Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Simu yake imejaa jumbe za wanawake, ananisaliti?

August 27th, 2019 2 min read

Na SHANGAZI

HUJAMBO shangazi? Nina umri wa miaka 25 na nimekuwa katika ndoa kwa mwaka mmoja sasa. Kuna jambo moja ambalo linanitia wasiwasi kuhusu mume wangu. Kila nikikagua simu yake ninapata jumbe nyingi za majadiliano kati yake na wanawake wengine. Nampenda sana na nitavunjika moyo sana nikijua ana uhusiano nje ya ndoa. Nishauri.

Kupitia SMS

Kulingana na maelezo yako ni kwamba unamshuku tu mume wako kwa kuwasiliana kwa simu na wanawake wengine wala huna ushahidi kuwa ana uhusiano nao. Inawezekana kuwa hao ni marafiki tu hana nia mbaya kwao. Hali kwamba amekuoa haina maana kuwa hawezi kuwa na marafiki wa kile. Hata hivyo, ni muhimu umwelezee unavyohisi ili mshauriane.

 

Jumbe za mapenzi kwa simu yake zanitia hofu sana

Kwako shangazi. Nina mwanamume mpenzi wangu lakini simwamini. Sababu ni kuwa kuna siku nilipata katika simu yake ujumbe wa kimapenzi kutoka kwa msichana mwingine. Nilipomuuliza alidai msichana huyo ni rafiki tu na amezoea kumchezea namna hiyo. Nina wasiwasi, naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Kama ujumbe huo ulikuwa wa kimapenzi na anadai ulitokana na mazoea kati yake na msichana huyo, basi una sababu ya kuwa na wasiwasi. Amekubali mwenyewe kuwa wamekuwa wakiwasiliana kwa njia hiyo na hiyo ina maana kwamba ni wapenzi ingawa hataki kukwambia hivyo. Haina haja uendelee kuwa katika uhusiano huo ukijua kuwa anayedai kuwa mpenzi wako ana mwingine.

 

Tunapendana ila yeye hanijali kabisa

Hujambo shangazi? Nina uhusiano na kijana fulani na ninampenda sana. Tatizo lake ni kwamba huwa hapendi kunipigia simu au kunitumia SMS kunijulia hali. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Ni lazima mwenzako ana sababu ya kutotaka kuwasiliana nawe kwa simu. Kama hujawahi kumuuliza, ni muhimu ufanye hivyo ili ujue ni sababu gani hiyo ndipo ujue hatua ya kuchukua.

 

Anadai tuwe marafiki tu lakini mimi nataka mapenzi si urafiki

Kwako shangazi. Nilikuwa na mpenzi lakini tukaachana kutokana na tofauti ndogo. Sasa ni mwaka mmoja tangu tuachane na alimwambia rafiki yangu kuwa amepata mwingine. Hata hivyo, amekuwa akimtuma kwangu akisema anataka tuwe marafiki tu. Bado nampenda na sitaki urafiki bali mapenzi. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Sielewi ni kwa nini mwanamke huyo anakufuata kupitia kwa rafiki yako akitaka muwe marafiki ilhali anadai ameshapata mchumba. Kuna uwezekano mkubwa kwamba hana mchumba na anatumia hiyo kama mbinu ya kutaka kujua kama bado unampenda. Kwa kuwa unasema kuwa bado unampenda, ushauri wangu ni kuwa ukubali tu huo urafiki unaotaka na ninaamini muda si mrefu atakwambia ukweli na utamtia tena mikononi mwako.

 

Mke wangu ameanza kujisongeza karibu na wanaume wenye vyeo anakofanya kazi

Hujambo shangazi? Nimeoa na tumejaliwa watoto wawili. Mke ameajiriwa ilhali mimi ninafanya biashara. Nina ushahidi wa kutosha kuwa mke wangu amekuwa akijaribu kuanzisha uhusiano na wanaume wakubwa katika mahali anakofanya kazi. Nimemuuliza nia yake hasa na ameanza kulalamika eti ninataka kumkosanisha na wakubwa wake. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Hujaelezea una ushahidi gani kuhusu jambo hilo. Iwapo kweli umethibitisha kuwa hiyo ndiyo tabia ya mke wako mahali anakofanya kazi, nahofia ndoa yenu. Sababu ni kuwa si wanaume wengi walio na maadili ya kikazi na kuna uwezekano mkubwa kuwa anaowatafuta watatumbukia katika mtego wake. Ndoa ni muhimu kuliko kazi na iwapo unaweza kumtimizia mahitaji yake akiwa nyumbani, ni heri umuachishe kazi ili kukinga ndoa yenu.