Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Tangu nijifungue majuzi mume halali nyumbani

March 15th, 2019 2 min read

Na SHANGAZI

SHIKAMOO shangazi! Huu ni mwaka wangu wa pili tangu niolewe na nilipata mtoto wangu wa kwanza wiki tatu zilizopita. Tangu nijifungue, mume wangu amekuwa akilala kazini kwa madai eti amepangiwa zamu ya usiku kwa muda wote huo mfulululizo. Ajabu ni kuwa hajawahi kufanya kazi usiku tangu tujuane. Ninashuku ana mpango wa kando na amekuwa akilala kwake. Nishauri.

Kupitia SMS

Sitaki kukuchochea, lakini nahisi kuna jambo fulani ambalo mume wako anakuficha na kwamba madai yake ni kisingizio tu. Kama hajawahi kupangiwa kazi ya usiku katika miaka miwili ambayo mmeishi pamoja, basi hapo kuna maswali. Isitoshe, hata wanaokuwa na zamu za usiku hupewa siku za kupumzika. Sijawahi kuona wala kusikia mtu amepangiwa kufanya kazi wiki tatu mfululizo. Ushauri wangu ni kwamba umkabili umuulize na ikibidi uende huko kazini kwao ili ujue ukweli wa jambo hilo.

 

Tulikosana akarudi kwao, wazazi wangu hawataki arejee

Kwako shangazi. Nilikosana na mke wangu tuliyekuwa tumeishi pamoja kwa miaka mitatu na akarudi kwao. Amekuwa akitaka turudiane lakini wazazi wangu wanakataa na badala yake wanataka nimuoe mwanamke jirani yetu ambaye tumekuwa marafiki. Mimi bado nampenda mke wangu. Nipe ushauri.

Kupitia SMS

Nijuavyo ni kwamba mwanamume huoa mke kwa manufaa yake mwenyewe wala si kwa manufaa ya wazazi wala jamaa zake. Kwa sababu hiyo ana haki ya kuchagua anayempenda na hafai kuingiliwa na mtu yeyote yule. Usikubali kulazimishwa na wazazi kuoa mwanamke usiyempenda. Shikilia msimamo wako na ufanye mipango umchukue mke wako kutoka kwao.

 

Nahangaika kwa kuota ndoto mbaya

Shikamoo shangazi. Nina umri wa miaka 21 na ninasoma katika chuo kikuu. Sielewi ni kitu gani kinachoendelea maishani mwangu kwani katika siku za hivi majuzi nimekuwa nikiota ndoto mbaya za kutisha karibu kila siku. Mara nyingi ninalazimika kukaa macho nikihofia kuota ndoto hizo na hali hiyo inaathiri masomo yangu. Sijamwambia mtu yeyote. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Ingawa watu huota ndoto mbaya wakati fulani maishani, si hali ya kawaida kwa ndoto za aina hiyo kuwa jambo la kila siku. Ni muhimu uwalezee jamaa zako na kama wewe ni mfuasi wa dini utafute msaada kutoka kwa viongozi wako wa kidini.

 

Mwanangu wa kambo ananisumbua eti tuwe wapenzi

Shikamoo shangazi? Kuna jambo fulani ambalo linanitatiza na nakuomba unisaidie kutatua. Nina umri wa miaka 32 na niliolewa mke wa pili hivi majuzi. Sasa kijana wa mume wangu ambaye ana umri wa miaka 25 amekuwa akiniandama akitaka tuwe na uhusiano wa pembeni. Nimemkanya vikali anikome lakini hasikii na nahofia nikimwambia baba yake watakosana vibaya. Nifanyeje?

Kupitia SMS

Sielewi kijana huyo ametoa wapi ujasiri wa kukutongoza ilhali wewe ni mama yake hata kama si wewe uliyemzaa. Ni lazima utafute namna ya kumkomesha la sivyo ataendelea kukusumbua. Mwambie wazi kwamba asipoachana nawe utamshtaki kwa baba yake. Asiposikia, basi mwambie baba yake, liwe liwalo, bora upate amani katika ndoa yako.

 

Nimeanza kuogopa mchumba wangu kutokana na ukali

Hujambo shangazi? Nina kijana tunayependana kwa dhati na natamani awe wangu maishani. Tatizo pekee ni kwamba nikimkosea huwa mkali sana na nimeanza kumuogopa. Sijui maisha yetu yatakuwaje atakaponioa. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Kama tayari anakuonyesha ukali hata unamuogopa ilhali nyinyi bado ni wapenzi, nahisi kutakuwa na shida utakapokuwa mke wake. Itabidi uchukue hatua inayofaa kabla hamjaenda mbali.