Michezo

Shauri Moyo Sportiff yalenga Nane Bora

August 25th, 2019 2 min read

Na JOHN KIMWERE

TIMU ya Shauri Moyo Sportiff ni miongoni mwa vikosi vinavyoshiriki kipute cha Super Eight Premier League (S8PL) vinavyolenga kujituma mithili ya mchwa ili kuibuka kati ya nane bora muhula huu.

Aidha imeorodheshwa kati ya timu zilizoanzishwa zaidi ya miaka kumi iliyopita katika Kaunti ya Nairobi.

Michezo ya kinyang’anyiro hicho msimu huu kamwe siyo mteremko mbali inapigiwa chapuo kushusha upinzani wa kufa mtu baina ya mahasimu wakuu ikiwamo Wasomi wa Chuo Kikuu cha Kiufundi cha Kenya (TUK), Githurai Allstars, Melta Kabiria, Mathare Flames awali ikifahamika kama Zamalek, Team Umeme bila kuweka katika kaburi la sahau mabingwa watetezi Jericho Allstars.

Bila shaka kati ya vikosi hivyo, Meltah Kabiria na Githurai Allstars zimeibuka kati ya wapinzani walioendelea kuonyesha ushindani mkali kwenye kampeni za ngarambe ya msimu huu.

”Mashindano ya muhula huu yanaendelea kuibua upinzani wa aina yake hali inayofanya timu nyingi kujipata kwenye wakati mgumu,” kocha wa Shauri Moyo Collins ‘Collo’ Okoth alisema na kuongeza kuwa ukosefu wa ufadhili umepelekea wachezaji wengi wa kikosi hicho kukosa hushirikiano mzuri kwenye kampeni za kuwania taji hilo.

”Bila kujisifia nina wanasoka wazuri ambao wanaweza kutesa wapinzani wao na kumaliza miongoni mwa nafasi bora kama ilivyokuwa muhula uliyopita. Lakini tatizo kubwa ni kwamba imekuwa vigumu kwetu kuwaweka wachezaji vizuri kimahitaji hali ambayo imefanya wengi kukimbia kusaka matunda mazuri kwingine,” ofisa mkuu wa klabu hiyo Joab Ogolla anasema.

Kadhalika anaongeza kuwa suala hilo limefanya wengi kutofika mazoezini na kuchangia kutofanya vizuri kwenye mechi za ligi.

Anadokeza kuwa endapo wanaweza kupata ufadhili ana imani kikosi hicho kinauweza wa kufanya bora zaidi kwenye mashindano mbali mbali pia kupata nafasi kushiriki Ligi za upeo wa juu nchini.

Ogolla anashukuru Extreme Sports waandalizi wa S8PL kwa kazi wanayofanya ingawa inapitia wakati mgumu baada ya SportPesa kujiondoa. Shauri Moyo Sportiff inashirikisha wachezaji kama: Julius Muhia, Mark Aura, Nicholas Cepha, Silas Onyango, Hesborn Omondi, Douglas Janja (nahodha), Maxi Matano, Frank Robert, Zeppaline Andefwa, Kevin Kavehele, William Njoroge, Rodgers Subira na Bramwel Ambetsa kati ya wengine.

Shauri Moyo Sportiff iliyoasisiwa mwaka 1983 inajivunia kukuza wachana nyavu wengi tu ingawa baadhi yao wamestaafu lakini wapo wengine ambao huchezea timu zingine zinazoshiriki mechi za FKF.

Kwa kutaja wachache tu wapo Anthony Otieno ambaye husakata soka la kulipwa nchini Zambia, Lutumba Nzunzi aliyekuwa akichezea Mt Kenya msimu uliyopita. Pia wapo Brian Magonya (Sofapaka FC), Chrispinus Onyango (KCB) na John Otieno (Bandari FC).

Kwenye msimamo wa kipute hicho, Jericho Allstars inaongoza kwa alama 39, moja mbele ya Meltah Kabiria baada ya kucheza mechi 20 kila moja.

Nayo Githurai Allstars ndiyo ya nne kwa kuzoa pointi 37, mbili mbele ya Mathare Flames huku TUK ikifunga tano bora kwa kufikisha alama 34.

Baada ya kusakata patashika 20 nayo Shauri Moyo Sportiff imeshikilia nafasi ya 14 kwa kukusanya alama 20, sita mbele ya mabingwa Kawangware United.