha majuzi nilipomwambia kuwa sie mpenzi wangu wa kwanza. Nimewahi kuwa na wengine wawili. Ninampenda sana na hatua yake hiyo imeniumiza sana moyoni. Nishauri.

Kupitia SMS

Kila mtu huwa na mambo fulani anayozingatia katika kumtafuta mchumba. Kulingana na maelezo yako, labda mwanamume huyo anatafuta mwanamke ambaye hajawahi kuwa na uhusiano na mwanamume mwingine na ndiyo maana amekuacha alipojua ulikuwa na wengine. Hiyo ni haki yake kwa hivyo hufai kumlaumu. Muelewe tu na na uondoe mawazo yako kwake uendelee na maisha yako.

 

Nahofia ataondoka aniachie mzigo wake

Shikamoo shangazi? Nimekuwa na uhusiano na mwanamume fulani kwa zaidi ya mwaka mmoja na huwa hatutumii kinga. Sasa mimi ni mjamzito na nimepata fununu kwamba ana mwingine. Nahofia anataka kuniachia mzigo. Naomba ushauri wako shangazi.

Kupitia SMS

Ulifanya makosa makubwa kukubali kubeba mimba bila mpango thabiti kati yako na mpenzi wako. Kama ulijua kwa hakika huna uwezo wa kulea mtoto, ungetumia kinga ili kuepuka mimba hiyo. Sasa umeona dalili za mwenye mimba kukuhepa umeanza kuhangaika. Hizo fununu ziwe za kweli au za uongo, mwanamume huyo akiamua kukuacha hutakuwa na budi ila kumlea mtoto. Jitayarishe kwa chochote kile.