Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Simtaki huyu wa familia ila akinipigia tu nabadili wazo

September 25th, 2019 2 min read

Na SHANGAZI

VIPI shangazi? Nina umri wa miaka 22 na nina mtoto mmoja ingawa sijaolewa. Nimependana na mwanamume ambaye ana familia. Amekuwa akitaka kunioa mke wa pili lakini mimi sitaki kwa sababu ninaamini ninaweza kupata mume wangu mwenyewe. Nimejaribu mara kadhaa kumtoa katika mawazo yangu lakini kila akinipigia simu tu, hisia zake hunasa mawazo yangu tena. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Kulingana na umri wako, wewe bado ni mwanamke mchanga na unaweza kumpata mume wako mwenyewe badala ya kupoteza wakati na mtu aliye na familia ilhali umeamua kuwa huwezi kuolewa mke wa pili. Kama kweli unataka kujiondoa katika uhusiano huo, ni lazima ukate kauli hiyo kwa moyo mmoja. Epuka kabisa sehemu mnazoweza kukutana na pia ukatize mawasiliano naye kwa kubadilisha nambari yako ya simu. Ni kwa njia hiyo tu ambapo utaweza kumuondoa katika maisha yako.

 

Natafuta mwaminifu nimuoe, je nitapata?

Shikamoo shangazi! Mimi ni mwanamume mwenye umri wa miaka 27. Sina mpenzi na natafuta mwanamke mwaminifu kwa uhusiano wa kimapenzi kisha nimuoe baadaye tuishi pamoja. Je, ninaweza kumpata?

Kupitia SMS

Bila shaka unaweza kumpata mwanamke mwenye sifa unazotaka. Hata hivyo, nakushauri uwe na subira unapomtafuta kwa sababu siku hizi kuna walaghai wengi wa kimapenzi miongoni mwetu.

 

Mpenzi ataka kunitupa baada ya rafiki yake kunichongea kwake

Kwako shangazi. Nina uhusiano na mwanamume ninayempenda sana naye pia ninajua ananipenda. Lakini hivi majuzi tulikosana baada ya mmoja wa marafiki zake kumwambia eti mimi ni mpenzi wake. Ukweli ni kuwa mwanamume huyo amekuwa akinitaka lakini nimemkataa. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Ni jambo la kushangaza kwamba mpenzi wako anamwamini rafiki yake huyo kuliko wewe. Inaonekana kuwa mwanamume huyo ameamua kuvuruga uhusiano wenu kwa sababu umemkataa. Ninaamini unachelea kumwambia hayo mpenzi wako kwa sababu hutaki wakosane. Kwa kuwa ameamua kuvunja uhusiano wenu, wewe pia hufai kumhurumia. Mwambie mpenzi wako nia ya rafiki yake kwako, liwalo liwe.

 

Tumekuwa tukitumia kinga lakini sasa yeye anahisi nina mimba, miye najua bado sina

Shikamoo shangazi! Huu ni mwaka wa pili nikiwa katika uhusiano na mwanamume tunayependana sana. Kwa muda wote huo, tumekuwa tukifurahia burudani ila kwa kutumia kinga. Ajabu ni kuwa mwenzangu ameanza kushuku kuwa nina mimba na anasisitiza kuwa haiwezi kuwa yake kwa sababu tunatumia kinga. Mimi ninajua kwa hakika kwamba sina mimba. Nimemwambia hivyo lakini haniamini. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Naona nyinyi wawili mnagombana kuhusu jambo ambalo ni rahisi sana kusuluhisha. Kama mpenzi wako anaamini una mimba nawe unajua huna, ambatana naye hadi hospitalini ama kituo kingine chochote cha kimatibabu ili upimwe. Matokeo ya ukaguzi huo yatamaliza ubishi kati yenu.

 

Nimempa mimba sasa amefukuzwa kwao nami sina kazi

Vipi shangazi? Nina shida kubwa na ninahitaji ushauri wako tafadhali. Nimempa mimba msichana mpenzi wangu. Sijui nitafanya nini kwa sababu mapato ya kazi yangu ni kidogo hata sina nyumba, ninaishi na ndugu yangu. Wazazi wake wamemfukuza kwao wakamwambia aende kwa aliyempa mimba. Kwa sasa anaishi na dada yake mjini. Tafadhali nisaidie.

Kupitia SMS

Hali yako hiyo ni sawa na mwiba wa kujidunga kwa hivyo mimi sitakwambia pole wala sina msaada wowote kwako. Sababu ni kuwa ulijiingiza mwenyewe katika uhusiano huo ukijua hali yako ya mapato. Pili, umekuwa ukishiriki mapenzi na msichana huyo bila kinga ukijua vyema kwamba kuna hatari yake kupata mimba na hilo limetokea. Huo ni mzigo wako, tafuta namna ya kuubeba.