Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Vya chumbani napewa tu yeye anapokuwa na njaa

October 4th, 2019 2 min read

Na SHANGAZI

HABARI zako shangazi? Nina mke na tumejaliwa watoto wawili. Tatizo ni kwamba mke wangu hunipakulia vya chumbani yeye mwenyewe anapokuwa na njaa. Nikiwa na njaa huniambia kuwa ni lazima ningoje hadi siku ambayo atahisi anataka. Ninaumia kimya kimya kwa kukosa huduma hiyo na nahofia nitashawishika kwenda nje ingawa singependa kufanya hivyo. Nishauri tafadhali.

Kupitia SMS

Msimamo wa mke wako unaashiria ubinafsi na kutokujali. Mojawapo ya manufaa ya ndoa ni kwa wahusika kufaana kwa hali na mali. Mke wako anakosea kwa kususia huduma hiyo hadi anapokuwa na haja bila kujali mahitaji yako. Mwelezee wazi hali unayokabiliana nayo kutokana na msimamo wake huo ukiwemo ushawishi wa kutafuta huduma hiyo kwingineko. Labda akijua hivyo atarekebisha mambo.

 

Nilitema kipusa kwa kugawa asali lakini naona sasa anitafuta

Habari zako shangazi? Nilikuwa nimeoa lakini nikamuacha mke wangu baada ya kumfumania na mwanamume mwingine kwenye lojing’i. Aliniachia mtoto wetu wa pekee akiwa na umri wa miezi minane. Ni mwaka mmoja sasa tangu tuachane na ameanza kunipigia simu akitaka kurudi. Mimi sina haja naye. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Umesema wazi kwamba huna mpango wa kurudiana na mke wako kutokana na kitendo chake kilichokufanya umuache. Kama umekata kauli moyoni mwako kwamba huwezi kumsamehe ili mrudiane, huhitaji ushauri mwingine wowote kutoka kwangu. Mwelezee msimamo wako huo ajue kwamba hana nafasi tena katika maisha yako.

 

Ninapenda wanawake wawili kwa dhati; nichague yupi kati yao?

Shangazi pokea salamu zangu. Tafadhali naomba ushauri wako. Nina uhusiano na wanawake wawili na ninawapenda wote. Mmoja ana mtoto na yule mwingine sasa ana mimba. Nahofia kumuacha mtoto wangu ateseke na pia sitaki kumuacha aliye na mimba wakati huu ambao ananihitaji hata zaidi. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Samahani kaka; nahisi kwamba hustahili ushauri wowote kutoka kwangu. Sababu ni kwamba hayo yako si mapenzi bali ni tamaa. Umekuwa ukiwahadaa wanawake hao na sasa ujanja wako umefika ukingoni umeamua kumuacha mmoja wao abebe mzigo wako? Tafuta mwenyewe jinsi ya kujitoa katika hali hiyo.

 

Lo! Nimegundua mume hunisengenya kwa wazazi wake

Kwako shangazi. Nimeolewa na nina watoto wanne. Nina tatizo moja kuhusu mume wangu. Mwenzangu hana siri, kila tukikosana kuhusu jambo dogo tu yeye hukimbia kwa wazazi wake kuwaambia. Nimegundua pia yeye na wazazi wake wamekuwa wakinisengenya. Tabia yake hiyo imesababisha chuki kati yangu na wazazi wake. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Kwa kawaida, mwanamume hasa ndiye anayefaa kuweka siri za nyumbani kwake. Ajabu ni kwamba huyo wako anafanya kinyume kwa kuwapelekea wazazi wake udaku kuhusu maisha yenu. Iwapo hujamwambia unavyohisi kuhusu tabia yake hiyo, ni vyema umwelezee uone kama atajirekebisha. Na iwapo hali hiyo imefikia kiwango ambacho huwezi kuvumilia, una haki ya kutoka katika ndoa hiyo.

 

Amesema waziwazi atatafuta wa kumpa burudani, hii ni haki?

Hujambo shangazi? Nina mpenzi tunayependana sana na sasa ni miezi 10 tangu tujuane. Aliniomba asali lakini nikamwambia asubiri hadi tutakapooana. Juzi nilishangaa aliponiambia eti atatafuta mwingine wa kumpakulia asali tu kisha mimi niwe mpenzi wake wa ndoa. Ananipenda kweli?

Kupitia SMS

Hatua ya mwanamume huyo imeonyesha wazi kuwa anachotafuta si mapenzi bali anataka mwanamke wa kumtumia. Kama anaweza kumtumia mwanamke mwingine kutosheleza tamaa yake kwa madai eti wewe ndiye mpenzi wake wa ndoa, basi huyo si mtu mzuri wala hakupendi. Mapenzi ya dhati yana subira. Muepuke kabisa.