Sheffield United yaduwaza Manchester United ligini kwa kuichapa 2-1 ugani Old Trafford

Sheffield United yaduwaza Manchester United ligini kwa kuichapa 2-1 ugani Old Trafford

Na MASHIRIKA

MANCHESTER United walipoteza fursa nzuri ya kurejea kileleni mwa jedwali la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo Januari 27 baada ya kupokezwa kichapo cha 2-1 kutoka kwa Sheffield United uwanjani Old Trafford.

Ushindi huo ulikuwa wa pili kwa Sheffield United wanaovuta mkia kwenye msimamo wa jedwali la EPL kusajili hadi kufikia sasa ligini msimu huu. Aidha, ilikuwa mara ya kwanza kwa Sheffield United kupiga Man-United ugani Old Trafford tangu 1992.

Chini ya kocha Ole Gunnar Solskjaer, Man-United walihitaji kutia kapuni alama zote tatu ili kuwaruka watani wao Manchester City na kurejea kileleni mwa jedwali.

Man-City kwa sasa wanadhibiti usukani wa jedwali la EPL kwa alama 41, moja zaidi kuliko Man-United ambao wamesakata mchuano mmoja zaidi kuliko mabingwa hao wa zamani wanaotiwa makali na kocha Pep Guardiola.

Leicester City waliowalazimishia Everton sare ya 1-1 uwanjani King Power katika mechi nyingine ya Jumatano usiku kwa sasa wanashikilia nafasi ya tatu kwa alama 39, nne mbele ya West Ham United wanaofunga mduara wa nne-bora.

Kujikwaa kwa Man-United kunatarajiwa sasa kuwapa Man-City fursa ya kufungua mwanya wa alama nne kileleni mwa jedwali huku matokeo yao dhidi ya Sheffield yakitazamiwa pia kuchochea ari ya wapinzani wao wakuu wakiwemo Tottenham Hotspur na mabingwa watetezi Liverpool.

Sheffield United ya kocha Chris Wilder walifungua ukurasa wa mabao kupitia kwa Kean Bryan katika dakika ya 23 kabla ya Anthony Martial kuchangia bao lililofungwa na Harry Maguire aliyesawazisha mambo katika dakika ya 64.

Bao la Maguire liliamsha makali ya Man-United walioshambulia zaidi lango la Sheffield United lililokuwa chini ya ulinzi wa kipa Aaron Ramsdale aliyefanya kazi ya ziada na kuzidhibiti fataki kutoka kwa Paul Pogba, Bruno Fernandes, Martial na Marcus Rashford.

Ingawa hivyo, ni Sheffield United ndio waliopata bao la ushindi katika dakika ya 74 kupitia kwa beki Axel Tuanzebe aliyejifunga baada ya kushindwa kudhibiti kombora la Oliver Burke aliyetokea benchi mwanzoni mwa kipindi cha pili.

Licha ya kuangusha Man-United, Sheffied United wangali mkiani mwa jedwali la EPL kwa alama nane, tatu nyuma ya Fulham ambao kwa pamoja na West Bromwich Albion, wako katika hatari ya kuteremshwa ngazi mwishoni mwa kampeni za muhula huu.

Kichapo kutoka kwa Sheffield United kilikuwa cha kwanza kwa Man-United kupokea kutokana na mechi 13 zilizopita za EPL tangu wapepetwe na Arsenal 1-0 mnamo Novemba 2020.

Man-United ambao hawajapoteza mchuano wowote wa nyumbani hadi kufikia sasa msimu huu, wanatarajiwa kujinyanyua dhidi ya Arsenal watakaowaalika uwanjani Emirates kwa gozi kali la EPL mnamo Januari 30. Kwa upande wao, Sheffield United watakuwa na kibarua kingine kizito dhidi ya viongozi wa jedwali Man-City ugani Etihad.

You can share this post!

Wafalme wa kudandia madaraka

Polisi wachunguza kisa cha mwanafunzi wa Kidato cha Nne...