Habari MsetoMakala

SHANGAZI AKUJIBU: Visura nawaona tele huku lakini mbona sipati mke?

March 5th, 2020 2 min read

Na SHANGAZI

KWAKO shangazi. Nina umri wa miaka 39 na huu ni mwaka wa pili nikitafuta mchumba na bado sijapata. Wanawake ni wengi na sikutarajia kuchukua muda mrefu kupata mke. Nimeanza kukata tamaa. Nishauri.

Kupitia SMS

Ninajua kuna wanawake ambao pia wanatafuta wanaume wa kuwaoa lakini wamekosa. Jambo hilo linategemea na sifa za mume ama mke ambaye mtu anatafuta. Ninaamini wewe pia unatumia kigezo hicho na labda ndiyo sababu kufikia sasa hujapata. Siamini kuwa unaweza kumkosa kabisa mwanamke unayemtaka. Endelea kutafuta.

 

Mume amewekwa boksi kimzaha tu, naona nikimpoteza

Vipi shangazi? Nina uhusiano na mwanamume aliyekuwa ameoa lakini wakaachana na mke wake mwaka mmoja uliopita. Katika wiki mbili zilizopita, mke wake huyo amekuwa akimpigia simu akimwambia anataka warudiane. Amekubali ombi hilo na anasisitiza kuwa ananipenda na anataka kunioa mke wa pili. Mimi pia nampenda lakini sijawahi kufikiria kuolewa mke wa pili. Tafadhali nishauri.

Kupitia SMS

Uamuzi wa mwanamume huyo wa kumrudia mke wake ni ishara kwamba hawakuwa wameachana rasmi na bado wanapendana. Mwaka mmoja ni muda mfupi na nahisi kuwa ungejipa muda zaidi ili kuhakikisha wameachana rasmi kabla hujampa moyo wako. Sasa itabidi uvunje uhusiano huo ama ukubali mpango wake wa kukuoa mke wa pili.

 

Ameahidi kunioa ila bado hajamwacha ‘x’

Shikamoo shangazi! Nina mpenzi tunayependana sana hata amenijulisha kwa jamaa zake na kuwatangazia kuwa amepanga kunioa. Tatizo pekee ni kuwa imekuwa vigumu kwake kumuacha mpenzi wake wa awali. Nishauri.

Kupitia SMS

Haiwezekani kwamba ulikubali kuingia katika uhusiano na mwanamume huyo ukijua kwamba ana mpenzi mwingine. Kama alikwambia wameachana na umethibitisha kuwa bado wako pamoja, unafaa kujiondoa katika uhusiano huo kwa sababu umejua kuwa mwanamume huyo si mwaminifu kwako.

 

Nilisafiri kikazi, kurudi napata tayari anatoka na rafiki yangu jamani!

Vipi shangazi? Nimekuwa katika uhusiano wa kimapenzi na mwanamume fulani kwa miaka mitatu sasa. Miezi miwili iliyopita nilitumwa kufanya kazi mbali. Nilirudi juzi nikapata mpenzi wangu ameshikana na mwanamke rafiki yangu. Nilipomuuliza sababu aliniambia niheshimu uamuzi wake. Nampenda sana na sijui kama nitaweza kumpenda mwanamume mwingine. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Kitendo cha mpenzi wako ni dharau kubwa kwako na bila shaka kimekuumiza sana moyoni. Pili, sasa umejua kuwa mwanamke uliyedhani ni rafiki yako ni adui ambaye alikuwa akitafuta nafasi ya kumnyakua mpenzi wako na hatimaye ametimiza lengo lake. Kauli yako kuwa huwezi kupenda mwanamume mwingine si ya kweli. Kama mpenzi wako amepata mwingine, wewe pia unaweza. Ni kwa kumuondoa katika mawazo na moyo wako ambapo utaweza kumkaribisha mwingine.

 

Mpenzi anataka nihamie dhehebu lake ilhali ndimi ninayemuoa

Kwako shangazi. Nina umri wa miaka 31 na nina mpenzi. Sisi sote ni Wakristo lakini tunaabudu madhehebu tofauti. Tumeamua kufanya harusi lakini tofauti ya madhehebu yetu imeleta shida. Mpenzi wangu anataka tufuate dhehebu lake ilhali ninaamini ndiye ninayemuoa kwa hivyo anafaa kuhamia katika dhehebu langu. Waonaje?

Kupitia SMS

Sawa tu na mapenzi, imani ya kidini ni suala la moyoni na nguzo muhimu ya maisha ya binadamu. Kama wewe na mpenzi wako ni Wakristo, tofauti ya madhehebu haifai kuwa kikwazo. Mmoja kati yenu anaweza kubadilisha madhehebu yake ingawa kwa kawaida mwanamke ndiye anayemfuata mume wake. Ushauri wangu ni kwamba mtafute mwongozo kutoka kwa wakuu wenu wa kidini ili kusuluhisha jambo hilo.