Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Ukatili wa mpenzi kunitema na kuhama wanishtua

January 4th, 2020 2 min read

Na SHANGAZI

HUJAMBO Shangazi? Nimekuwa nikiishi na mpenzi wangu ambaye tumezaa mtoto pamoja. Amekuwa akiahidi kunioa lakini kitendo chake kwangu kimenishangaza. Juzi, alinishauri niwatembelee wazazi wangu na akanipa pesa niwapelekee. Nilirudi baada ya siku mbili nikapata amehama kutoka kwa nyumba ambamo tumekuwa tukiishi. Nilipompigia simu, aliniambia ameoa mwanamke mwingine na wakahamia mahali pengine. Sina kazi na nimelazimika kurudi kwa wazazi wangu pamoja na mtoto wangu. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Mpenzi wako amekuchezea akili. Ingawa mmekuwa mkiishi pamoja huku akiahidi kuwa atakuoa, inaonekana aliamua kwamba hilo halitawahi kutokea na amekuwa akipanga jinsi ya kukutenga. Hatimaye alikuwekea mtego na akafaulu. Sasa ameoa mwanamke mwingine. Kwa kiwango fulani, unafaa kujilaumu mwenyewe pia kwa kukubali kuzaa na kuishi naye kabla ya kuhalalisha uhusiano wenu. Kwa sababu hiyo, hakuna unachoweza kufanya kwa sababu hukuwa mke wake.

 

Simpendi na simtaki

Kwako Shangazi. Kuna mwanamume ambaye tumekuwa wapenzi kwa mwaka mmoja sasa. Nilikubali ombi lake baada ya kunifanyia hisani wakati fulani nilipokuwa taabani. Ukweli ni kwamba, simpendi na sitaki kuendelea kupoteza wakati kwake nikijua uhusiano wetu hautatupeleka popote. Lakini nahofia kumwambia kwa sababu ninajua ananipenda kwa dhati na sijui itakuwaje akijua ukweli huo . Tafadhali nishauri.

Kupitia SMS

Mapenzi ni suala la moyoni na hayafai kuingizwa mzaha. Kuna watu wengi ambao wamejitoa uhai kwa sababu ya mapenzi. Wewe unajua kuwa uliingia katika uhusiano huo kwa sababu ya wema ambao mwanamume huyo alikufanyia. Lakini yeye hajui hivyo. Anaamini ulikubali ombi lake kutokana na mapenzi ya dhati. Bila shaka ataumia sana moyoni akijua ukweli. Lakini itabidi umwambie kwani sio wewe tu unayepoteza wakati wako bali yeye pia. Fanya hivyo haraka iwezekanavyo.

 

Anihangaisha na SMS

Vipi Shangazi? Kuna mwanamke tuliyekuwa wapenzi lakini nikamuacha nilipogundua alikuwa akinicheza na mwanamume mwingine. Licha ya kumuacha, ameendelea kuniandama akiniambia ni mimi anayependa lakini mimi simtaki. Sasa nimepata mwingine na huyo wa awali anaendelea kunipigia simu na kunitumia SMS za kimapenzi. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Vitendo vya mwanamke huyo vinaonyesha kuwa anakupenda kwa dhati na huenda kitendo chake cha kukucheza na mwanamume mwingine kilitokana na tamaa tu. Hiyo ndiyo sababu ameendelea kukufuata kwa matumaini kwamba utamrudia. Kutokana na hali hiyo, ni rahisi sana kwake kukuharibia uhusiano wako akipata nafasi na hiyo hasa inaweza kuwa nia yake. Ni muhimu umwambie ukweli mpenzi wako kisha ubadilishe nambari yako ya simu ili kuepuka kero zake.

 

Pato limetugawanya

Kwako Shangazi. Nimependana na mwanamke ambaye ameajiriwa kazi nzuri na analipwa mshahara mkubwa. Mimi pia ninafanya kazi lakini mapato yangu ni duni yakilinganishwa na yake. Tunapendana kwa dhati. Tatizo ni kuwa, mpenzi wangu anatumia hali yake hiyo kunitawala kimawazo. Wakati mwingine pia huwa ananionyesha dharau mbele ya marafiki zetu. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Uwezo wa kifedha na mamlaka haufai kuwa kikwazo katika uhusiano wa kimapenzi. Mapenzi ya dhati ni kumheshimu mwenzako, awe maskini au tajiri. Tabia ya mpenzi wako ya kutaka kukudhalilisha kwa sababu ana pesa nyingi kukushinda ni dalili mbaya katika uhusiano wenu. Itakuwa vyema uketi naye chini mshauriane kuhusu jambo hilo. Kama anathamini uhusiano wenu, ni lazima ajirekebishe. Asipojirekebisha sasa, hali itakuwa hiyo hiyo utakapomuoa.

 

Hawajali nimeolewa

Mimi nimeolewa. Lakini wanaume wengi wananifuata na wanajua nimeolewa. Nifanyeje, kwani nimejaribu kuuwapuuza lakini hakuna mabadiliko.

Kupitia SMS

Kuwapuuza pekee hakutoshi, bali wakabili na waeleze bayana kwamba haitatokea kamwe uwagawie tunda lako. Sio ajabu kwamba wanaendelea kukuandama hata baada ya kuwapuuza, yawezekana bado wanayo matumaini, lakini wakiona hutetereki, hayo matumaini yatadidimia.