Habari Mseto

SHANGAZI: Mke wa mpenzi wangu ananitishia maisha, nifanyeje?

November 11th, 2019 2 min read

NA SHANGAZI SIZARINA

Hujambo Shangazi? Nina umri wa miaka 20 na nina uhusiano na mwanamume ambaye alikuwa ameoa lakini akatengana na mke wake. Mwanamume huyo yuko tayari kunioa lakini mke wake amefahamu kuhusu uhusiano wetu na ameanza kunitishia maisha. Juzi, alinipigia simu akaniambia nisipoachana na mume wake atatuma watu waniue. Kwa sasa amerudi nyumbani kwa mwanamume huyo. Nina wasiwasi, nishauri.

Kupitia SMS

Hali kwamba mwanamke huyo amerudi kwa mume wake ni ishara kwamba walitengana tu, hawajaachana rasmi. Huenda mwanamume alikuwa ameamua kuendelea na maisha yake lakini mke wake bado alikuwa na mpango wa kurudi. Baada ya kufahamu kuhusu uhusiano wenu, amehisi kuwa unatishia ndoa yake na ndiyo maana amerudi haraka. Huna sababu ya kuweka maisha yako hatarini kwa sababu ya mwanamume aliye na mke. Tafuta wako, wewe bado ni msichana mdogo na una muda wa kutosha wa kutafuta mume anayekufaa.

Amebadilika ghafla

Hujambo Shangazi? Mwanamume mpenzi wangu wa miezi miwili amenicheza vibaya. Alikuwa ameahidi kuwa atanioa lakini naona ghafla amebadili mienendo yake. Nilimpatia mwenyewe pesa za kukodi nyumba na pia nimemnunulia vitu vya nyumbani. Tangu nimpe pesa hizo amekatiza mawasiliano kabisa. Nimekutana naye mara kadhaa akiwa na mwanamke mwingine na nikimuuliza anasema yeye ndiye anajua anayependa. Ninaumwa sana moyoni, sijui nitafanya nini. Tafadhali nishauri.

Kupitia SMS

Mwanamume huyo hakupendi wala hana shughuli nawe. Ingawa hajakwambia hivyo, amekuonyesha kupitia kwa mwanamke ambaye umewaona pamoja. Ninaelewa jinsi ambavyo hatua yake hiyo imekuvunja moyo hasa baada ya kushughulika ukimtafutia nyumba na vitu vingine. Shida iliyopo ni kwamba, kama hakupendi huwezi kumlazimisha akupende kwa hivyo itabidi uachane naye na kumuondoa katika maisha na mawazo yako.

Hataki kinga kamwe

Vipi Shangazi? Nina umri wa miaka 22 na nina mpenzi ambaye tunapendana sana. Hata hivyo tumetofautiana kuhusu jambo moja. Amekuwa akitaka kuonja asali na hatimaye niko tayari. Tatizo ni kwamba, nimemwambie tutumie kinga lakini hataki. Anadai eti pendekezo langu lina maana kwamba ninamcheza. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Mbali na hatari za magonjwa ya kuambukizwa, kuna sababu nyingine inayowalazimu kutumia kinga. Nyinyi ni wapenzi na bila shaka hamngependa kupata mtoto nje ya ndoa. Labda mwenzako hajui hilo kwa hivyo ni muhimu umwelezee ili aweze kuelewa maana ya pendekezo lako. Kwa vyovyote vile, ushauri wangu ni kwamba usikubali kushiriki mapenzi bila kinga kwa sasa. Kuna wanawake wengi ambao wameomba ushauri katika ukumbi huu wakilia baada wapenzi wao kuwapachika mimba kisha kuwahepa.

Sijapata afaaye lakini…

Shangazi ni matumaini yangu kwamba wewe ni mzima. Nina umri wa miaka 28 na sijaolewa wala sina mpenzi. Kuna wanaume kadhaa ambao wananitaka lakini sijaona mmoja kati yao ambaye anatosha kuwa mume wangu. Hata hivyo, ninasumbuliwa sana na joto mwilini hadi wakati mwingine ninashindwa kulala. Nafikiria kuwa na mmoja wa kunishughulikia lakini sitaki kupata mimba. Nishauri tafadhali.

Kupitia SMS

Kuna jinsi mbili pekee za kuepuka mimba na pia magonjwa ya zinaa. Jinsi ya kwanza ni kuepuka kabisa kushiriki mapenzi. Namna ya pili ni kutumia kinga, ambayo inaweza kuwa dawa ama kondomu. Unasema umeshindwa kuvumilia na unahitaji mwanamume yeyote anayeweza kuzima joto mwilini hata kama hakuna hisia za kimapenzi kati yenu. Kwa sababu hiyo, utahitaji kinga ya kondomu ili kuzuia, sio mimba tu, bali pia magonjwa.

Siamini ananipenda

Mimi ni kijana wa umri wa miaka 23. Nina mpenzi ambaye nampenda sana. Pia huniambia ananipenda. Yuko Kidato cha Nne. Kila kitu anachohitaji namnunulia. Lakini naogopa kumwambia anipe burudani. Na siamini kama ananipenda. Tumekaa naye muda wa miaka miwili. Nisaidie.

Kupitia SMS

Miaka miwili bila shaka umemuelewa mwenzako vizuri. Na kila safari huanza na hatua. Bila kufungua mdomo na kueleza yaliyo moyoni mwako kuhusiana na suala hilo, mwenzako hawezi kujua. Pia utafanya busara iwapo utampatia muda amalize masomo yake kwanza.