Makala

SHANGAZI: Nina mpenzi ila jamaa mwingine anirai nimpe nafasi

July 26th, 2019 2 min read

Na SHANGAZI

VIPI shangazi? Nina mpenzi lakini kuna mwanamume mwingine ambaye amekuwa akiniandama kwa muda mrefu akidai ananipenda. Nimemwambia wazi kuwa nina mpenzi lakini anaomba nimpe nafasi ili anionyeshe jinsi anavyonipenda. Nifanyeje?

Kupitia SMS

Ninaamini mnapendana kwa dhati na mpenzi wako kwa hivyo huhitaji kumpa nafasi mwanamume mwingine ili akuonyeshe mapenzi. Mwambie wazi kwamba hakuna nafasi ya mtu mwingine moyoni mwako kwa sababu umetosheka na uliye naye.

 

Nilimwambia nimeoa lakini bado hasikii

Vipi shangazi? Kuna msichana fulani anayeniambia ananipenda na nikimwambia nimeoa hataki kuniamini. Hata anataka kunionjesha asali kwa lazima. Sijui nitamfanya nini. Nishauri.

Kupitia SMS

Hakuna mtu anayeweza kukulazimisha umpende. Unasema una mke kwa hivyo unafaa kuheshimu ndoa yako kwa kumuepuka kabisa msichana huyo kwani huenda nia yake ni kuvuruga ndoa yako. Hilo la kukulambisha asali kwa lazima ni upuuzi tu na wewe mwenyewe unajua hivyo.

 

Aliniacha ghafla akatoweka, imekuwa vigumu kumsahau

Shangazi natumai wewe ni mzima. Tafadhali pokea salamu zangu. Nilikuwa na msichana mpenzi wangu hata tukazaa mtoto pamoja. Lakini siku moja nilishtuka ghafla aliponiambia tuachane kisha akatoweka. Nimejaribu sana kumsahau lakini nimeshindwa. Nishauri.

Kupitia SMS

Uhusiano wa kimapenzi hutokana na uamuzi wa mtu binafsi. Ukihisi umetosha uhusiano una haki ya kujiondoa. Hali kwamba umeshindwa kumsahau ni ishara kuwa ulimpenda kwa dhati. Hata hivyo, huna budi kukubali uamuzi wake huo ndipo uweze kuendelea na maisha yako. Kuwa na subira, hatimaye ukweli huo utazama moyoni na utaweza kumsahau.

 

Nashuku anampenda

Hujambo shangazi? Nina mwanamke mpenzi wangu ambaye ninampenda kwa dhati. Tulipokutana alikuwa ameachana na mpenzi wake wa kwanza baada ya kugundua alikuwa na wapenzi wengine wa pembeni. Ajabu ni kuwa mpenzi wangu anapenda sana kumtaja sana mwanamume huyo na ninashuku kuwa bado anampenda. Nishauri.

Kupitia SMS

Ingawa hujaelezea huwa anamtaja mpenzi wake wa awali kuhusiana na nini, ni muhimu umwelezee unavyohisi kuhusu jambo hilo. Pili, hali kwamba anapenda kumtaja si thibitisho kuwa anampenda. Hilo ni suala unaloweza kumuuliza ili ujue maana yake.

 

Nimetafutiwa mke

Vipi shangazi? Nimependana na mwanamke aliye na kila kitu ambacho ningetaka kwa mke. Ni mrembo sana na pia ana tabia nzuri. Hata hivyo, wazazi wangu wamenitafutia mwanamke mwingine ambaye wanasisitiza nimuoe.

Kupitia SMS

Sijui ni kwa nini unataka ushauri wangu ilhali inaonekana tayari umekata kauli kufuata maagizo ya wazazi wako kumuoa mwanamke waliyekutafutia. Hata hivyo, ukweli ni kuwa mapenzi na ndoa ni masuala ya moyoni na mke anafaa kuwa chaguo la mtu binafsi wala si kutafutiwa. Hoja si mke tu bali mapenzi tena ya dhati. Zingatia sana hilo katika uamuzi wako.

 

Asema wao urafiki tu

Kwako shangazi. Ninampenda sana mwanamke mpenzi wangu. Hata hivyo, nimemuona mara nyingi akiwa na wanaume wengine na nikimuuliza anasema ni marafiki tu. Nifanyeje?

Kupitia SMS

Inaonekana unashuku kwamba mpenzi wako si mwaminifu kwako ingawa huna hakika ya jambo hilo. Mambo ni mawili; ukubali na kuamini anavyokwambia ama uachane naye badala ya kuendelea kuhangaisha moyo wako kwa kumshuku.

 

Sijawahi kumwamini

Habari yako shangazi? Nina mpenzi ambaye tumekuwa katika uhusiano kwa karibu mwaka sasa lakini sijawahi kumwamini. Nifanyeje?

Kupitia SMS

Kama una sababu nzuri za kutomwamini mpenzi wako, haina haja uendelee kupoteza wakati wako kwake. Achana naye utafute mwingine unayeweza kumwamini.