Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Yeye ni muuzaji dukani, nahofia ana tabia uchwara

September 20th, 2019 2 min read

Na SHANGAZI

KWAKO shangazi. Mwanamume mchumba wangu amepanga kunioa hivi karibuni. Lakini kuna jambo fulani linalonitia wasiwasi. Anafanya biashara ya duka na nimemfumania mara kadhaa na wanawake tofauti ambao ninashuku anawataka ama wanamtaka. Sitaki anioe kisha anivunje moyo kwa kunichezea na wanawake wengine wa pembeni. Nishauri.

Kupitia SMS

Ninaamini kuwa wasiwasi wako huo unatokana na wivu tu kwani unamshuku mpenzi wako tu, huna ushahidi kuhusu madai yako dhidi yake. Kumbuka kuwa hiyo ndiyo kazi yake na huwezi kumwambia awapige marufuku wateja wanawake eti kwa kuwa unashuku anawataka ama wanamtaka. Iwapo unamwamini, huna sababu ya kuwa na hofu. Isitoshe, mpenzi asiye mwaminifu anaweza kumchezea mwenzake mahali popote pale, si lazima iwe katika biashara.

 

Alikosana na mumewe sasa kakatalia kwangu

Hujambo shangazi? Kuna mwanamke ambaye tumekuwa marafiki ingawa ameolewa. Hivi majuzi alikosana na mume wake na akahamia kwangu. Nimejaribu kumshawishi arudi lakini amekataa. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Kutokana na maelezo yako, nahisi kuna jambo fulani ambalo unaficha. Ingawa unasema mmekuwa mafariki, inaonekana mmekuwa wapenzi na huenda wewe hasa ndiwe kiini cha mwanamke huyo na mume wake kukosana. Hatua yake ya kuja kwako inaonyesha kuwa anaamini unaweza kumuoa na ndiyo maana amekatalia kwako. Kama umekuwa ukimhadaa kuwa unampenda, sasa utakuwa mashakani kwani hatimaye amehamia anakoamini anapendwa.

 

Mume hana kazi na hashughuliki kutafuta

Kwako shangazi. Nina mume na tumejaliwa watoto wawili. Tatizo ni kuwa mume wangu hana kazi wala hashughuliki kutafuta. Sasa wanawake marafiki zangu wananishauri kwamba nimuache. Waonaje?

Kupitia SMS

Ni wajibu wa mwanamume mwenye nyumba kukimu familia yake na ninashangaa kwamba mume wako hashughuliki kutafuta kazi. Ingawa hujasema, ninaamini kuwa maisha ni magumu kwako na watoto wenu. Kama una hakika kuwa ukimuacha utaweza kuishi maisha nafuu au bora, ni heri ufanye hivyo.

 

Akijua tatizo langu ninahisi ataniacha

Kwako shangazi. Nilikuwa nimeolewa lakini mume wangu akaniacha ilipobainika kimatibabu kuwa sina uwezo wa kupata watoto. Sasa nimechumbiana na mwanamume mwingine na yuko tayari kunioa. Lakini nahofia yeye pia ataniacha akigundua shida yangu hiyo. Nishauri tafadhali.

Kupitia SMS

Lengo kubwa la watu wengi katika ndoa ni kujenga familia kwa kuzaa watoto. Halitakuwa jambo la busara kumficha mwanamume huyo hali yako hiyo kwa sababu hatimaye atagundua tu na atakulaumu kwa kutomwambia.

 

Nisaidie vidokezo…

Hujambo shangazi. Mimi ni mwanamume mwenye umri wa miaka 32 na bado sijapata mpenzi. Nahisi nimechelewa na nimeamua kuoa mwaka ujao. Nakuomba unielezee mambo ninayofaa kuzingatia katika kutafuta mke.

Kupitia SMS

Kwanza, huwezi kutenga wakati wa kuoa kabla hujapata mchumba. Inafaa umpate kwanza ndipo mpange pamoja wakati wa kufunga ndoa. Pili, watu tofauti huvutiwa na mambo tofauti katika kuchagua mume au mke. Kuna wanaovutiwa na maumbile ya mwili ilhali wengine huangalia tabia miongoni mwa mambo mengine. Unajua sifa za mwanamke unayetaka kuwa naye maishani, kwa hivyo mtafute.

 

Mpenzi amerejea ila ananizungusha tu

Hujambo shangazi? Mpenzi wangu amekuwa ng’ambo kwa miaka miwili akisoma. Akiondoka alinihakikishia kuwa ananipenda na akaniomba nimsubiri arudi kisha tuoane. Hatimaye amerudi lakini amekuwa akinizungusha tu, hataki kuniambia iwapo mpango huo bado upo ama haupo. Nina wasiwasi, nishauri tafadhai.

Kupitia SMS

Inaonekana kwamba mwenzako amebadili msimamo wake na labda anaona vigumu kukwambia kwa sababu alikuwa amekuahidi kukuoa akirudi kutoka masomoni. Ni muhimu uzungumze naye ujue ukweli kungali mapema usipoteze muda.