Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Sina uwezo wa kuzaa tena, niweke siri?

June 7th, 2019 2 min read

Na SHANGAZI

KWAKO shangazi. Mume wangu tuliyezaa mtoto pamoja aliniacha alipogundua kuwa siwezi kupata watoto zaidi kisha akamchukua mtoto wetu. Kuna mwanamume mwingine anayenitaka na natamani sana kuolewa tena. Je, niwaambie ukweli ama niweke hiyo kuwa siri yangu?

Kupitia SMS

Inawezekana kuwa mwanamume anayekutaka anakupenda kwa dhati na ana nia ya kukuoa. Hata hivyo, kumbuka kuwa watu hufunga ndoa kwa ajili ya kupata watoto ingawa si wote. Ni muhimu umwambie ukweli ili afanye uamuzi wake akijua hali yako.

 

Sioni dalili ya kupata asali, ananichezea?

Kwako shangazi. Nimekuwa na mpenzi kwa mwaka mmoja sasa lakini bado sijaonja asali. Kila nikiuliza huniambia nisijali niendelee kusubiri. Ananichezea?

Kupitia SMS

Sielewi una haraka ya nini kwani mwaka mmoja ni muda mfupi sana na mwenzako bado anakupa matumaini. Pili, hiyo asali si haki yako kwa sababu wenu ni uhusiano tu wala si ndoa. Ukiweka tamaa mbele utaambulia patupu.

 

Nasikia mpenziwe wa kitambo ana virusi

Hujambo shangazi? Kuna mwanamke ambaye tumekuwa wapenzi kwa karibu mwaka mmoja sasa na ninampenda sana. Lakini nimeingiwa na hofu baada ya kupata fununu kuwa mwanamume aliyekuwa mpenzi wake ana virusi. Sasa ninahofia mimi pia nimeambukizwa. Nishauri.

Kupitia SMS

Hakuna jinsi unavyoweza kujua kwa hakika kuwa mwanamke huyo pia anaugua ugonjwa huo. Ushauri wangu ni kwamba upimwe ili ujue iwapo umeambukizwa au la. Ukigundua kweli umeambukizwa utashauriwa pamoja na mwenzako kuhusu jinsi ya kuishi na hali hiyo.

 

Mwalimu asisitiza miye pekee ndiye wake

Vipi shangazi? Mimi ni mwanafunzi wa shule ya upili na nina uhusiano wa kimapenzi na mwalimu wangu. Nimepata fununu kuwa mwalimu huyo ana uhusiano na mwanafunzi mwenzangu lakini nikimuuliza anakana akisema mimi pekee ndiye wake. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Ni makosa makubwa tena ni haramu kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mwalimu wako. Sielewi jinsi ambavyo utaweza kuzingatia masomo yako mmoja wa walimu wako akiwa mpenzi wako. Kumbuka kuwa mwalimu wako tayari ashamaliza masomo yake na sasa anafanya kazi. Isitoshe, unasema kuwa ana uhusiano na mwanafunzi mwenzako kwa hivyo ni wazi kuwa nia yake ni kuwatumia. Wazazi wako wakijua utakuwa mashakani. Vunja uhusiano huo mara moja.

 

Sijui kutoa mistari

Hujambo shangazi? Nina umri wa miaka 21. Natamani sana kuwa na mpenzi lakini nina shida ya kuzungumza na wasichana. Kuna wengi ambao wamenionyesha hisia za kunipenda lakini ninashindwa nitaanzia wapi. Tafadhali nishauri.

Kupitia SMS

Hakuna kazi rahisi kama kumnasa mwanamke ambaye tayari amekuonyesha kuwa anakupenda. Unachohitaji ni wewe pia kumwelezea hisia zako kwake na papo hapo ataingia mikononi mwako. Iwapo unadhani msichana atakuja kwako nyumbani akwambie anakupenda utaendelea kungojea.

 

Kumbe amekuwa na wa pembeni miaka yote

Shikamoo shangazi! Nina umri wa miaka 26 na nilimaliza masomo ya chuo kikuu majuzi tu. Sasa nimegundua kuwa mwanamume ambaye tumekuwa wapenzi tangu tukiwa shule ya upili amekuwa na mpenzi mwingine wa pembeni kwa muda wote huo. Yeye mwenyewe ameungama huku akiniomba msamaha na kuahidi kuwa atamuacha. Nahitaji ushauri wako.

Kupitia SMS

Ni jambo la kuvunja moyo sana kugundua kuwa mtu ambaye umempa moyo wako amekuwa akikuhadaa kwa miaka yote hiyo. Ukweli ni kwamba kitendo chake hicho kimetia doa uhusiano wenu. Isitoshe, hutakuwa na hakika kwamba ataacha tabia yake hiyo. Ningekuwa wewe ningemtema mara moja.