Makala

SHANGAZI: Tangu nimshauri tukapimwe, mpenzi ananihepa

December 1st, 2019 2 min read

NA SHANGAZI SIZARINA

Hujambo Shangazi? Nimekuwa na mwanamke mpenzi wangu kwa karibu mwaka mmoja na nimetosheka kwamba ndiye anayefaa kuwa mke wangu. Kwa sababu hiyo, juzi nilimuomba twende tukapimwe tujue hali yetu. Tangu siku hiyo amekuwa akinihepa. Bado nampenda na sijui nitafanya nini. Nishauri.

Kupitia SMS

Ni jambo la kawaida siku hizi kwa wapenzi kupimwa ili kujua hali yao hasa kama wana mpango wa kufunga ndoa. Hali kwamba mpenzi wako ameanza kukuhepa baada ya wewe kumshauri mkapimwe ni ishara kuwa kuna kitu anachoogopa. Usikubali kurudi katika uhusiano huo kama hataki kupimwa.

Bado wanawasiliana

Kwako Shangazi. Mwanamume tuliyependana aliniacha akashikana na mwanamke mwingine. Hata mwezi haukuisha walikosana akarudi kwangu na kuniomba msamaha. Ninampenda, kwa hivyo nilikubali. Sasa nimegundua amekuwa akiwasiliana na pia kuonana kisiri na huyo mwingine. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Ulifanya makossa kumpa nafasi tena mwanamume huyo bila kumwekea masharti ya uhusiano wenu mpya. Iwapo alikuacha kwa ajili ya mwingine na anaendelea kukusaliti, sioni haja yako kuendelea naye.

Nahisi anagawa nje

Vipi Shangazi? Nimeoa na ninampenda sana mke wangu. Hata hivyo, ninahisi kama anatembea nje ya ndoa ingawa sina ushahidi. Je, ni fikira zangu tu ama ni kweli?

Kupitia SMS

Huwezi kumshuku mtu bure tu bila kuona dalili za kuonyesha kuwa si mwaminifu. Unasema unampenda sana mke wako na inawezekana kwamba hisia zako hizo zinatokana na wivu. Hadi utakapoona ishara kamili za kuonyesha kuwa anatoka nje, endelea kumwamini.

Hajibu simu wala SMS

Vipi Shangazi? Msichana mpenzi wangu wa miaka mitatu amekatiza mawasiliano ghafla. Nikimpigia simu hapokei na SMS pia hajibu. Sielewi sababu kwani sijamkosea. Nampenda sana, nisaidie.

Kupitia SMS

Labda kuna mambo anayojaribu kuchanganua kuhusu uhusiano wenu na anahitaji utulivu wa akili. Lakini hali hiyo ikiendelea, itabidi uchukue hatua zaidi ili ujue kinachoendelea. Labda umtembelee anakoishi mzungumze ana kwa ana.

Mpenziwe ndugu anisaka

Shikamoo Shangazi. Nina umri wa miaka 21 na bado sijawahi kuwa na mpenzi. Kuna msichana mpenzi wa ndugu yangu ambaye amekuwa akinishawishi tuwe na uhusiano wa kisiri akidai eti ananipenda hivi kwamba amekuwa akiota nami kila siku. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Msichana huyo ni hatari. Hana nia nzuri kwako wala kwa ndugu yako. Kama kweli anampenda kwa dhati ndugu yako, anatafuta nini kwako. Usipochunga atawafanya mkosane. Kataa kabisa mambo yake na akisisitiza, umwambie utamshtaki kwa kaka yako.

Amekataa kuondoka

Shangazi nahitaji ushauri wako. Nilimpa mimba mpenzi wangu ingawa sikuwa na mpango wa kumuoa. Aliniomba nimruhusu kuishi kwangu hadi ajifungue kisha arudi kwao. Hatimaye amepata mtoto lakini amekataa kuondoka. Nifanyeje?

Kupitia SMS

Huo wako ni msiba wa kujitakia kaka. Ulimhadaa mtoto wa wenyewe kwamba unampenda kumbe ulitaka tu kukidhi tamaa zako. Kumruhusu kuishi kwako ni sawa na kumkubali kuwa mke wako na huwezi kumfukuza kwa sababu tayari ana mtoto wako. Ulijitwika mwenyewe mzigo huo na huna budi ila kuubeba.

Mamake hanipendi

Vipi Shangazi? Nina mume ambaye mama yake alifanya tutengane kwa sababu amekuwa akiongea vibaya akisema yeye si mama yetu. Mwanamume anadai ananipenda sana na mimi pia nampenda sana. Nifanyeje?

Kupitia SMS

Nashangaa kwamba mlitengana kwa sababu ya msimamo wa mama ya mume wako kuhusu ndoa yenu. Kumbuka kuwa mapenzi na ndoa ni kati yenu tu, mzazi hana haki ya kuingilia. Kama mnapendana rudini katika ndoa.

Alisema hakunipenda

Nilioa kwa miezi mitatu, tukaachana mwezi wa nne. Nimeshindwa kumsahau na alisema hakunipenda.

Kupitia SMS

Ukweli huwa unauma sana, tena ukitoka mdomoni mwa mtu unayempenda kwa dhati. Lakini mwenzako amekueleza ukweli wa hisia zake kwako. Huwezi kulazimisha hisia za mtu, hivyo pamoja na uchungu wote unaohisi, utajitendea haki iwapo utakubali yaliyotokea na usonge mbele. iwapo unaona wazi hakuna uwezekano wa kuokoa ndoa yenu.