Habari Mseto

SHANGAZI: Iweje wananishuku ilhali ‘mali’ nimetia kufuli?

April 10th, 2018 2 min read

Shikamoo shangazi. Mimi ni msichana mwenye umri wa miaka 19. Kuna wanaume wengi ambao wamekuwa wakinitaka lakini nimewakataa kwa sababu mimi bado ni mdogo na sitaki kuharibu maisha yangu. Nimeamua kujiweka vizuri hadi wakati utakapofika Mungu anipe wangu aliyeniwekea. Tatizo ni kuwa wazazi wangu hunishuku bure. Mama hunipigia kelele sana nikichelewa kidogo kufika nyumbani na kuniambia niende nikaolewe nilikokuwa. Baba pia ni mkali hapendi kuona nikiongea na vijana mtaani. Wakati mwingine vitendo vyao hivyo hunifanya nilie nikikumbuka jinsi nilivyo na msimamo mkali kuhusu jambo hilo ilhali wao wananishuku. Naomba ushauri wako.
Kupitia SMS

Ni vyema sana kwamba unatambua hujafikia umri wa kuwa katika uhusiano wa kimapenzi na umeamua kusubiri hadi wakati utakapofika. Ninaelewa unavyohisi kuhusu wazazi wako kwa sababu wanakushuku bure. Lakini usiwalaumu kwa sababu wanajaribu kukukinga na masaibu yanayotokana na mahusiano ya mapema ya kimapenzi. Ninaamini wewe na mama yako huwa mnazungumza kwa hivyo ni vyema uwe ukimwelezea msimamo wako huo na kumhakikishia hutaingia katika uhusiano kabla ya wakati unaofaa.

 

Nisaidie kuchagua kati ya madume haya mawili yanayonimezea

Shikamoo shangazi. Nina umri wa miaka 18 na kuna mwanamume mwenye umri wa miaka 26 ambaye ananipenda. Kuna mwingine pia anayenipenda na ana umri wa miaka 20. Sijali kuwa na uhusiano na yeyote kati yao lakini nimechanganyikiwa, sijui nitachagua nani kati yao kwani naona mmoja amenizidi umri sana ilhali mwingine ni karibu rika yangu. Tafadhali nishauri.
Kupitia SMS

Umri huwa si hoja sana katika uhusiano wa kimapenzi bora tu wawili wanapendana. Hata hivyo, ninaelewa kwamba bado hujawa na uhusiano na yeyote kati yao na unataka kujua ni nani anayekufaa zaidi kwa kuzingatia umri wao. Mara nyingi wanawake huchagua kuolewa na wanaume waliowazidi umri kwani tofauti hiyo hudumisha heshima kati yao. Pili, huwa wanaamini kuwa mwanaume aliyekomaa kuwazidi ana uwezo wa kuwashughulikia vyema na kuwakinga na hatari za kila namna. Ndoa za watu wa rika moja mara nyingi huwa na matatizo kutokana na wao kukoseana heshima. Ningekuwa wewe ningechagua huyo mwenye umri mkubwa.

 

Ninahisi mpenzi  anabagua wanangu ingawa wote si wake

Hujambo shangazi. Nina mpenzi na pia nina watoto wawili ingawa si wake. Ajabu ni kuwa nimegundua kuwa anampenda mmoja wao kuliko mwingine. Hali hiyo inanitatiza kwa sababu ameahidi kunioa na singependa ambague mmoja wa wanangu. Nishauri.
Kupitia SMS

Ninashangaa kwamba mpenzi wako anampenda mmoja wa watoto wako na kumchukia mwingine ilhali hakuna kati yao aliye wake. Ninaelewa wasiwasi wako na ushauri wangu ni kwamba uketi chini naye umwelezee unavyohisi kuhusu jambo hilo. Ukigundua kuwa hatawahi kuwapenda kwa usawa watoto hao ni heri uepuke ndoa hiyo kwa sababu hatimaye suala hilo litazua hali ya kutoelewana na kuathiri vibaya ndoa yenu.

 

Wiki tatu sasa tukikutana kwa siri nimweleweje huyu?

Vipi shangazi? Ni wiki tatu pekee tangu nikutane na jamaa anayenipenda nami pia nampenda. Hata hivyo kuna jambo fulani kumhusu ambalo linanisumbua akili. Hataki mtu mwingine yeyote ajue kuhusu uhusiano wetu, hata marafiki zake, na kwa sababu hiyo tumekuwa tukikutana kisiri faraghani. Kuna nini?
Kupitia SMS

Si jambo la kawaida kwa mwanamume kumficha mpenzi wake hasa kwa marafiki zake. Kulingana na maelezo yako, ninashuku huenda mwanamume huyo ana mpenzi na anaogopa kuwa akikujulisha kwa watu wanaomjua utaambiwa. Kama unawajua marafiki zake, tumia ujanja kumchunguza kupitia kwao ili umjue vizuri.

 

Kila nikimwita kwangu anakataa

Nina msichana mpenzi wangu wa dhati na tumezaa pamoja ingawa hatujaoana. Lakini nikimuita kwangu anakataa. Nifanyeje?
Kupitia SMS

Kama una maana kuwa unamuita kwako muishi pamoja, inaonekana hajaamua kuolewa nawe na labda anakuweka tu kama rafiki kwa sasa hadi atakapopata mtu wa kumuoa. Zungumza naye ujue msimamo wake kuhusu ndoa kati yenu.