Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Tumekuwa pamoja kwa mwaka ila naona simpendi

September 26th, 2019 2 min read

Na SHANGAZI

KWAKO shangazi. Kuna mwanamke ambaye tumekuwa na uhusiano wa kimapenzi kwa karibu mwaka mmoja sasa ingawa mimi simpendi. Kisa ni kwamba alikuja kwangu mwenyewe akaniambia ananipenda na nikakubali kwa sababu sikuwa na mpenzi. Isitoshe, aliahidi kuwa atakuwa akinipakulia asali kila ninapoihitaji na kusema kweli hajanivunja moyo katika hilo. Sasa nataka kutafuta mpenzi wa dhati na sijui nitamwambia nini kwa sababu anaamimi kuwa nampenda. Tafadhali nishauri.

Kupitia SMS

Kupitia kwa maelezo yako, unaungama kwamba ulimhadaa mwanamke huyo kwamba unampenda ili umtumie tu. Sasa umemtumia hadi ukatosheka na unatafuta namna ya kumtema. Huo ni utapeli wa kimapenzi na watu kama wewe wanafaa kukemewa vikali na kutengwa. Kama unatafuta uongo zaidi wa kumwambia ili umuache, siwezi kukusaidia kwa hilo. Beba msalaba wako.

 

Ana watoto 3 na nataka anizalie nami pia, huu mzigo nitauweza jamani?

Shangazi pokea salamu zangu. Nina uhusiano wa kimapenzi na mwanamke mwenye umri wa miaka 28 huku mimi nikiwa na umri wa miaka 22. Mwanamke huyo yuko tayari nimuoe lakini ana watoto watatu wa wanaume tofauti waliokuwa wapenzi wake. Ninampenda sana lakini pia nahisi nitakuwa na mzigo mkubwa wa kutunza familia kwa sababu mimi pia nataka anizalie watoto wangu. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Uamuzi kuhusu suala hili mwishowe utatoka kwako tu. Unajua kwa hakika kwamba ukimuoa mwanamke huyo ni lazima utawakubali watoto wake hao kama wako hata kama atakuzalia wengine. Ingawa unaungama mapenzi yako kwake, yasije yakakufunga macho ushindwe kuona mzigo uliopo wa kulea watoto. Utakosea kujitwika mzigo ambao unajua kwa hakika huwezi kubeba. Ni muhimu ujue kuwa kushindwa kwako kukimu mahitaji ya familia pia kutaathiri vibaya mapenzi na ndoa yenu. Zingatia mambo haya kwa makini kisha ufanye uamuzi wako.

 

Niliolewa juzi tu lakini sasa sina hisia kwa mume wangu

Hujambo shangazi? Niliolewa mwaka uliopita muda mfupi tu baada ya kuachana na mpenzi wangu wa kwanza nilipomfumania na mwanamke mwingine. Tayari nimepata mtoto lakini hisia za kimapenzi kwa mume wangu zimetoweka kabisa. Nina umri wa miaka 29 pekee na siwezi kuishi na mtu nisiyempenda. Nishauri.

Kupitia SMS

Ninaamini kuwa ulishikana na mwanamume huyo bila kuzingatia kwanza hisia zako kwake kwa sababu ulikuwa na maumivu ya kumpoteza mpenzi wako wa kwanza. Kama umeamua kuwa huwezi kuishi katika ndoa hiyo, itabidi utafute namna ya kujiondoa. Ni muhimu mume wako ajue kuhusu unavyohisi kisha umwelezee mpango wako. Ninaelewa kuwa haitakuwa rahisi lakini hiyo ndiyo jinsi pekee ya kutatua tatizo lako.

 

Nifafanulie Shangazi; mapenzi ni nini?

Shikamoo shangazi! Nina umri wa miaka 16 na mimi ni mwanafunzi nikiwa katika shule ya upili. Tafadhali nina jambo ambalo naomba unielezee. Je, mapenzi ni nini?

Kupitia SMS

Kuna usemi kuwa asiyejua maana haambiwi maana. Kwa sababu hiyo, utanisamehe kwa kutojibu swali lako. Kazi yangu katika ukumbi huu ni kutoa ushauri kwa watu walio katika uhusiano wa kimapenzi na ambao tayari wanaelewa maana ya mapenzi. Wewe bado ni mtoto wa shule na umri wako haukuruhusu kujua wala kujihusisha na mapenzi. Acha kupoteza wakati kwa mambo yasiyokuhusu na badala yake uzingatie masomo yako.

 

Mpenzi wa awali ataka turudiane kwa kuwa niliacha mume, lakini yeye ana mke

Kwako shangazi. Nilikuwa nimeolewa lakini nikamuacha mume wangu nilipogundua alikuwa na mpango wa kando. Mpenzi wangu wa hapo awali amejua na anataka turudiane ingawa tayari ameoa. Bado nampenda lakini sitaki kuharibu ndoa yake. Nishauri.

Kupitia SMS

Inashangaza kwamba mwanamume huyo anadai anakupenda ilhali mlikuwa wapenzi na akakuacha akaoa mwanamke mwingine. Nia yake ni kukutumia tu kwa sababu tayari ameoa. Ni heri utafute wako.