Michezo

Sharp Boys na Young Elephants wajivunia ushindi

July 22nd, 2019 1 min read

Na JOHN KIMWERE

SHARP Boys na Young Elephants FC za wavulana wasiozidi umri wa miaka 14 zilitangulia kutwaa uongozi wa mapema kwenye mechi za Ligi ya KYSD baada ya kila moja kuandikisha ufanisi wa magoli 7-1 dhidi ya State Rangers na Locomotive FC mtawalia uwanjani KYSD Kamukunji, Nairobi.

Nayo Pro Soccer Foundation ilikandamiza Young Achievers kwa magoli 4-0 na kukamata tatu bora kwa alama sita. Sharp Boys kati ya vikosi vinavyopigiwa chapuo kutesa msimu huu ilinasa ushindi huo baada ya Victor Aguya na Victor Mugambi kufunga mabao matatu na mawili mtawalia, nao Erick Mutiso na Edward Njuguna kila mmoja aliitingia goli moja.

Wafungaji wa Young Elephants walikuwa Michael Otieno na Kevin Karanja magoli mawili kila mmoja huku Ben Kieti, Tony Mutua, Collins Omondi na Dennis Kilonzo kila mmoja akicheka na wavu mara moja.

”Nashukuru chipukizi wangu kwa kutwaa ushindi mnono dhidi ya wapinzani wetu,” kocha wa Sharp Boys, Boniface Kyalo alisema na kuongeza kuwa tayari kikosi chake kimeanza safari ya kutwaa taji kwa mara ya kwanza.

Sharp Boys inaongoza kwa alama sita sawa na Young Elephants pia Pro Soccer Foundation zinazofuatana kwa usajli huo tofauti ikiwa idadi ya mabao.

Kwenye matokeo hayo, MASA ilishinda Gravo Legends magoli 4-3, Fearless FC ilizabwa magoli 4-1 na Lemans FC, Tico Raiders iliirarua Pumwani Ajax kwa magoli 6-4 nayo Pumwani Foundation ilirandwa goli 1-0 na Volcano FC.