Habari Mseto

SHANGAZI: Nataka kumsahau mpenzi lakini nalemewa na hisia

May 14th, 2018 2 min read

Na SHANGAZI SIZARINA

Kwako Shangazi. Mimi ni msichana mwenye umri wa miaka 22. Sijaolewa lakini nilizaa mtoto na mwanamume tuliyekuwa wapenzi. Punde tu nilipojifungua, tulianza kukosana na hatimaye tukaachana aliponitambulisha kwa mpenzi wake mwingine. Muda si mrefu, waliachana na tangu hapo tumekuwa tukikutana na kufurahia mahaba kama awali. Hata hivyo, nataka kumsahau ili niendelee na maisha yangu lakini nimeshindwa kwa sababu nampenda sana. Nipe ushauri.
Kupitia SMS

Kulingana na maelezo yako, nahisi kuwa unajaribu kubishana na moyo wako. Ukweli ni kwamba, hutaki kumuacha mwanamume huyo kama unavyodai kwa sababu unamalizia kwa kukiri kuwa unampenda sana. Na hiyo ndiyo sababu yako kumkaribisha tena katika maisha yako baada yake kuachana na mpenzi aliyemfanya akuache. Kama yuko tayari mrudiane, acha maringo. Isitoshe, ndiye baba ya mtoto wako.

 

Kumbe ni kiruka njia
Vipi Shangazi. Nina kijana mpenzi wangu ninayempenda sana. Hata hivyo, juzi niliona kwenye mitandao msichana mwengine aliye na jina sawa na langu ambaye wanaitana wapenzi. Je, nimuache?
Kupitia SMS

Kama unayosema ni ya kweli, basi ina maana kuwa huyo unayemuita mpenzi wako si mwaminifu bali ni ndumakuwili. Sasa umejua kuwa ana mpenzi mwingine kwa hivyo utaamua mwenyewe iwapo utamuacha ama utaendelea kumvumilia na tabia yake hiyo.

 

Baba mzazi aniwinda
Shikamoo Shangazi. Mimi ni msichana mwenye umri wa miaka 16 na nina tatizo ambalo nataka unisaidie kutatua. Baba yangu mzazi amekuwa akitaka tushiriki mahaba na nimeshindwa nitafanya nini.
Kupitia SMS

Maajabu ya ulimwengu hayo! Siamini kuwa baba mzazi anaweza hata kufirikia kushiriki tendo hilo na binti yake mwenyewe. Usikubali kamwe kwani kitendo hicho ni mwiko katika jamii nzima ya binadamu. Pili, mfahamishe mara moja mama yako kuhusu jambo hilo. Kama mama yako hayupo, mwambie jamaa yako mwingine uliye karibu naye ili akupe mwelekeo zaidi.

 

Mimi kivutio kwa vipusa
Hujambo Shangazi. Mimi ni kijana mwenye umri wa miaka 22. Ninashangaa kwamba, warembo wanapenda sana kunifuata wakinitaka, si kwa simu, si kwa mitandao. Sijui nina jini la kupendwa ama vipi. Nishauri.
Kupitia SMS

Je, ina maana kwamba unalalamika kwa kupendwa ama nini? Mimi ninaamini kuwa mtu hupendwa kutokana na maumbile au tabia yake. Hayo yako eti una jini la kupendwa mimi siyajui. PiIi, unafaa kushuruku badala ya kulalamika kwa sababu kuna wenzako ambao wamekuwa wakisaka wapenzi kwa muda mrefu bila kufaulu.

 

Nifanyeje nipate mpenzi?
Kwako Shangazi. Nina umri wa miaka 26 na natamani sana kuwa na mpenzi. Nifanye nini?
Kupitia SMS

Kazi yangu katika safu hii ni kutoa ushauri wala si kusaidia watu kutafuta wapenzi. Kama wewe ni mwanamume, itabidi ujitahidi kutafuta mpenzi la sivyo utaishi pweke. Kama wewe ni mwanamke, kuwa na subira na ujaribu kutangamana na wanaume wala si kuketi kitako nyumbani ukitarajia mpenzi aanguke kutoka angani.

 

Mke alianza kuzurura nje
Shangazi naomba ushauri wako. Nilikuwa na mke na tukajaliwa mtoto mmoja ambaye ninampenda sana naye pia ananipenda. Lakini mke wangu alianza kutembea sana nje na nikalazimika kumuacha. Alirudi kwao na mtoto na sijui nitafanya nini ili nimpate mtoto wangu. Nisaidie tafadhali.
Kupitia SMS

Wazazi wanapotengana na kukosa kupatana kuhusu ni nani kati yao anayefaa kuishi na mtoto au watoto, mzozo huo hutatuliwa mahakamani. Kama mke wako amekataa na mtoto na unahisi wewe ndiye unayefaa kuishi naye, itabidi utafute suluhisho kortini.

 

Nikimkumbuka nalia
Nina miaka 45. Mpenzi wangu alifariki. Usiku silali. Nikimkumbuka nalia tu. Nitafanya nini?
Kupitia SMS

Pole zangu nyingi kwa kumpoteza mwenzako. Kuombeleza na kukubali kwamba umempoteza mwenzako sio jambo la siku moja. Huchukua hatua moja hadi nyingine hadi pale akili na mwili wako vitakapokubali kwamba mwenzako hayuko tena. Lia pale unapojisikia kufanya hivyo, mwandikie barua pale unapohisi unashindwa kumtoa mawazoni. Zungumza na watu wa karibu nawe kuhusu unavyojisikia. Lakini ukiona haya yote hayasaidii, ni vizuri umuone mshauri nasaha.