Habari Mseto

SHANGAZI: Mpenzi anarusha chambo kisiri kwa rafiki yangu

November 4th, 2019 2 min read

Vipi Shangazi? Nina umri wa miaka 31 na nina mwanamume mpenzi wangu ambaye nampenda kwa dhati. Nina mwanamke rafiki yangu ambaye anafanya biashara ya kuuza nguo za wanaume na mpenzi wangu anamjua. Juzi aliniomba nambari yake ya simu akisema alitaka kununua nguo kutoka kwake.

Baadaye rafiki yangu alinionyesha SMS alizotumiwa na mpenzi wangu akimwambia jinsi anavyompenda na kumuomba wawe na mpango wa kando. Jambo hilo limeniudhi sana na bado sijamuuliza mpenzi wangu. Nipe mwelekeo.

Kupitia SMS

Umejua na kuthibitisha kuwa unayemchukulia kuwa mpenzi wako wa dhati ni ndumakuwili ambaye anaweza kukusaliti kimapenzi wakati wowote hata kwa marafiki zako. Sidhani ungependa kuendeleza uhusiano na mtu kama huyo. Kitendo chake hicho kimemuonyesha kuwa mlaghai hatari wa kimapenzi na unafaa kumtema mara moja. Nina hakika kuwa ukimuuliza atakana, kwa hivyo zungumza na rafiki yako ahifadhi SMS alizomtumia ili ziwe ushahidi.

Husema namsumbua

Mambo Shangazi? Nilikuwa nimeoa lakini mke wangu akaniacha. Sababu yake kuniacha ni kwamba, alinikosea na nilipomwambia aombe msamaha akakataa akisema hajanikosea. Badala yake aliamua kuondoka pamoja na mtoto wetu mwenye umri wa miaka miwili. Ninatamani sana arudi lakini kila nikimpigia simu huniambia niache kumsumbua. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Nahisi kwamba unahangaisha moyo wako kuhusu mtu ambaye hana haja nawe na ambaye alitoa kitambo mawazo yake kwa ndoa kati yenu na akaamua kuendelea na maisha yake. Huenda hata aliamua mapema kukuacha na akakukosea makusudi ili kutimiza mpango wake. Majibu yake ya kijeuri kwako ni ishara kamili kwamba hakutaki tena katika maisha yake, kwa hivyo achana naye.

Nashuku uhusiano wao

Shikamoo Shangazi. Mimi ni mwanafunzi wa chuo kikuu na kuna msichana ambaye tunapendana. Hata hivyo, juzi nilimuona mahali akizungumza na rafiki yangu lakini hawakuniona. Baadaye nilimuuliza akaniambia walikuwa wanashauriana kuhusu masomo. Ninashuku kuwa huenda rafiki yangu anamtaka lakini sina hakika. Nishauri.

Kupitia SMS

Tukio hilo la siku moja halitoshi kwako kumshuku mpenzi wako na rafiki yako. Lingekuwa jambo ambalo umeshuhudia mara kadhaa, hapo ungekuwa na maswali. Na iwapo bado unashuku kuwa uhusiano wao ni zaidi ya masomo, anza kuchunguza mienendo yao. Kama kuna njama ya kupindua serikali, utajua.

Wazazi hawampendi

Shikamoo Shangazi. Mimi ni mwanafunzi wa shule ya upili na nimependana na mwanamume ambaye anafanya kazi. Wazazi wangu wamejua na wanapinga uhusiano wetu. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Wazazi wako wana haki ya kupinga uhusiano huo kwa sababu wewe ni mtoto wa shule na mapenzi yataathiri vibaya masomo yako. Kumbuka kwamba ndio wanaogharamia masomo yako na unawakosea kwa kujihusisha na mambo mengine yasiyo na manufaa kwako badala ya kusoma. Ushauri wangu ni sawa na wao tu, achana na mambo mengine umalize masomo kwanza.

Nimsamehe turudiane?

Vipi Shangazi? Nilikosana na mwanamume tuliyekuwa wapenzi na hatujaonana wala kuwasiliana kwa mwaka mzima. Alinipigia simu juzi akaomba msamaha na kuniuliza iwapo ningependa turudiane. Je, nimsamehe turudiane ama niachane naye?

Kupitia SMS

Wewe ndiye unayejua jinsi alivyokukosea na iwapo unaweza kumsamehe au la. Uamuzi wako pia utategemea iwapo bado unampenda. Ukweli ni kwamba msamaha huwa si hoja palipo na mapenzi ya dhati. Ni muhimu utafakari haya kwanza kabla hujaamua kuhusu ombi lake.

Mimi hubadilisha wapenzi

Mimi ni kijana wa umri wa miaka 22. Nikimpenda msichana na nikiwa naye kwa wiki moja pekee roho yangu inachafuka na nahisi simpendi tena. Lakini baada ya muda najiona nilimkosea. Nifanyeje?

Kupitia SMS

Roho yako ni ya kukinai mapema. Yaani unachoka mtu haraka. Lakini inabidi ujifunze kutuliza roho yako kwa mtu mmoja. Na inamaanisha itabidi upambane na roho yako ili usimchukie mtu kwa haraka hasa hao unaowaita wapenzi.