Michezo

Sherehe za Ingwe@60 zaanza kwa mbwembwe na madoido

March 12th, 2024 1 min read

Na JOHN ASHIHUNDU

SHANGWE, nderemo na vigelegele vilihanikiza mitaa mbalimbali ya Nairobi wakati mashabiki wa soka walijitokeza kuanza sherehe za miaka 60 tangu kubuniwa kwa klabu ya AFC Leopards.

Wachezaji wa klabu hiyo waliungana na mashabiki kwa shughuli mbali mbali za kijamii kama upanzi wa miti, kutembelea watoto wanaoishi atika makao ya watoto kwa ajili ya kuadhimisha siku hiyo mihumu, huku kilele chake kikitarajiwa kufanyika Machi 24 katika Uwanja wa Kitaifa wa Nyayo.

Wakiongoza na mlezi wa klabu hiyo, Alex Muteshi akiandamana na mwenyekiti wa kamati andalizi ya sherehe hizo, Vincent Shimoli mashabiki wa Ingwe watakusanyika mtaani Shauri Moyo kwa nyumba ya aliyekuwa mmoja wa waanzilishi wa klabu hiyo, marehemu Israel Mutoka.

Mutoka alikuwa miongoni mwa waanzilishi wa AFC Leopards pamoja na Ben Ashihundu, Joseph Akoya, Peter Shiyuka na Zakaroia Shimechero, Ben Amimo (wote marehemu).

Leopards ilianzishwa na timu mbali mbali za Nairobi zilizokuwa na asili Magharibi mwa Kenya, lengo likiwa kushindana na Luo Union iliyokuwa ikitawala soka katika ngazi ya kitaifa.

Kufikia sasa, Leopards inajivunia mataji 12 ya Ligi Kuu ya Kenya, 10 ya Kombe la Shirikisho, matano ya Shirikisho la Soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) miongoni mwa mengine mengi ya viwango vya chini.

Shimoli alisema kutakuwa na burudani ya kila aina kuanzia Machi 22 hadi Machi 24 ambayo ndio siku ya kilele cha tamasha hizo zitakazofanyika katika uwanja wa kitaifa wa Nyayo.

Alisema Leopards imealika timu ya AE Ramassa kutoka Uhispania katika mechi ya kirafiki kuipamba siku ya kilele na kileleta cha maadhimisho. Kabla ya mechi hiyo, timu ya Leopards Ladies itacheza na TBC, halafu AFC Leopards Legends wacheze na Gor Mahia Legends.

Wakati wa sherehe hizo, Shimoli alisema mashabiki watakaomiminika uwanjani humo watatumbuizwa na wasanii maarufu kwa vibao motomoto kuanzia Machi 23, 2024, huku wakipata burudani moja baada ya nyingine sambamba na mbwembwe za Ingwe@60.