Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Umri unazidi kuyoyoma, nitampata wapi wa kuoa?

January 22nd, 2020 2 min read

Na SHANGAZI

HABARI zako shangazi? Nakuja kwako na matumaini kwamba utanisaidia. Sijawahi kuwa na mpenzi maishani. Sasa nina umri wa miaka 45 na ninastahili kuwa na familia. Naomba unisaidie kumpata mwanamke yeyote yule aliye tayari kuolewa ili tufunge ndoa tuishi pamoja.

Kupitia SMS

Samahani sana, sitaweza kukusaidia kwa ombi lako hilo. Sababu ni kuwa mapenzi na ndoa hutokana na chaguo la mtu binafsi. Naona kwamba umri umeanza kukupa kisogo na usipochukua hatua ya haraka kutafuta mke utaishi bila. Tunaambiwa kwamba mwenye kiu ndiye huingia kisimani. Kazi kwako.

 

Tuliyeng’ang’ania naye kidosho kazini amepewa cheo na kuwa bosi wangu

Hujambo shangazi? Nimekuwa katika uhusiano wa kimapenzi na mwanamke fulani kwa miezi mitatu sasa. Alikuwa mpenzi wa mwanamume tunayefanya kazi pamoja lakini wakaachana. Sasa mwanamume huyo amepandishwa cheo amekuwa bosi wangu na nimeingiwa na hofu. Nishauri.

Kupitia SMS

Ninaelewa kwamba hofu yako imetokana na uhusiano wa awali kati ya mpenzi wako na bosi wako. Hata hivyo, nahisi kwamba unababaika bure tu kwa sababu wawili hao waliachana kabla ya mwanamume kupandishwa cheo. Pili, itakuwa makosa kwa bosi wako kukuonea ama kukubagua kwa namna yoyote ile eti kwa sababu una uhusiano na mpenzi wake wa awali. Ondoa wasiwasi.

 

Wazazi wanataka niachane na mume kwa sababu kwao ni maskini

Kwako shangazi. Nina umri wa miaka 28, nimeolewa na nina watoto wawili. Mume wangu anatoka familia maskini na wazazi wangu wamekuwa wakinishauri nimuache nitafute mwingine. Licha ya hali yake hiyo, amekuwa akitushughulikia kwa hali na mali mimi na mtoto wetu na ninampenda sana. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Msimamo wa wazazi wako kuhusu ndoa yako unaonyesha kwamba wameweka pesa mbele kuliko hisia zako. Ni bora zaidi kuishi katika umaskini wenye mapenzi kuliko kuishi katika utajiri uliojaa majonzi. Ni wazi kwamba umetosheka na maisha yako ya ndoa na unafaa kuwaambia ukweli huo wazazi wako; kwamba unampenda kwa dhati mume wako licha ya asili yake ya umaskini na huwezi kumpenda mwingine. Hiyo ni haki yako.

 

Demu aliniacha bure akahepa na rafiki yangu; mapenzi yao yameingia mdudu anataka turudiane

Kwako shangazi. Nilikuwa na msichana niliyempenda sana lakini akaniacha, akashikana na rafiki yangu. Hakuwa amenikosea wala sikumkosea. Wamekuwa pamoja kwa miezi kadhaa tu na wameachana. Sasa amerudi kwangu akidai eti ananipenda na anataka turudiane. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Kama msichana huyo alikuacha bila sababu akashikana na rafiki yako, inaonekana yeye ndiye mwenye shida. Ninashuku kuwa uamuzi wa kuachana na rafiki yako umetokana naye. Hiyo ina maana kuwa hata mkirudiana anaweza kukuacha tena kwa ajili ya mtu mwingine. Hata kama unampenda, ni muhimu uzingatie hilo kabla hujakubali ombi lake. Haina maana kuanzisha uhusiano ambao hautadumu.

 

Anadai ni matani tu anafanyia mademu na mimi ndiye kipenzi chake. Nimwamini?

Vipi shangazi? Nina umri wa miaka 25 na nina mpenzi. Kwa miezi kadhaa sasa, nimekuwa nikiona katika simu yake jumbe za kimapenzi kutoka kwa wanawake wengine na hatimaye niliamua kumuuliza. Nilishangaa alipoungama kuwa ana uhusiano na wanawake wengine wawili lakini eti hawapendi, anawachezea tu. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Maajabu hayo. Kama mpenzi wako ameungama mwenyewe kuwa anawalaghai kimapenzi wanawake wengine wawili, amekubali kwamba si mwaminifu kwako. Usikubali kuendelea na uhusiano ambao unakuumiza moyo na akili. Kama hiyo ndiyo tabia yake, itabidi ufanye uamuzi wa haraka. Nina hakika ukimwambia wewe pia utatafuta wanaume wa pembeni kuwacheza hatakubali.