Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Sili silali baada ya mpenzi kukataa kupokea simu

August 10th, 2019 2 min read

Na SHANGAZI

SHIKAMOO shangazi! Nina umri wa miaka 20 na nina uhusiano na kijana aliye na umri wa miaka 24. Tumekuwa pamoja kwa mwezi mmoja na hajawahi kunipeleka nyumbani kwao. Kwa wiki moja sasa sijamuona wala kuwasiliana naye kwani amekuwa akipuuza simu na SMS zangu. Mara ya mwisho tulipozungumza aliniambia amepata mpenzi mwingine. Nifanyeje?

Kupitia SMS

Inaonekana kuwa katika muda mfupi ambao mmekuwa pamoja, kijana huyo amehisi kuwa uhusiano wenu hautaenda mbali, labda kwa sababu hana hisia kwako ama kutokana na sababu zake nyingine. Hiyo ndiyo sababu ameamua kukatiza mapema uhusiano wenu badala ya kuendelea kukuharibia wakati. Kama yamekuwa hayo, usiwe na hofu, kwani hilo ni jambo la kawaida. Hatimaye utampata wako wa maisha.

 

Nimeamua kuolewa naye kama mke wa pili baada ya kumzalia 2

Mambo shangazi? Nina umri wa miaka 23 na nimependana na mwanamume wa miaka 40 ambaye ameoa. Mke wake ameshindwa kumpa watoto lakini mimi nimemzalia watoto wawili. Ninampenda sana na nimeamua kuolewa naye mke wa pili. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Unasema tayari umeamua kuolewa mke wa pili na mwanamume huyo kwa hivyo huhitaji ushauri wangu katika jambo hilo. Hata hivyo, kama mmekubaliana, itakuwa vyema akujengee kwako mbali na mkewe wa kwanza ili kuepuka ugomvi. Hali kwamba ameshindwa kumpa mumewe watoto ilhali wewe umemzalia inaweza kumfanya awe na kinyongo nawe.

 

Kipusa mpenzi wangu amehamishwa hadi shule ya mashambani

Shikamoo shangazi! Nimependana na mrembo fulani mwanafunzi wa shule ya upili. Mimi pia ninasoma shule ya upili na nimeamua kuwa wakati ukiwadia ndiye atakuwa mke wangu. Kwa bahati mbaya, juzi wazazi wake walimhamisha hadi shule nyingine mashambani. Tumekuwa tukiwasiliana kwa simu lakini nina hofu kwamba huko aliko anaweza kupata mpenzi mwingine mwenye penzi tamu kuliko langu. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Kwanza, mimi kamwe siungi mkono mahusiano ya kimapenzi kati ya wanafunzi. Kama kweli unathamini masomo yako na ya msichana huyo unayedai unampenda, katiza mara moja uhusiano huo hadi mmalize shule. Pili, hali ya mpenzi wako kuwa mbali nawe si hoja bora tu uhusiano wenu umejengwa katika msingi wa mapenzi ya dhati na uaminifu.

 

Sababu atamaliza shule mbele yangu hakika nina hofu tele

Kwako shangazi. Nina msichana mpenzi wangu ambaye anamaliza shule mwaka huu ilhali mimi ninamaliza mwaka ujao na tumekubaliana kuwa tutaoana. Hofu yangu ni kwamba anaweza kuniacha kwa msingi kwamba mimi bado ni mwanafunzi. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Huyo ni mpenzi wako tu wala si mke wako na ana haki ya kufanya uamuzi wowote anaotaka kuhusu uhusiano wenu. Kwa sasa itabidi uamini kuwa anakupenda na atasubiri hadi umalize masomo. Akiamua kukuacha hutakuwa na la kufanya ila kusalimu amri.

 

Nilipomtembelea kwao, aliramba lakini baada ya hapo hawasiliani nami

Vipi shangazi? Kuna kijana aliyedai ananipenda akiahidi kuwa atanioa. Aliniita kwake ili nione maisha anayoishi ili nikiridhika nikubali anioe. Siku hiyo alinishawishi nimpe mahaba na nikakubali. Tangu siku hiyo hajanipigia simu na ninaumwa sana moyoni kwa sababu nahisi alinitumia kukidhi haja yake tu. Nifanyaje?

Kupitia SMS

Ukweli ni kuwa kijana huyo alikuhadaa tu ili atomize haja yake ya muda huo tu wala hakuwa na mipango yoyote kuhusu ndoa kati yenu. Ndiyo maana hujamuona wala kumsikia tena. Ulikosea kumtimizia haja yake hiyo kabla hujamfahamu vyema kiasi ya kujua nia yake hasa. Kubali kuwa uliteleza na hilo litakuwa funzo muhimu kwako kuhusu wanaume.