Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Wadai kunipenda lakini nikieleza nina mtoto wananitoroka

August 28th, 2019 2 min read

Na SHANGAZI

SHIKAMOO shangazi! Nina umri wa miaka 25 na nina mtoto niliyezaa na mpenzi wangu wa kwanza lakini tukaachana. Kuna wanaume wengi ambao wamekuja kwangu wakitaka tuwe wapenzi lakini nikiwaambia nina mtoto wanatoweka. Je, ninakosea kuwaambia ukweli?

Kupitia SMS

Huwezi kuficha ukweli kwamba una mtoto kwani hata ukificha hatimaye utagunduliwa. Ni kweli kuna wanaume wasiopenda kuoa wanawake wenye watoto lakini si wote. Huenda unatamani sana kuolewa lakini hilo lisiwe jambo la kufa kupona. Tafuta kwa subira, siku ikiwadia utampata anayekufaa.

 

Amenidi umri kwa miaka 13,nitaweza?

Hujambo shangazi? Nina umri wa miaka 25. Nina uhusiano wa kimapenzi na mwanamke wa miaka 38 na amekubali kuwa mke wangu. Je, inawezekana?

Kupitia SMS

Hakuna lisilowezekana palipo na mapenzi na maelewano kati ya wawili. Kama umeridhika moyoni mwako kwamba huyo ndiye anayekufaa naye pia anaamini ni wewe, hakuna tatizo lolote.

 

Ameamua tuvunje uhusiano, nifanyeje?

Shikamoo shangazi! Nimekuwa kwenye uhusiano na mwanamke fulani kwa mwaka mmoja sasa na nimeamua ndiye atakuwa mwenzangu maishani. Lakini alinishangaza juzi aliponitumia ujumbe wa SMS kuniambia ameamua tuvunje uhusiano wetu. Hakunipa sababu yoyote ya hatua yake hiyo. Nahitaji ushauri wako.

Kupitia SMS

Bila shaka mpenzi wako amefikia uamuzi huo kwa sababu zake mwenyewe. Inawezekana amepata mwingine ama ameamua tu kuwa hataki tena kuendelea na uhusiano huo. Ni heri umtafute uzungumze naye ili ujue sababu hasa ya uamuzi wake huo wa ghafla na uwe tayari kuendelea na maisha yako.

 

Moyo unatamani mpenzi mwingine

Shikamoo shangazi! Nimekuwa na mpenzi kwa miaka miwili na nimegundua sina mapenzi ya dhati kwake. Kuna mwanamume mwingine ambaye ameteka moyo wangu na ninaamini ndiye anayenifaa maishani. Naomba ushauri wako. Nishauri.

Kupitia SMS

Hakuna haja ya kuendelea na uhusiano ambao unajua wazi hautaenda mbali. Kama una hakika umempata anayekufaa, itakuwa muhimu umwambie uliyenaye. Uamuzi wako huo utamuumiza moyoni lakini ni heri kumwambia mtu ukweli.

 

Alinitoroka na ataka turudiane, nikubali?

Shikamoo shangazi! Kuna msichana tuliyekuwa wapenzi kwa miaka mitatu lakini akaniacha na kuolewa na mwanamume mwingine. Sasa anataka turudiane na hisia zangu kwake bado zipo. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Mapenzi yanaweza kumteka akili mtu na kumfunga macho akose kufikiria wala kuona. Ingawa unasema bado unampenda msichana huyo, ni muhimu kwanza utafute ni kitu gani kilichomfanya akuache na ni kwa nini sasa ameamua kumuacha huyo mwingine. Huenda kuna jambo fulani ambalo si sawa kwake na ni muhimu utahadhari usije ukajitafutia balaa.

 

Nampenda sana ila hata SMS hatumi

Hujambo shangazi? Nina uhusiano na kijana fulani na ninampendasa sana. Tatizo lake ni kwamba hapendi kunipigia simu au kunitumia SMS. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Ni lazima mwenzako ana sababu ya kutotaka kuwasiliana nawe kwa simu. Kama hujawahi kumuuliza, ni muhimu ufanye hivyo ili ujue ni sababu gani hiyo ndipo ujue hatua ya kuchukua.

 

Nimemfumania na mpenzi wa kale

Vipi shangazi? Nina mpenzi wangu wa dhati. Lakini nilishangaa sana juzi nilipomtembelea nyumbani kwake nikampata na mwanamume aliyekuwa mpenzi wake. Sijamuuliza walikuwa wakizungumzia nini lakini nimeingiwa na wasiwasi. Nishauri.

Kupitia SMS

Una sababu ya kuwa na wasiwasi hasa ukizingatia kwamba wawili hao walikuwa wapenzi. Badala ya kunyamaza na kuumia kwa hofu, ni muhimu umuulize mpenzi wako ili ujue kiini hasa cha mpenzi wake wa zamani kumtembelea.