Michezo

Shaqiri asema alitamani Liverpool ikutanishwe na Bayern

February 18th, 2019 1 min read

NA CECIL ODONGO

WINGA wa Liverpool Xherdan Shaqiri sasa anadai kwamba aliitaka timu yake ikutane na Bayern Munich kabla ya kuandaliwa kwa droo ya timu 16 ya kuwania taji la Klabu Bingwa Barani Uropa (UEFA).

Raia huyo wa Uswizi amesema mechi ya mkondo wa kwanza kati ya timu hizo mbili ugani Anfield Jumanne Februari 19 itampa jukwaa bora la kudhihirishia timu yake ya zamani kwamba walifanya kosa kumwondoa kikosini na kumpeleka Stoke City kwa mkopo.

Shaqiri alikuwa mcheza wa kutegemewa wa Bayern Munich kati ya mwaka 2012 na  2015, timu hiyo ilipomchoka na kumhamisha kwa mkopo hadi Stoke City kisha baadaye ikampiga mnada kwa washiriki hao wa zamani wa Ligi Kuu ya Uingereza(EPL).

“Nafurahi sana jinsi droo hiyo ilivyofanywa kwasababu nilitaka sana kukutana na Bayern Munich na wachezaji wenzangu timuni kipindi kile. Nasubiri sana kusakata mechi hiyo kwa hamu na hamumu,”

“Nilikuwa na wakati mzuri sana Bayern kwa kuwa tulishinda mataji mengi likiwemo taji la Uchampioni kwa sababu ya ubora wa timu yetu wakati huo,” akasema Shaqiri.

Ingawa hivyo, sadfa katika mpambano huo ni kwamba kocha wa Liverpool Jurgen Klopp ataongoza Shaqiri kukutana na timu ya Bayern waliompokonya taji la kipute hicho mdomoni msimu wa 2012-13, wakati huo akiifundisha Borussia Dortmund. Mchuano huo uliosakatwa ugani Wembley uliishia 2-1 kwa faida ya Bayern Munich.

Mechi hiyo ya UEFA hata hivyo itakuwa mtihani mkubwa kwa Liverpool ambao wanasaka ubingwa wa EPL pamoja na Manchester City huku wakiratibishwa kukutana na Manchester United, Everton na Tottenham Hot Spurs kabla ya mwisho wa mwezi huu wa Machi.