Makala

SHANGAZI: Mamangu achukia mume wangu ataka nimtaliki

November 18th, 2019 2 min read

NA SHANGAZI SIZARINA 

Hujambo Shangazi. Nimeolewa kwa miezi kadhaa sasa. Juzi tulikosana na mume wangu lakini tukasuluhisha tofauti zetu. Mamangu anaishi karibu na tangu alipopata habari hizo amemchukia sana mume wangu na ananishauri nimuache kwa kuwa pia hana kazi. Kuna mwanamume mwingine aliyeachana na mke wake na yuko tayari kunioa ili nimsaidie kulea watoto wake. Nimemfahamisha kuwa nina mimba ya mume wangu na ananishauri niiharibu kisha anioe. Nishauri.

Kupitia SMS

Ingawa si vibaya kusikiliza ushauri wa mzazi wako, wewe ni mtu mzima na una uwezo na haki ya kuamua kuhusu mwelekeo wa maisha yako. Hali kwamba wewe na mume wako mnaweza kusuluhisha tofauti zenu ni ishara kuwa mnapendana. Lakini ninahisi umeanza kutoa akili yako katika ndoa hiyo kutokana na ushawishi wa mama yako na huyo mwanamume mwingine. Iwapo unaamini ndiye anayekufaa, kubali tu akuoe ila usikubali kuharibu mimba. Kama anakupenda, anafaa kumpenda mwanao pia kwani yeye anataka umsaidie kulea watoto wake.

Najipendekeza kwake

Shikamoo Shangazi. Mimi ni msichana mwenye umri wa miaka 22 na nina mpenzi tunayependana kwa dhati. Ninajua kwa hakika kuwa ananipenda lakini wakati mwingine nahisi kuwa najipendekeza kwake kwa sababu mara nyingi mimi ndiye humpigia simu kumjulia hali. Je, hiyo ni sawa? Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Baadhi ya mienendo ya watu hutokana na maumbile yao au kutoelewa. Inawezekana kuwa mwenzako haoni wala haelewi kuwa ni muhimu kuwasiliana nawe mara kwa mara ili kudumisha uhusiano wenu. Mwambie unavyohisi kuhusu suala hilo na ninaamini atabadilika.

Aninyima unyumba

Vipi Shangazi? Nimekuwa na mrembo kwa miaka miwili sasa na amekuwa akiniambia ananipenda sana. Lakini ameshindwa kabisa kunionjesha asali ilhali mimi niko tayari. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Ni muhimu ujue kuwa hiyo ni hatua muhimu kwa mwanamke na wanawake wanaojiheshimu huchukua muda kuamua. Miaka miwili ni muda mfupi sana na bila shaka mwenzako anahisi kuwa anahitaji kukufahamu zaidi kabla hajachukua hatua hiyo. Usiwe mchoyo wa kujali hali yako tu. Kama unampenda, kuwa na subira hadi atakapokuwa tayari kwa jambo hilo.

Mpenzi ana wivu tele

Vipi Shangazi? Nina umri wa miaka 18 na nimependana na kijana wa miaka 22. Shida ni kuwa mpenzi wangu ana wivu sana hivi kwamba hapendi kuniona nikizungumza na vijana wengine. Wazazi wake wanajua kuhusu uhusiano wetu na tunapanga kuoana. Hata hivyo nina wasiwasi kuhusu hali yake hiyo. Nishauri.

Kupitia SMS

Mahusiano mengi ya kimapenzi huandamana na wivu kati ya wahusika na hiyo ni mojawapo ya ishara za mapenzi ya dhati. Inaonekana mapenzi yenu ni ya dhati na ndiyo maana mmeamua kufunga ndoa. Unajua kuwa mwenzako ana wivu, kwa hivyo kama unataka kudumisha uhusiano wenu, itabidi uepuke kuzungumza na wanaume wengine akiwa karibu.

Jamaa mkono gamu

Shangazi pokea salamu zangu. Nina mwanamume mpenzi wangu ambaye amenipumbaza kwa penzi lake. Tatizo lake pekee ni kuwa, ni mkono gamu, hajali mahitaji yangu mengine. Lakini pia naona vigumu kumuacha kwani sidhani kuna mwingine anayeweza kunipenda kama yeye. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Hujaelezea iwapo umezungumza naye kuhusu jambo hilo au la. Kama umemwambia na amepuuza, itabidi uchague kuendelea naye kwa ajili ya mapenzi yake ama uachane naye ili utafute anayekutimizia mahitaji yako yote.

Ni kama amenitema

Hujambo Shangazi, nina mpenzi wangu ambaye tunapendana sana. Hata tuliahidiana ya kwamba tutaoana. Sasa amemaliza chuo wiki tatu zilizopita. Lakini nikimpigia simu ni mwanaume anayepokea hiyo simu akidai eti ni mwalimu wake. Nifanyaje?

Kupitia SMS

Mwenzangu akufukuzaye sio lazima akuambie nenda zako, wakati mwingine utaona mambo yakibadilika.