Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Sitaki kumueleza nina mke akaja akanitoroka!

February 14th, 2020 2 min read

Na SHANGAZI

KWAKO shangazi. Mimi nina mke na tuna mtoto. Kuna mwanamke mwingine ambaye nampenda naye pia ameniambia ananipenda. Aliniambia alikuwa na mpenzi lakini akamuacha alipogundua alikuwa na uhusiano na msichana mwingine tena akampa mimba. Sasa sitaki kumwambia kuwa nina mke kwa sababu ninajua ataniacha. Nishauri.

Kupitia SMS

Nashangaa kwamba unataka nikushauri kuhusu jinsi unaweza kumsaliti kimapenzi mke wako wa ndoa. Kamwe siwezi. Wewe ni mume wa mtu na unafaa kuheshimu ndoa yako na mke wako. Unajua kuwa unaongozwa na tamaa na unataka tu kumtumia mwanamke huyo kisha umteme. Hata usipomwambia sasa kuwa una mke, hatimaye atajua na atakuacha. Nakuonya tena, heshimu ndoa yako na utulie kwa mke wako.

 

Alinitoroka akaolewa na mwingine sasa hataki hata nione watoto wetu

Kwako shangazi. Nilikuwa nimeoa lakini mke wangu akaniacha nilipogundua alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na mwanamume mwingine. Muda si mrefu aliolewa na mwanamume huyo. Lakini waliachana majuzi na sasa yuko kwao. Tatizo ni kuwa amenikataza kabisa kuwaona au kuwasiliana na watoto ambao tulizaa pamoja. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Kama ameachana na mwanamume aliyemuoa na sasa yuko kwao, hana sababu ya kukuzuia kuwaona au kuwasiliana na watoto wenu kwa sababu hiyo ni haki yako. Ushauri wangu ni kuwa utumie utaratibu wa kisheria kupitia mahakamani ili upate rasmi ruhusa ya kuwaona watoto wako.

 

Alinipachika mimba akanitema sasa sijui kama nikubali wale wanaoniandama?

Shikamoo shangazi! Nilikuwa na mwanamume mpenzi wangu niliyempenda kwa dhati. Hatimaye alinihadaa akanipa mimba kisha akanitema. Wazazi wangu walikuwa wamenionya niachane naye lakini nikawapuuza. Sasa sina amani kabisa kwani hawanitaki mimi na mtoto wangu nyumbani kwao sijui nitaenda wapi. Kuna wanaume kadhaa ambao wamekuwa wakinitaka lakini nimewakataa kwa hofu kuwa watanitendea aliyonitendea mpenzi wangu. Nishauri.

Kupitia SMS

Ni kweli ulikosea, sio tu wazazi wako, bali kwako wewe mwenyewe, kwa kuzaa kabla hujaolewa. Hata hivyo, si vyema kwa wazazi wako kukutenga kwani hakuna binadamu asiyekosea. Kama kuna wanaume wanaokutaka, chagua mmoja wao ambaye unahisi ana mapenzi ya dhati kwako na ambaye yuko tayari kukuoa.

 

Nampenda lakini siko tayari kulea mtoto aliyezaa nje, nishauri

Shangazi ni matumaini yangu kuwa wewe ni mzima. Nimevutiwa kimahaba na mwanamke tunayesoma pamoja chuo kikuu. Juzi nilimdokezea hisia zangu kwake na akakubali. Katika ile hali ya kufahamiana vizuri, niligundua kuwa ana mtoto aliyemzaa akiwa shule ya upili. Nampenda sana mwanamke huyo lakini sijui nitafanya nini kwa sababu siko tayari kuwa baba ya mtoto ambaye si wangu. Nishauri.

Kupitia SMS

Kama unajua huwezi kumuoa mwanamke huyo, usimdanganye bali mwambie ukweli. Usikubali kuongozwa na tamaa umdanganye na kumtumia ukijua vizuri kwamba hawezi kuwa mke wako.

 

Simuelewi kabisa huyu mwanamume sijui ananipenda au hanipendi?

Kwako shangazi. Nilipendana na mwanamume fulani na baada ya miezi mitano akaniambia eti mpenzi wake wa awali anamlazimisha warudiane. Aliniambia hamtaki ananipenda mimi. Aliniomba msamaha pia kwa sababu huyo mpenzi wake alinitusi vibaya kwa simu. Tangu wakati huo mpenzi wangu amepunguza mawasiliano, hanipigii simu kama awali na mara nyingi nikimpigia hapokei na akipokea hudai kuwa bado ananipenda. Je, ananipenda au ananichezea akili?

Kupitia SMS

Inaonekana mwanaume huyo alikuhadaa mkaanza uhusiano akijua vizuri kuwa alikuwa na mwingine. Ingawa hujaelezea, huenda alipata alichotaka kwako kisha akaamua kuhepa kwa madai eti mpenzi wake wa awali amerudi kwa lazima. Tangu lini mtu akalazimisha mwingine kumpenda? Isitoshe, amekatiza mawasiliano. Huyo anakuchezea tu, achana naye.