Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Wakwe zangu wananichukia ajabu lakini mume haoni

November 30th, 2019 2 min read

Na SHANGAZI

NIMEOLEWA miaka mitatu sasa. Tumejaliwa mtoto mmoja. Mume wangu ananipenda sana lakini mama na dada zake wananichukia. Wanajaribu juu chini kuvunja ndoa yetu. Juzi nilipigana na mmoja wa dada zake aliponitukana, nikaamua kwenda kwetu. Sasa mume wangu ananiomba msamaha akitaka nirudi na kuahidi kuwa atawakanya. Nataka sana kudumisha ndoa yangu lakini sina hakika kwamba nikirudi hali itabadilika. Nishauri Shangazi.

Kupitia SMS

Kulingana na maelezo yako, bado mnaishi nyumbani kwa wazazi wa mume wako. Hicho ndicho kiini cha kuzuka kwa tofauti za mara kwa mara baina yako na jamaa zake. Hali kwamba ameomba urudi ni ishara kuwa anakupenda, nawe pia unasema unampenda. Hata hivyo, suluhisho pekee la kumaliza mzozo kati yako na jamaa zake ni kutafuta makao yenu wawili. Mpe mumeo hilo kama sharti la wewe kumrudia.

 

Sponsa anatishia kumwaga mtama

Vipi shangazi? Kuna wakati nilikosana na mume wangu na tukatengana kwa karibu miaka miwili. Upweke ulinimaliza nikaamua kushikana na mwanamume mwingine ambaye ameoa. Hatimaye tumerudiana na mume wangu, lakini huyo mwingine hataki kuniacha. Isitoshe, anatishia kumuambia mume wangu kuhusu uhusiano wetu. Nifanyeje?

Kupitia SMS

Ninaamini uliposhikana na mwanamume huyo ulimuambia ukweli kwamba wewe ni mke wa mtu, ingawa mlikuwa mmetengana. Kama ulifanya hivyo basi anafaa kuelewa kuwa sasa umerudi kwako na hamuwezi kuendelea na mirindimo yenu ya pembeni. Kama anatishia kumuambia mume wako, hata wewe muambie akithubutu nawe pia utamuambia mke wake.

 

Mwanamke niliyeoa amenisaliti vibaya sana

Shangazi, nilioa mwanamke aliyekuwa na mimba ya mwanamume mwingine. Mke wangu alijifungua na nimekuwa nikimtunza mtoto huyo kama wangu, lakini nimegundua kwamba mke wangu na baba ya mtoto huyo huwa wanawasiliana kwa simu na hata kukutana kisiri. Hilo linaniuma sana; nataka kumuacha. Tafadhali naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Nahisi mwanamke huyo hakupendi. Pengine alipotemwa na mwanamume huyo akiwa na mimba, alitaka mtu wa kumshughulikia wakati wa ujauzito na kisha baadaye kumsaidia kulea mtoto. Hisia zake ziko kwa baba ya mtoto ndiyo maana bado wanaendelea kuwasiliana na kukutana kisiri. Achana naye arudi kwa baba mtoto wake.

 

Dadake amenigeuzia mashtaka ilhali ni yeye ananimezea mate

Hujambo, nina mwanamke mchumba wangu ambaye tumepanga kufunga ndoa hivi karibuni. Tayari amenijulisha kwa jamaa zake. Kuna dadake mmoja ambaye amekuwa akinitaka kimapenzi na nimejaribu kumkanya lakini hasikii. Imebidi nimuambie mpenzi wangu na sasa amenikasirikia akidai ni mimi ndiye ninamtongoza dadake.

Kupitia SMS

Ni jambo la kushangaza kwamba umemfahamisha mpenzi wako kuhusu suala hilo ili akusaidie kulishughulikia, badala yake amekugeuka akidai wewe si mwaminifu. Hali yake hiyo inatokana na wivu kwani amejua kwamba unawavutia wanawake wengine, akiwemo dadake. Jaribu kuzungumza naye umueleze kwamba, iwapo hungekuwa mwaminifu kwake hungemuambia lolote. Mhakikishie kuwa ndiye chaguo lako wala hutaki mwingine. Akiendelea kusisitiza kuwa wewe si mwaminifu, itabidi uachane naye kwani itadhihirisha kuwa hata ukimuoa hatawahi kukuamini.

 

Juzi nilipata kondomu chumbani, leo ni sketi. Dunia yangu imepasuka!

Shangazi nakusalimu. Kuna kijana tunayependana lakini nimeanza kushuku uaminifu wake kwangu. Nimewahi kupata kondomu iliyotumiwa chumbani mwake. Nilipomuuliza, alijitetea eti alikuwa ametembelewa na rafiki yake ambaye alikuja na mpenzi wake, akawaacha humo akienda kazini na anaamini walifanya mambo. Juzi nilipata sketi ya mwanamke chumbani na sasa nimeamini ako na mwingine. Nimekuwa mwaminifu kabisa kwake na imeniuma sana kiasi kwamba nahisi kujitoa uhai. Nishauri tafadhali.

Kupitia SMS

Visa hivyo viwili ni ushahidi kuwa mpenzi wako si mwaminifu. Ninajua umevunjika sana moyoni lakini kujitoa uhai kamwe si suluhisho. Kama unahisi huwezi kumvumilia zaidi, ni heri kujiondoa katika uhusiano huo. Wanaume ni wengi, utampata mwingine.