Habari Mseto

SHANGAZI: Mpenzi hajawahi kuniambia kuwa ni mke wa mtu

May 21st, 2018 3 min read

Na SHANGAZI SIZARINA

Shangazi, nimependana na mwanamke fulani kwa mwaka mmoja sasa. kuna mwanaume amekuwa akinipigia simu mara kwa mara akiniambia kama nathamini maisha yangu niachane na mke wake. Nashindwa kuelewa kwa sababu mpenzi wangu hajawahi kuniambia kuwa ni mke wa mtu. Nishauri.
Kupitia SMS

Inawezekana mwanamke huyo alikuwa na mume au mpenzi na wakaachana na sasa mwanaume huyo anaumwa kuhusu uhusiano wenu. Usichukulie vitisho hivyo kuwa mzaha kwani hujui mwanaume anayekupigia ni nani au ana nia gani. Muulize mpenzi wako kuhusu jambo hilo na pia upige ripoti kwa polisi.

 

Ushauri wako wanifaa
Shikamoo Shangazi? Mimi nakuandikia tu kukushukuru sana kwa mawaidha unayotupa katika safu hii kwani yanatufaa sana maishani. Mungu akubariki sana.
Kupitia SMS

Ahsante sana, nashukuru. Ni furaha yangu kujua kwamba ushauri wangu katika safu hii unawafaa wengine.

 

Ana pupa kupindukia
Kwako Shangazi. Nina mpenzi na tumekuwa tukilishana burudani  lakini sifurahii. Sababu ni kuwa, hanipi muda wa kutosha kujiandaa tena ana pupa nyingi. Nimekuwa nikiumia kutokana na hali hiyo. Nimemwambia mara kadhaa na hajirekebishi. Nimechoka, naomba ushauri wako.
Kupitia SMS

Mojawapo ya mambo yanayodumisha uhusiano ni watu kufahamiana vyema na kufanya mambo kwa manufaa ya kila mmoja wao. Kulingana na maelezo yako, inaonekana mwenzako anajali tu nafsi yake na ndiyo maana hajali iwapo unafurajia au la bora tu atosheleza haja yake. Kama ameshindwa kujirekebisha suluhisho ni kutengana naye.

 

Kumbe ana watoto nje
Kwako Shangazi. Nimekuwa katika ndoa kwa miaka mitatu na tumejaliwa mtoto mmoja. Juzi mume wangu alikuja nyumbani na watoto wawili akaniambia ni wake na kunitaka niwalee akisema hamtaki mama yao. Nimeshangaa sana kwa sababu hajawahi kuniambia kuwa alikuwa ameoa. Nifanye nini?
Kupitia SMS

Hili ni suala zito na linahitaji mazungumzo ya kina, sio tu kati yako na mume wako, bali pia wazazi wenu. Sababu ni kuwa, mume wako hakukwambia alikuwa ameoa na hatarajii kwamba utachukua watoto wa mwanamke mwingine uwalee bila maswali. Panga kikao na wazazi wenu mzungumze. Hata hivyo, uamuzi wa mwisho utakuwa wako.

 

Anataka kuacha shule
Hujambo Shangazi. Nina uhusiano na msichana ambaye bado anasoma. Sasa amekuwa akitaka kuacha shule ili nimuoe. Nifanye nini?
Kupitia SMS

Nimesema mara nyingi hapa kuwa, wanafunzi hawafai kushiriki mahusiano ya kimapenzi kwa sababu yanaathiri vibaya masomo yao. Pili, ninakulaumu kwa kuanzisha uhusiano na mwanafunzi huyo na kumteka akili kiasi cha kutaka kuacha shule. Kama kweli unampenda na unajali maisha yake, vunja mara moja uhusiano huo hadi amalize masomo.

 

Adai wao ni marafiki tu
Shikamoo Shangazi? Kijana mpenzi wangu alihamia mjini mwezi uliopita baada ya kupata kazi. Tumekuwa tukiwasiliana vizuri lakini rafiki yangu anayeishi mjini aliniambia amemuona mara kadhaa na mwanamke mwingine. Juzi nilimpigia simu ikapokewa na mwanamke ambaye alidai kuwa mke wake. Nilipomuuliza mpenzi wangu aliniambia kuwa wao ni marafiki tu hajamuoa. Habari hizo zimenitia huzuni. Nishauri.
Kupitia SMS

Huhitaji maelezo zaidi kujua kwamba mpenzi wako amepata mwingine. Rafiki yako alikwambia amekuwa akimuona na mwanamke mwingine na wewe mwenyewe ukathibitisha ulipopiga simu. Isitoshe, mpenzi wako pia amethibitisha ingawa anadai eti huyo ni rafiki tu. Uongo mtupu! Kama bado unafikiria una mpenzi unajidanganya.

 

Nitajuaje ni bikira?
Mimi sijaoa na sijawahi kukutana kimwili na msichana yeyote. Nahitaji bikira. Lakini nitajuaje kama msichana ni bikira. Robert Laibuni. Nkandone, Meru.
Kupitia SMS

Kaka, ingawa siku hizi suala la bikira sio muhimu sana, sitapinga uamuzi wako. Msichana bikira huwa haingiliki kwa urahisi, yaani mlango wake unakuwa mdogo sana. Na wakati mwingine baada ya kuingiliwa mara ya kwanza anaweza kutokwa na damu kidogo, ingawa sio lazima.

 

Amepoteza makali yake
Nimeolewa na nina watoto wawili. Umri wangu ni miaka 29. Mume wangu ana umri wa miaka 47. Zamani mume wangu alikuwa akiniridhisha. Lakini siku hizi hamalizi hata dakika mbili anafika ukingoni na kulala fofofo. Nikimuuliza ananiambia hajui chanzo. Nishauri.
Kupitia SMS

Wanaume wanapotimiza umri wa miaka 40 na kuendelea, baadhi yao hupunguza makali. Yaani ile kasi ya mwanzoni inapungua. Hata hivyo kuna jinsi nyingi za kuamsha hisia za mumeo. Mojawapo ikiwa ni kubadili mazoea yenu ya masuala ya mapenzi na pia kubadili mbinu za burudani. Na kama hiyo haisaidii mumuone daktari ambaye anaweza kuwapatia mbinu za kitaalamu zaidi.