HabariSiasa

Shebesh atoa amri machifu wavumishe BBI mashinani

December 11th, 2019 2 min read

Na CHARLES WANYORO

Waziri Msaidizi katika Wizara ya Jinsia Bi Rachel Shebesh, amewaamrisha machifu na manaibu wao kuwafunza Wakenya kuhusu ripoti ya Jopo la Maridhiano (BBI) kwenye mikutano ya hadhara katika maeneo yao.

Bi Shebesh alisema kuwa hilo litawasaidia Wakenya katika maeneo ya mashinani kuifahamu ripoti hiyo kwa undani.

Alisema kuwa uongozi wa mikoa umo chini ya Afisi ya Rais, hivyo machifu wanapaswa kuhakikisha kuwa wamefikisha ujumbe huo kwa Wakenya wote.

Alitoa kauli hiyo jana akiwahutubia machifu na manaibu chifu kutoka Kaunti ya Meru katika Shule ya Upili ya Wasichana ya Kaaga.

Mkutano huo ulilenga kupanga mikakati ya utekelezaji wa agizo la Rais Uhuru Kenyatta kumaliza tohara miongoni mwa wasichana kufikia mwaka 2022.

Bi Shebesh alimwagiza kamishna wa kaunti hiyo Bw Allan Macharia kuchapisha nakala za ripoti hiyo na kuziwasilisha kwa wenyeji. Alisema kuwa machifu hawana kisingizio chochote cha kutofahamu yaliyopo kwenye ripoti hiyo.

Aliwaonya dhidi ya kupuuzilia mbali ripoti hiyo, akisema kuwa wanategemewa sana na umma kuwaeleza na kuwafafanulia yale yaliyo kwenye ripoti hiyo.

Kiongozi huyo aliwaomba machifu kuwafafanulia wananchi kuhusu ripoti hiyo, hasa kipengele kinachoeleza kuwa serikali kuu itaongeza mgao wa fedha katika maeneo ya mashinani.

Alisema kuwa ikiwa ripoti hiyo itatekelezwa, itaongeza fedha zinazotengewa maeneo hayo, hali ambayo itawafaa sana wananchi.

“Ikiwa huko tayari kuunga mkono ripoti hiyo, basi unapaswa kunyamaza. Wakati mwingine unawapata machifu katika mikutano ya umma wakiwaambia wenyeji kwamba hawajaisoma ripoti. Huwezi kuwa serikalini, ilhali unashindwa kuwafafanulia wananchi kuhusu ripoti hiyo.

Rais alisema kwamba hii ni ripoti ya umma. Wakati machifu wanaandaa mikutano yao, lazima wawaruhusu wananchi kuijadili na kuuliza maswali, kwani si wote walio na nakala,” akasema Bi Shebesh.

Kuhusu suala la ukeketaji, Bi Shebesh alisema kuwa kiwango hicho kinaendelea kupungua nchini.

Kwa sasa, idadi hiyo ni asilimia 21 ikilinganishwa na asilimia 27 mnamo 2008/2009 na asilimia 32 mnamo 2003.

Alitaja mikakati ya serikali na mashirika ya kijamii kama mojawapo ya sababu ambazo zimechangia kupungua kwake.

Hivyo, aliwaomba maafisa hao kushirikiana na mashirika ya kidini kukabili tamaduni hiyo katika maeneo yao.