Habari Mseto

SHANGAZI: Nina mke ila namtamani sana kisura fulani afisini

February 7th, 2019 2 min read

NA SHANGAZI SIZARINA

Hujambo shangazi? Nimeoa kwa miaka miwili sasa. Hata hivyo, nimependana na mwanamke fulani tunayefanya kazi pamoja. Kusema kweli ameniteka kabisa kwa penzi lake na nimeishia kumpenda hata kuliko mke wangu. Sitaki kuharibu ndoa yangu na nimejaribu kumuacha lakini nimeshindwa. Nifanyeje?

Kupitia SMS

Penzi haramu ni tamu lakini athari zake ni kali kama shubiri. Mtu akioa au kuolewa huwa ameamua kuachana na wengine wote na kujifunga kikamilifu katika ndoa. Uhusiano huo unaosema umekunasa kiasi cha kuharibu ndoa yako uliutafuta mwenyewe na ni wewe tu unayefaa kuuvunja la sivyo utavunja ndoa yako. Hali itakuwa mbaya zaidi mke wako akigundua kuwa unamchezea.

Mpenzi alinifaa kwa mengi lakini sasa amenyamaza ghafla

Shangazi nina swali kwako. Nina mpenzi ambaye tumekuwa pamoja kwa muda wa miezi sita na amekuwa akinitimizia mahitaji yangu yote. Hakuna siku niliyotaka chochote kutoka kwake nikakosa. Lakini hali imebadilika ghafla nikimpigia simu hapokei na pia SMS hajibu. Nimechanganyikiwa, naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Ni kawaida ya watu kubadili nia zao kuhusu mambo mbalimbali katika maisha yao. Hali kwamba mwenzako hataki tena kuwasiliana nawe ni dalili kuwa amebadili nia yake kuhusu uhusiano wenu na labda hataki kukwambia hivyo. Mpe muda usiozidi mwezi mmoja uone kama atawasiliana nawe na asipofanya hivyo ujue huo ndio mwisho wa uhusiano wenu.

Sipendi anavyoongea na mkewe wa zamani

Shangazi pokea salamu zangu. Nina umri wa miaka 21, nimeolewa na tumejaliwa mtoto mmoja. Mume wangu alinioa akiwa na watoto wawili aliozaa na mwanamke mwingine. Shida iliyopo ni kwamba bado wanawasiliana na mwanamke huyo na tumekuwa tukikosana mara kwa mara kuhusu jambo hilo. Nifanyeje?

Kupitia SMS

Ninaamini kwamba mwanaume huyo alikuoa kwa sababu hakutaka kumuoa mama ya watoto hao. Hiyo ndiyo sababu alikuletea watoto hao ili uwalee kama wako na hafai kuendeleza uhusiano na mwanamke huyo hata kama ni mawasiliano pekee. Kama unahisi uhusiano huo unaathiri vibaya ndoa yenu, mwelezee wazi kuwa huwezi kuvumilia hali hiyo ili aamue mwenyewe anavyotaka.

Hanipigii simu, hata SMS ni shida

Hujambo shangazi? Nina uhusiano na kijana fulani na ninampendasa sana. Tatizo lake ni kwamba hataki kunipigia simu au kunitumia SMS. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Ni lazima mwenzako ana sababu ya kutotaka kuwasiliana nawe kwa simu. Kama hujawahi kumuuliza, ni muhimu ufanye hivyo ili ujue ni sababu gani hiyo ndipo ujue hatua ya kuchukua.

Mama watoto amepata kazi ya baa

Hujambo shangazi? Mimi nina mke na watoto wawili. Sasa mama watoto ametafuta kazi ya kuuza pombe katika baa na ameniambia hatarudi kwangu. Nifanyeje?

Kupitia SMS

Kitendo na matamshi ya mke wako ni dalili kwamba hana haja na ndoa. Kazi ya baa si mbaya lakini kwake kusema kwamba hatarudi kwako ina maana kuwa amejiondoa katika ndoa hiyo. Zungumza naye ujue ni kwa nini ameamua kuchukua hatua hiyo. Labda ameona kasoro fulani katika maisha yenu ambayo mnaweza kurekebisha.

Yawezekana ataniacha?

Kwako shangazi. Niliolewa kwa mwaka mmoja lakini sikuweza kupata mtoto na hali hiyo ilimfanya mume wangu aniache. Sasa nimechumbiana na mwanaume mwingine na yuko tayari kunioa. Lakini nahofia yeye pia ataniacha nikishindwa kumzalia. Nishauri tafadhali.

Kupitia SMS

Hujaelezea iwapo hali yako hiyo ilithibitishwa na mtaalamu wa afya ya uzazi ama unadhania tu kuwa una kasoro. Kama hujakaguliwa na daktari, ni muhimu ufanye hivyo kwani huenda huna tatizo lolote. Isitoshe, kuna hali zinazoweza kurekebishwa. Na iwapo unajua kwa hakika huna uwezo wa kupata mtoto, ni heri umwambie ukweli mwanaume huyo.