Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Wivu kupindukia umefanya wapenzi wanitoroke

January 2nd, 2020 3 min read

Na SHANGAZI

SHIKAMOO Shangazi! Mimi ni mwanamume mwenye umri wa miaka 27. Nina tatizo fulani kuhusu nafsi yangu. Nina wivu sana na hali yangu hiyo imenifanya nishindwe kudumisha uhusiano wa kimapenzi. Ninapokuwa na mpenzi, sipendi kumuona akizungumza na mwanamume mwingine. Nimewahi kuwa na wawili lakini waliniacha kwa sababu ya hali yangu hiyo. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Wivu wako huo unatokana na hali ya kutojiamini na pia ubinafsi. Ni muhimu uelewe kwamba, kila mtu ana haki ya kuwa na marafiki wanawake na wanaume pia. Pili, unafaa pia kuamini kwamba mwanamke anaweza kukupenda wewe tu na pia adumishe urafiki na wanaume wengine. Ninaamini wewe pia una marafiki wa kike ambao si wapenzi wako. Wanawake unaokutana nao na kuwapenda wana marafiki wa kiume ambao hawana uhusiano wa kimapenzi nao. Ni lazima ukubali ukweli huo wa maisha ndipo uweze kumaliza shida yako hiyo.

 

Agizo lake limenishtua

Shikamoo Shangazi! Nina mpenzi lakini kuna jambo ambalo linanitatiza kumhusu. Ni mwaka mmoja sasa tukiwa wapenzi na kwa muda wote huo, tumekuwa tukiwasiliana kwa simu. Sasa ameniwekea sharti kwamba nisiwe nikimpigia simu, niwe nikimtumia SMS pekee. Nina shaka na uamuzi wake huo.

Kupitia SMS

Ni lazima mpenzi wako ana sababu kubwa ya kukatiza mawasiliamo kwa simu na ninahisi si kwa nia njema. Kama mmekuwa mkiongea kwa simu kwa muda ambao mmekuwa pamoja, ni kitu gani kinaweza kubadilisha mtindo huo? Inawezekana mwenzako ana mwingine na anahofia utampigia simu wakati mmoja wakiwa pamoja, umharibie. Chunguza ujue ukweli ili uchukue hatua inayofaa.

 

Anishuku bila sababu

Kwako Shangazi. Nimekuwa na mpenzi ninayempenda kwa dhati lakini hali yake ya kutoniamini imetufanya tukosane mara kadhaa. Amekuwa akinishuku bure tu kwani mimi sina mwanamume mwingine isipokuwa yeye. Amewahi kuniacha akashikana na mwanamke mwingine lakini akamuacha akarudi kwangu. Nilimkubali kutokana na penzi langu kwake nikiamini uhusiano wetu utadumu. Mwezi mmoja uliopita, aliniacha tena kwa kunishuku na sasa anaomba turudiane tena. Nishauri.

Kupitia SMS

Uhusiano wa kimapenzi unaokumbwa na misukosuko kuhusu ukosefu wa uaminifu mara nyingi huishia kwa wahusika kuachana. Mpenzi wako anasumbuliwa na wivu na ndiyo maana anakushuku bure tu bila ushahidi wowote kuhusu madai yake. Inaonekana kwamba kila anapokuacha, huwa anatathmini moyo wako na kugundua kuwa anakushuku bure na ndiyo maana amekuwa akirudi. Tatizo ni kwamba, hali yake hiyo ni vigumu kubadilika na inaweza kuendelea hata katika ndoa. Ningekuwa wewe ningemuepuka kabisa.

 

Jamaa ameniumbua

Shikamoo Shangazi! Kuna mwanamume ambaye amekuwa akinitaka lakini nimemkataa kwa sababu sina hisia kwake. Sijamuona wala kumsikia kwa miezi kadhaa na nilidhani kuwa alinielewa. Lakini nilishtuka juzi aliponipigia simu akanitusi vibaya akisema eti ninaringa ilhali mimi ni sura mbaya. Matamshi yake hayo yamenichafua roho na kunifanya nihisi kujichukia. Nahitaji ushauri wako.

Kupitia SMS

Matamshi ya mwanamume huyo yanatokana na machungu anayohisi kwa sababu umemkataa. Kama ulimwambia kuwa huna hisia kwake anafaa kuelewa na kuachana nawe badala ya kutumia mbinu duni kama hiyo kukulazimisha umpende. Kama kumwambia ukweli kwake ni maringo, acha iwe hivyo. Jambo la pili, kama wewe ni sura mbaya, kwa nini amekuwa akikutaka? Mpuuze kisha umzime katika simu yako ama ubadilishe nambari yako ili kumuepuka.

 

Aenda kwao kila mara

Shangazi, nimeoa na nina mtoto mmoja. Ni miaka minne sasa na tumekosana mara tatu. Sababu ya kukosana ni kwenda kwao kila siku. Nikitoka asubuhi naye anatoka anaenda kwao. Nikimwachia pesa anashughulika na mambo ya kwao. Hana kazi na kila kitu namtimizia majukumu yote ya nyumba. Shida ni kwenda kwao bila kuniambia.

Kupitia SMS

Ndoa ni maelewano na masikilizano. Pia ni kuheshimiana na kutilia maanani anachosema mwenzako. Chukua hatua ya kuketi na mkeo kwa upendo na wala sio shari na umweleze yaliyo moyoni mwako, yale yanayokukwaza na yale ambayo ungependa arekebishe. Ni vyema pia umwulize sababu inayomfanya aende kwao kila siku na labda jinsi mnavyoweza kukubaliana kuhusiana na suala hilo.