Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Tuliachana kwa uzembe wake lakini bado nampenda…

December 4th, 2019 2 min read

Na SHANGAZI

VIPI shangazi? Nilikuwa nimeolewa lakini nikamuacha mume wangu kwa sababu ya uzembe, hakutaka kuwajibika hata kulea mtoto tuliyezaa pamoja. Tulikuwa tunaishi kwangu kwa hivyo alirudi kwao na anaishi nyumbani kwa mama yake pamoja na dada zake wawili. Hapendi kabisa kuchoka na mama yake anampendekeza sana kwa sababu ndiye kijana wake pekee. Amekuwa akinishawishi turudiane lakini nachukia hali yake hiyo ingawa nampenda. Nifanyeje?

Kupitia SMS

Ninaamini kwamba mwanaume kamili ni yule anayefahamu na kutekeleza majukumu yake kwa mke na watoto wake. Uzembe hauna nafasi kabisa maishani. Iwapo unampenda na anataka mrudiane, mwambie kwamba ni lazima ajirekebishe. Mwambie atoke katika nyumba ya mama yake atafute kwake na awe tayari kusghulikia familia yake. Kama hayo hataweza, ina maana hakufai na itakuwa heri utafute mwingine iwapo unatamani kuwa na mume.

 

Mpenzi hapendi tukutane faraghani

Shangazi nina mpenzi na ninaamini ananipenda. Ajabu ni kwamba huwa hataki kabisa tukutane faraghani. Kila tukipanga aje nyumbani kwangu siku hiyo ikikaribia yeye hupangua kwa kunipa visingizio. Simuelewi kabisa, naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Hilo linategemea muda ambao mmejuana. Tabia ya mpenzi wako ni dalili kuwa hajakufahamu vizuri kiasi cha kukutana nawe faraghani. Ushauri wangu ni kwamba umpeleke taratibu hadi atakapohisi kuwa salama mikononi mwako mkiwa wawili.

 

Fununu mchumba amepata wa kando zanipa kichefuchefu

Shikamoo shangazi! Nimetumwa kazi mji tofauti na anakoishi mwanamke mpenzi wangu. Nimepata habari kutoka kwa marafiki zangu kuwa ameshikana na mwanamume mwingine. Habari hizo zimenichafua moyo ingawa sina hakika. Nishauri.

Kupitia SMS

Kuna mambo ya kuambiwa na kuna ukweli. Utakosea kwa kuamini unayoambiwa na marafiki zako kumhusu mpenzi wako. Jambo la kufanya ni kuchunguza mwenyewe ujue ukweli badala ya kuchafuka moyo kutokana na uvumi. Kumbuka kuwa si marafiki wako wote wanaokutakia mema.

 

Naomba kukutana nawe shangazi ana kwa ana

Shikamoo shangazi! Kuna mambo ya kibinafsi ambayo nataka unishauri kuyahusu moja kwa moja badala ya kuyazungumzia katika ukumbi wako huu kwa sababu naona aibu kuyaanika hapa. Je, inawezekana tunaweza kukutana ama unitumie nambari yako ya simu nikupigie?

Kupitia SMS

Hatuwezi kukutana wala kuzungumza kwa simu. Ninashughulikia masuala yoyote katika ukumbi huu kwa manufaa ya wanaoyatuma na wasomaji wengine. Pili, unaweza kuuliza kuhusu jambo lolote la kibinafsi bila hofu kwani si lazima ujitambulishe kwa jina wala sihifadhi nambari za simu za wanaotaka ushauri.

 

Nahisi familia ya mke inanitumia vibaya

Vipi shangazi? Mimi nimeoa na tumejaliwa mtoto mmoja. Tatizo ni kwamba jamaa wa mke wangu wamekuwa mzigo kwangu. Wazazi, ndugu na dada zake wamekuwa wakielekeza kwangu mahitaji yao ya pesa. Nawaheshimu kama wakwe zangu lakini nahisi kwamba wananitumia vibaya. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Natumai kuwa umekuwa ukimlipia mahari mke wako kuambatana na makubaliano kati yako na wazazi wake. Kama ndivyo, tabia yao hiyo si nzuri na hata inaweza kusababisha migongano kati yako na mke wako. Kama mke wako ana hisia sawa na zako kuhusu jamaa zake, unaweza kumtuma ashauriane nao kuhusu suala hilo.

 

Nina uhusiano wa kimapenzi na bosi sasa amekuwa kero

Shikamoo shangazi! Niliajiriwa mwaka uliopita na nikaanzisha uhusiano na bosi wangu ingawa ana familia. Sasa hataki kuona nikizungumza na mwanamume mwingine yeyote na nahisi hali ikiendelea hivyo atanifuta kazi. Nifanyeje?

Kupitia SMS

Ulifanya makosa kukubali uhusiano na bosi wako ilhali unajua ana familia. Sasa amekushika mateka, kazi yako inategemea uhusino wenu. Ukiamua kumuacha uwe tayari pia kuacha kazi kwani atakufuta tu.