Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Wakwe wamekuwa kero kwenye ndoa yangu

May 28th, 2019 2 min read

Na SHANGAZI

SHIKAMOO shangazi! Nimeolewa na nina mtoto mmoja. Tatizo langu ni kuwa jamaa za mume wangu wameingilia vibaya ndoa yetu. Mama mkwe na binti zake wamekuwa wakija kwetu na kuishi hata mwezi mzima. Isitoshe, wakiwa kwangu huwa hawanitambui na hunionyesha madharau sana. Ndoa imenishinda na nimeamua kujiondoa. Tafadhali nishauri.

Kupitia SMS

Ni makosa makubwa kwamba mama mkwe na binti zake wanakuonyesha madharau nyumbani kwako. Je, mume wako anasema nini kuhusu jambo hilo? Kama anashuhudia hayo bila kuwakanya jamaa zake hao, hayo ni madharau yaliyokiuka mipaka na hustahili kuwa katika ndoa kama hiyo. Huenda wamekula njama wakufukuze kwa hivyo usingoje hadi wakati huo ufike.

 

Mpenzi anisaliti ila nimekwama kwake

Shangazi nimekuwa na mpenzi kwa mwaka sasa lakini nimegundua ana wanawake wengine. Ajabu ni kwamba nimeshindwa kumuacha ingawa nina ushahidi wa kutosha kwamba ana wapenzi wengine. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Mwanamume huyo amekupumbaza kwa mapenzi yake hivi kwamba hujali kuwa katika msururu wake wa wapenzi. Hakuna jinsi ninavyoweza kukusaidia kwa sababu wewe mwenyewe unasema umeshindwa kumuacha.

 

Aniaibisha mtaani bila haya kabisa

Shikamoo shangazi! Nimekuwa na mpenzi kwa miaka mitano sasa lakini ameanza tabia mbaya na zenye aibu. Nimegundua kuwa anatembea ovyo na wanawake wengine mtaani. Nimemuuliza akakiri na kuniambia eti nisijali mimi ndiye wake tu. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Sijui unataka ushauri wa aina gani kutoka kwangu kama tayari umejua kuwa mpenzi wako si mwaminifu kwako. Je, unataka kuendeleza uhusiano huo? Mwanamume mwenye tabia kama hizo hafai kupewa nafasi. Achana naye na ujipe shughuli.

 

Wamenipokonya mke kisa, mahari

Hujambo shangazi? Nilikuwa nimeoa mke lakini baada ya mwaka mmoja jamaa zake wakaja wakamchukua kwa sababu sikuwa nimelipa mahari ilhali tulikuwa tumepata mtoto. Nilijitahidi nikawapelekea wazazi wake kiasi fulani cha pesa kama sehemu ya mahari. Waliniahidi kuwa mke wangu atarudi lakini bado hajarudi. Nimepata habari kuwa hata nyumbani kwao hayuko. Nikiwauliza wazazi wananipeleka huku na kule. Nampenda sana mke wangu na mtoto wetu na ninaumia sana moyoni hata sina raha maishani. Nishauri.

Kupitia SMS

Inaonekana kuwa jamaa za mke wako walipokuja kumchukua walikuwa wameamua kumtoa kwako kabisa lakini hawakutaka kukwambia. Na ndio maana hata ameondoka nyumbani kwao ili usije ukaanza kumfuata huko. Pesa zako walizochukua waliamua kwamba ni mahari ya muda ambao uliishi na binti yao hata mkazaa pamoja. Kama hali ni hiyo, sioni matumaini yako kumpata tena mke wako, ni heri umsahau.

 

Ndoa imeingia mdudu, nifanyeje?

Hujambo shangazi? Nina umri wa miaka 28 na nimekuwa katika ndoa kwa miaka miwili sasa. Lakini ndoa yangu imeingia doa. Mume wangu ana uhusiano na mwanamke ambaye anaweza kuwa mama yake kulingana na umri wake. Nimemuuliza sababu akaniambia wazazi wake hawanitaki kwa hivyo ameamua kuoa mke mwingine. Nimewauliza wazazi wakaniambia huo si mpango wao. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Hiyo yako sasa si ndoa bali ni mateso, dhuluma na kejeli. Mume wako ameshikwa mateka na huyo mwanamke mwingine na usitarajie kwamba atabadilika hivi karibuni. Isitoshe, amekwambia wazi kwamba hakutaki na ndiyo maana ameamua kushikana na mwanamke huyo. Usingoje mambo yaharibike zaidi ya yalivyo sasa. Hata kama wazazi wake wanakupenda, hiyo ni bure tu kwa sababu hawawezi kuchukua nafasi yake.