Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Wanawake mtaani wananichukia kwa ajili ya mume

October 25th, 2019 2 min read

Na SHANGAZI

VIPI shangazi? Nina umri wa miaka 24 na niliolewa mwaka uliopita. Hata hivyo, kuna jambo ambalo linanikosesha amani katika ndoa yangu. Nimekuwa nikishangaa ni kwa nini baadhi ya wanawake katika mtaa tunamoishi wananichukia ilhali mimi ni mgeni katika mtaa huo. Sasa nimejua kuwa walikuwa wapenzi wa mume wangu na wanahisi vibaya kwamba amenioa mimi. Ajabu ni kwamba nilipokutana mara ya kwanza na mume wangu aliniambia hajawahi kuwa na mwanamke mwingine. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Sasa umejua kuwa mume wako alikudanganya kama umethibitisha kuwa alikuwa na wapenzi katika mtaa huo. Lakini hali kwamba aliwaacha akakuoa wewe ni thibitisho kuwa moyo wake ulitua kwako. Si vyema kuishi miongoni na watu walio na kinyongo nawe. Shauriana na mume wako muone kama mnaweza kuhamia mtaa tofauti ili upate kuwa na amani.

 

Jibaba limegundua nina mpenzi kando, sasa asema nichague ilhali ndiye mfadhili!

Hujambo shangazi? Nina umri wa miaka 20 na nimekuwa katika uhusiano na mwanamume fulani kwa miaka miwili. Lakini majuzi niligundua kuwa ni mume wa mtu na nikaamua kuanzisha uhusiano wa pembeni na kijana wa rika yangu. Sasa mwanamume huyo amegundua na ameniambia nichague kati yake na kijana huyo. Nimeamua kumuacha lakini tatizo ni kuwa amekuwa akinisaidia kwa mahitaji yangu ya pesa na kijana niliye naye hana uwezo huo. Nishauri.

Kupitia SMS

Uliamua kutafuta mpenzi wako mwenyewe baada ya kugundua kuwa mwanamume huyo ameoa na nia yake ni kukutumia tu. Usikubali kuwa mateka wake kutokana na msaada wa pesa ambao umekuwa ukipata kutoka kwake. Tosheka na uliye naye pamoja na msaada kidogo unaopata kutoka kwake. Ukiweka pesa mbele katika uhusiano wa kimapenzi utapotea.

 

Ningali bikira lakini mpenzi ataka sana kukagua chungu, nimpatie idhini?

Shikamoo shangazi! Nina umri wa miaka 19 na nina uhusiano na kijana ambaye nampenda sana. Kwa mwaka mmoja ambao tumekuwa wapenzi, amekuwa akinishawishi tushiriki mapenzi. Mimi bado ni bikira na siko tayari kwa jambo hilo kwa sasa. Nahitaji ushauri wako.

Kupitia SMS

Ingawa unaungama mapenzi yako kwa kijana huyo, ushauri wangu ni kwamba usikubali kushawishika kushiriki jambo ambalo hujawa tayari kwalo. Wewe bado ni mdogo sana kiumri na ni mapema sana kuanza kushiriki mambo hayo. Mwambie ukweli mpenzi wako. Kama anakupenda atasubiri hadi utakapokuwa tayari.

 

Mume alinioa tu na kunipeleka kwao, nampenda ila maisha huku ni magumu mno

Hujambo shangazi? Niliolewa majuzi tu na mume wangu akanipeleka nyumbani kwao. Lakini maisha ya kwao ni magumu sana na kusema kweli siyawezi. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Sijui ulitarajia maisha ya aina gani katika ndoa na iwapo mlikuwa mmeshauriana jambo hilo na mume wako. Kama umekuwa ukiishi mjini na unahisi maisha ya mashambani ni magumu, itakuwa vyema ushauriane na mume wako kuhusu jambo hilo ili mtafute suluhisho.

 

Nimekaa jela miaka 4, nimerejea na mke naye ameolewa, sasa nifanye nini?

Kwako shangazi. Nina umri wa miaka 42. Nilikuwa nimeoa lakini nikashikwa na kesi na kufungwa jela kwa miaka minne. Nimemaliza kifungo na nikapata mke wangu ameolewa na mwanamume mwingine. Nimeulizia nikaambiwa aliolewa mwaka mmoja tu baada ya mimi kwenda jela. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Inaonekana mke wako alihisi kuwa miaka minne ni muda mrefu na ndiyo maana aliamua kuolewa na mwanamume mwingine. Sidhani kwamba unafikiria kumtoa katika ndoa hiyo na hata kama una nia hiyo haitakuwa rahisi. Ningekuwa wewe ningetafuta mke mwingine.