Shanky Abbs msanii anayefuata nyayo za  baba’ke

Shanky Abbs msanii anayefuata nyayo za baba’ke

Na JOHN KIMWERE

ANASEMA kwamba amepania kujituma mithili ya mchwa anakolenga kuibuka kati ya wanamaigizo tajika miaka ijayo.

Shankaroun Abrahams ama ukipenda Shanky Abbs anaorodheshwa kati ya waigizaji chipukizi wanaolenga kutinga hadhi ya kimataifa ambapo amekumbatia uigizaji na uana mitindo. Binti huyo aliyetua duniani mwaka 1993 kando na uigizaji pia anafanya na kampuni ya usafiri licha ya kwamba amehitimu kama mwana habari.

Ni chipukizi anayepania kupambana mwanzo mwisho kuhakikisha anatimiza azma yake kuibuka msanii mahiri kama Gal Gadot mzawa wa Israel aliyeshiriki filamu maarufu kama Wonder Woman.

”Kila mtu huamini anatosha mboga katika taaluma yake ambapo bila kujipigia debe nimefanya kazi nyingi tu zinanidhihirishia kuwa nina talanta ya uigizaji,” amesema na kuongeza kuwa anataka kutinga kiwango cha waigizaji wa Hollywood.

Binti huyo anasema kuwa alianza kushiriki uigizaji mwaka 2013. Katika mwanzo wa ngoma anasema kuwa alifikia uamuzi huo alipovutiwa na maigizo baada ya kutazama filamu iitwayo Tomb Raider yake Angelina Jolie mzawa wa Marekani. Anadokeza kuwa anafuata nyayo za babake mzazi ambaye pia ni mwana maigizo.

Mwigizaji chipukizi Shankaroun Abrahams ama ukipenda Shanky Abbs…Picha/JOHN KIMWERE

”Kusema pia nilipata motisha zaidi kujiunga na maigizo katika matangazo ya kibiashara baada ya kumtazama kazi zake babangu ,” akasema. Binti huyu anasema kuwa ndani ya miaka mitano ijayo analenga kuwa msanii bora na tajika nchini na Afrika kwa jumla.

Chozi na Varshita

Anasema anajivunia kushiriki filamu kadhaa ambazo tayari zimepata mpenyo na kupeperushwa kupitia runinga tofauti ikiwamo Auntie Boss (NTV), Njoro wa Uba, Varshita na Chozi zote Maisha Magic East bila kusahau A covid XIX Situation in Nairobi chini ya brandi iitwayo Safari Media Ke-Isolated.

Na Pia amebahatika kufanya matangaza ya kibiashara mara kadhaa ikiwamo Co-operative Bank (MGM Studios LTD), SWVL (Tufilamu Pictures).

Charlize Theron

Kimataifa dada huyu angependa kufanya kazi na waigizaji mahiri kama Charlize Theron wa Afrika Kusini ambaye hushiriki filamu za Hollywood. Charlize ameshiriki vipindi nyingi tu ikiwamo ‘Atomic Blonde’ na ‘Fast and the Furious 9’ kati ya zingine.

Pia yupo mwenzio kutoka taifa hilo, Pearl Thusi anayejivunia kushiriki kipindi ambapo hupatikana kupitia Netflix kiitwacho Queen Sono. Kwa wenzie hapa nchini anasema angependa sana kujikuta jukwaa moja nao Sanaipei Tande anayeshiriki ‘Kina’ ‘Aziza’ na Sheila Munyiva wa vipindi vya ‘Rafiki,’ pia stage play ya Sarafina.

Changamoto

Ansema kuwa amepitia milima na mabonde katika uigizaji ikiwamo malipo duni bila kuweka katika kaburi la sahau kushawishiwa kuwa katika mahusiano ya kimapenzi ili kupata ajira. Anaonya wenzie kamwe wasikubali kujihusisha na utumwa wa mahusiano ya kimapenzi ili kupata ajira. ”Kiukweli hali hiyo ni kudhalilisha mwanamke na kumshusha hadhi,” akasema.

Mwigizaji chipukizi Shankaroun Abrahams ama ukipenda Shanky Abbs..Picha/JOHN KIMWERE

 

You can share this post!

Chinese wakali wamlemea, uigizaji wampa ajira

Buccaneers inataka taji la ligi kuu ndani ya miaka miwili...

T L