Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Wazazi wangu wamekataa kutambua mume wangu

April 5th, 2019 2 min read

Na SHANGAZI

KWAKO shangazi. Nimeolewa na mume wangu tunapendana sana na tumejaliwa watoto wawili. Tatizo kubwa ni kwamba wazazi wangu hawamtaki na sidhani kama ninaweza kupata mwingine kama yeye. Nifanyeje?

Kupitia SMS

Huwezi kuvunja ndoa kati yako na chaguo la moyo wako eti kwa sababu wazazi wako hawampendi. Ndoa ni kati yako na mume wako na wazazi wake au wako hawafai kuingilia kati. Waambie tena na tena kuwa huyo ndiye uliyechagua na hutaki mwingine. Hatimaye watazoea na wataheshimu uamuzi wako.

 

Hajanitembelea kwa mwaka mzima

Vipi shangazi? Nina mpenzi anayeishi mbali nami na hajanitembelea kwa karibu mwaka mzima sasa. Hata simu hanipigii kama ilivyokuwa awali. Nimeingiwa na wasiwasi, nishauri.

Kupitia SMS

Sitaki kukata kauli lakini nashuku kuwa moyo wa mwenzako hauko tena kwako na huenda umehamia kwingineko. Hata kama anaishi mbali nawe, siamini kwamba kwa mwaka mzima hajapata muda wa kukutembelea na haonekani kuwa na hamu nawe. Chunguza kwa makini ujue msimamo wake kwako.

 

Ameanza kuniudhi

Shangazi pokea salamu zangu. Kuna mwanamume ambaye tumekuwa na uhusiano kwa mwaka mmoja na nampenda sana kwa jinsi anavyonihudumia kwa kila njia. Lakini siku za hivi karibuni simuelewi kwani ameanza kunitumia SMS za kuniudhi na nahisi anafanya hivyo kimaksudi. Nifanyeje?

Kupitia SMS

Mabadiliko unayoona katika mienendo ya mwenzako labda ni ishara kuwa hakutaki tena lakini hataki kukwambia hivyo. Itakuwa vyema umkabili ana kwa ana umuulize nia yake hasa ili usiendelee kupoteza wakati wako.

 

Apenda wanawake wa pembeni sana

Shikamoo shangazi! Nina umri wa miaka 30 na nimeolewa. Ninampenda mume wangu sana lakini ameshindwa kuachana na wanawake wengine wa pembeni. Nifanyeje?

Kupitia SMS

Iwapo kweli mume wako ana wanawake wengine wa pembeni, hayo ni maisha hatari na huwezi kuwa na raha katika ndoa yako. Jaribu kuhusisha wazazi au jamaa zenu wamkanye. Ndoa ni jambo la mtu kujitakia na ukihisi haina manufaa kwako una haki ya kujiondoa.

 

Ananihepa

Shikamoo shangazi! Kuna msichana aliyekubali kuwa mpenzi wangu lakini baada ya siku chache akaanza kunihepa. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Kama ameamua kukuacha huwezi kumzuia kwa sababu yeye si mke wako na hata mke wako anaweza kuamua ametosha ndoa na kuondoka. Kubali uamuzi wake.

 

Nimemzidi umri kwa miaka 10

Shikamoo shangazi! Mimi ni mwanamke mwenye umri wa miaka 38 na nimependana na mwanamume ambaye nimemzidi umri kwa miaka kumi. Je, kuna tatizo?

Kupitia SMS

Kama mwanamume huyo hana shida na tofauti hiyo ya umri, sioni tatizo lolote bora tu mnapendana na mnaelewana. Ondoa wasiwasi.

 

Ananizungusha tu!

Vipi shangazi? Kuna mwanamke ambaye nampenda lakini amekuwa akinizungusha huku na kule kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa, hasemi anataka ama hataki. Nifanyeje?

Huo ni muda mrefu wa mtu kufanya uamuzi kuhusu hisia zake kwa mwingine. Inawezekana kuwa mwanamke huyo hakutaki lakini hataki kukwambia. Sasa ni juu yako uamue iwapo utampa muda zaidi ama utaachana naye utafute mwingine.

 

SMS zimeleta balaa

Shikamoo shangazi! Juzi mwanamume mpenzi wangu alikasirika sana alipopata SMS katika simu yangu ambazo nilitumiwa na mwanamume mwingine anayenitaka ingawa mimi nimemkataa. Sasa mpenzi wangu anatishia kuniacha akidai mimi si mwaminifu kwake. Nifanye nini?

Ingawa hujasema mwanamume huyo alikwambia nini katika jumbe hizo, itabidi ufanye juu chini kumhakikishia mpenzi wako kuwa huna uhusiano naye. Ikiwezekana panga mkutane naye ili wazungumze na mpenzi wako.