Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Tuliyeachana kisha tukarudiana hataki tupimwe

January 8th, 2020 2 min read

Na SHANGAZI

VIPI shangazi? Nilikuwa na mpenzi lakini akaniacha akashikana na mwanamume mwingine. Uhusiano wao umechukua miezi mitatu tu na sasa wameachana. Juzi aliniomba tukutane ambapo alijuta kwa kuniacha na kuniomba turudiane. Niliamua kumpa nafasi nyingine kwa sababu sijapata mwingine na bado nampenda. Kinachonishangaza ni kwamba nimependekeza twende tukapimwe tujue hali yetu lakini amekataa. Nishauri.

Kupitia SMS

Hatua yako ya kumkubali tena mwanamke huyo licha ya kukuacha kwa ajili ya mwanamume mwingine ni thibitisho kwamba unampenda kwa dhati. Pili, pendekezo lako kwake ni hatua muhimu ya tahadhari ambayo imekuwa kawaida siku hizi na sielewi ni kwa nini analikataa. Isitoshe, ni yeye aliyeomba kurudi kwako kwa hivyo anafaa kukubali masharti unayompa. Kwake kukataa ni ishara kuwa anashuku hali yake. Shikilia msimamo wako, akikataa basi achana naye. Afya yako ni muhimu kuliko mapenzi.

 

Uraibu wa pombe unatishia kuvunja familia yangu, sijui njia ya kujiokoa

Habari yako shangazi. Mimi ni mwanamume mwenye umri wa miaka 32 na nina familia. Tatizo langu ni kuwa nimeanza kulemewa sana na pombe kiasi kwamba ninashindwa kukimu familia yangu ipasavyo. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Bila shaka unaelewa kuwa familia yako ni muhimu kuliko starehe zako binafsi. Pombe haina manufaa yoyote kwa afya yako. Itabidi utahadhari sana kwa sababu ulevi wa kupindukia huanza hivyo na ni hatari kwa familia. Iwapo kweli unajali familia yako, fanya uamuzi wa busara sasa kwa kuacha pombe.

 

Ninapiganiwa sana na wasichana ilhali sijawa tayari miye

Hujambo shangazi? Nina umri wa miaka 22 na mimi ni mwanafunzi wa chuo kikuu. Sielewi ni kitu gani wanawake wameona kwangu. Wamekuwa wakiniandama wakitaka penzi langu hata hawanipi nafasi ya kupumua. Mimi bado sijaamua kuwa na mpenzi, nahofia kutumbukia katika ushawishi wao. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Ni jambo la kushangaza kwamba unalalamika kwa kupendwa ilhali kuna wenzako ambao wamekosa wa kuwapenda. Wengine wamejitoa uhai kwa kukataliwa. Unafaa kuchukulia hiyo kuwa bahati yako. Utakapoamua kuwa na mpenzi itakuwa mteremko kwako kwani utachagua mmoja kati ya wengi wanaokuandama. Lakini usiwaone wanakupigania ukawa mjeuri kwao. Wanaweza kukutoroka ushindwe kumpata hata mmoja wao. Kuwa mpole kwa kila mmoja wao. Umwambie wakati wako bado, ukiwadia utazingatia ombi lake.

 

Aliyezaa na mpenzi wake wa kike sasa anataka kunioa mimi

Hujambo shangazi? Kuna mwanamume ambaye tunapendana sana lakini nimegundua alizaa mtoto na mwanamke aliyekuwa mpenzi wake ingawa waliachana. Ameahidi kunioa lakini jambo hilo limeniingiza baridi. Tafadhali nishauri.

Kupitia SMS

Sidhani una sababu ya kuwa na wasiwasi kwa sababu wawili hao waliachana hata baada ya kuzaa mtoto pamoja. Mwanamke huyo alikuwa mpenzi wake tu, hakuwa mke wake. Hata mtu huachana na mke wake wakiwa na watoto na kuoa mwingine. Kama unampenda, hilo lisikutie hofu.

 

Walimu na wavulana shuleni ninakosoma hawaniachi hata kidogo japo siwataki

Shikamoo shangazi! Mimi ni msichana mwanafunzi wa shule ya upili. Kuna shida ambayo ninataka unitatulie. Baadhi ya walimu wangu wa kiume na wanafunzi wenzangu wamekuwa wakinifuata wakitaka tuwe wapenzi. Nimewaambia sitaki lakini hawataki kunisikia. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Hiyo ni changamoto kubwa kwa wasichana kama wewe walio na msimamo mkali kuhusu wanachotaka maishani. Nitakwambia ukweli, kwamba wanaume wataendelea kukuandama maishani na huwezi kuwazuia. Hata hivyo, usikubali kabisa kuwapa nafasi. Shikilia msimamo wako huo hadi utakapomaliza masomo na kuwa tayari kwa uhusiano ndipo uchague mwenyewe anayekufaa.