Michezo

Sheffield Wednesday wapokonywa alama 12 za msimu ujao

August 4th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

KIKOSI cha Sheffield Wednesday kimepokonywa alama 12 za kampeni ya msimu ujao wa 2020-21 na Jopo Huru la Nidhamu la soka ya Uingereza (EFL) kwa hatia ya kukiuka kanuni za matumizi ya fedha.

Miongoni mwa makosa yaliyofanywa na Sheffield ambao wanashiriki Ligi ya Daraja la Kwanza (Championship) ni kujumisha fedha za mauzo ya uwanja wao wa nyumbani wa Hillborough katika hesabu za msimu wa 2017-18 licha ya uga huo kunadiwa mwaka mmoja baadaye.

Hatia nyingine ni ukosefu wa uaminifu, kuficha habari muhimu na kuzuia kimakusudi vinara wa EFL kufanyia akaunti zao ukaguzi wa hesabu za fedha.

Wasimamizi wa Sheffield hata hivyo wamesema kwamba “wamefadhaishwa sana” na adhabu iliyotolewa dhidi yao.

Iwapo alama za Sheffield zingeondolewa katika jumla ya pointi walizojizolea muhula huu wa 2019-20, basi wangelazimika kushuka ngazi hadi Ligi ya Daraja la Pili (League One) kwa kampeni za muhula ujao.

Hatua hiyo ingaliwaokoa pia Charlton Athletic dhidi ya kuteremshwa ngazi kwenye Championship kwa minajili ya msimu wa 2020-21.

Sheffield wamefichua kwamba wanasubiri kusoma maandishi ya sababu zote zilizochangia kuadhibiwa kwao kabla ya kuamua kukata rufaa au la.

Iliwachukuwa Sheffiled takriba miezi tisa na siku 17 kujua adhabu dhidi yao kwa kosa waliloshtakiwa kwalo kwa mara ya kwanza kabisa mnamo Novemba 2019.

Jopo Huru la Nidhamu lililokuwa likishughulikia kesi dhidi ya Sheffield lilianza kazi mnamo Juni 2020, wakati ambapo kampeni za msimu huu kampeni za muhula huu zilikuwa tayari zimevurugwa kabisa na janga la corona.

Mapema Julai 2020, kocha Garry Monk wa Sheffield alisema “haikuwa na maana wala mantiki yoyote” kwa kikosi chake kuendelea kusubiri maamuzi ya kesi dhidi yao wakati ambapo haki ilikuwa tayari imecheleweshwa “kimakusudi”.

Maamuzi ya kuondolewa kwa alama 12 katika kampeni zao za ligi msimu ujao yanatolewa siku tisa baada ya msimu huu uliorefushwa kwa sababu ya ugonjwa wa Covid-19 kutamatika.

Kuuzwa kwa uwanja wa Hillsborough kwa kima cha Sh8.4 bilioni na fedha hizo kujumuishwa kwenye hesabu za mwaka wa kifedha wa 2017-18 kulimaanisha kwamba Sheffield wanaandikisha faida ya Sh350 milioni kabla ya kutozwa ushuru.

Bila hesabu hiyo, ingemaanisha kwamba kikosi hicho kinakadiria hasara ya Sh4.9 bilioni ambao ingefuata hasara ya Sh1.3 bilioni na Sh2.9 bilioni katika misimu miwili ya awali.

Kwa mujibu wa kanuni mpya za EFL zinazodhibiti matumizi ya fedha miongoni mwa vikosi vya soka ya Uingereza, klabu za Championship zinaruhusiwa kukadiria hasara ya hadi Sh5.5 bilioni pekee katika kipindi cha jumla ya misimu mitatu mfululizo.

Ingawa Sheffield inakuwa kikosi cha kwanza kuadhibiwa kwa hatia ya kujumuisha fedha za mauzo ya uwanja kwenye akaunti zao, klabu hiyo si ya kwanza kuwahi kufanya kosa hilo lililowahi pia kuhusishwa na Derby County na Aston Villa.