Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Simpendi wala sina hisia kwake ila ataka kunioa

May 21st, 2019 2 min read

Na SHANGAZI

ZA kwako shangazi? Kuna mwanamume anayenipenda lakini mimi simpendi wala sina hata hisia kidogo kwake. Ajabu ni kwamba anasisitiza kuwa ni lazima atanioa. Je, nitawezaje kuishi na mtu nisiyempenda? Tafadhali nishauri.

Kupitia SMS

Sielewi unataka ushauri gani kutoka kwangu. Ukweli ni kwamba mwanamume huyo hawezi kukuoa kwa lazima. Kwake kufikia hatua ya kukuoa ni lazima kwanza muwe wapenzi, wachumba kisha mshauriane na kukubaliana kuhusu ndoa. Sasa unahangaika bure kuhusu maisha na mtu usiyempenda. Madai yake eti ni lazima atakuoa yanatokana na machungu aliyonayo kwa sababu umemkataa. Mpuuze na uendelee na maisha yako.

 

Ndoa ni ya miezI mitatu pekee na anataka mtoto

Hujambo shangazi? Nimeolewa kwa miezi mitatu pekee na bado sijapata mtoto. Mume wangu amezua ugomvi mara kadhaa akisema nimeshindwa kumpa mtoto. Nishauri tafadhali.

Kupitia SMS

Kusema kweli dada yangu haiwezekani kwa mwanamke kupata mtoto miezi mitatu katika ndoa. Hata mimba ya miezi mitatu haiwezi kuonekana kwa macho. Zungumza na mume wako umwambie awe na subira. Mkimaliza mwaka mmoja kabla hujapata mimba, basi mnaweza kutafuta ushauri wa kitaalamu hospitalini.

 

Nashuku anataka tu kunitumia aniteme

Za kwako shangazi? Nina umri wa miaka 22 na kuna kijana tunayependana ambaye ananiambia anataka kunioa. Lakini mimi nahisi kuwa hawezi kunioa bali anataka kunitumia tu. Nahitaji ushauri wako.

Kupitia SMS

Si kila uhusiano wa kimapenzi huishia katika ndoa. Inafika wakati unahisi kuwa mpenzi wako hakufai kwa ndoa na unalazimisha kukatiza uhusiano ili kumtafuta wako wa maisha. Ninaamini una sababu ya kuhisi kuwa kijana huyo hafai kuwa mume wako kwa hivyo fuata moyo wako na umwambie ukweli hata kama utakuwa mchungu kwake.

 

Sili silali baada ya kutenganishwa na mwanafunzi barafu ya nafsi yangu

Shikamoo shangazi! Natumai wewe u mzima. Nina umri wa miaka 17 na ninasomea shule ya upili. Kuna kijana tuliyekuwa wapenzi kwa miaka miwili hadi majuzi tu jamaa zangu walipoingilia uhusiano wetu wakanilazimisha nimuache wakidai ataniharibia masomo. Ninampenda kwa moyo wangu wote na siko tayari kumuacha. Nisaidie tafadhali.

Kupitia SMS

Hisia za mapenzi ya dhati huwa nzito sana na mara nyingine zinaweza kumsukuma mtu kufanya mambo bila kujali matokeo yake. Kuna watu ambao wamewahi kujitoa uhai kwa ajili ya mapenzi. Wewe ni msichana mdogo tena bado unasoma. Tafadhali nakusihi uwasilikize na kuwaelewa jamaa zako kwa sababu wanayokwambia ni ya kweli. Mapenzi na masomo kamwe hayatangamani. Pili, masomo ni ya muda tu ilhali mapenzi hayana wakati bali yapo leo, kesho na milele.

 

Barua ya kibinti imenivuruga akili

Shikamoo shangazi! Mimi ni mwanafunzi wa shule ya upili. Kuna msichana ambaye ameniandikia barua akiomba tuwe wapenzi. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Mwambie kuwa wewe bado ni mwanafunzi na kwamba jambo muhimu zaidi kwako sasa ni masomo yako. Kama anakupenda asubiri hadi ukamilishe hatua hiyo yako kielimu.

Mwanamume ninayempenda ghafla ameanza kunionyesha madharau

Za kwako shangazi? Nina mwanamume mpenzi wangu ninayempenda kwa dhati lakini nimeanza kupoteza matumaini katika uhusiano wetu. Sababu ni kwamba kila anaponikosea nikimuuliza huwa mkali tena kwa matusi. Hivi ninapokuandikia ujumbe huu amesusia kuja kwangu na pia amenizima kwa simu yake hivi kwamba siwezi kumpigia. Nifanyeje?

Kupitia SMS

Ingawa unamuita mwanamume huyo mpenzi wako, mimi nahisi kuwa hana haja nawe ila unajipendekeza kwake tu. Uhusiano uliofikia kiwango cha mtu kumtusi mwenzake na kumzima kumpigia simu hauwezi kwenda popote. Kama una haja sana ya mapenzi, nakushauri uachane na mwanamume huyo uyatafute kwingine.