Habari Mseto

Sherehe za Jamhuri Dei zanoga Nyayo

December 12th, 2020 1 min read

Na SAMMY WAWERU

AGHALABU katika sherehe na maadhimisho ya siku za kitaifa nchini, ndege za kikosi cha wanajeshi wa Kenya (KDF) ndizo hushiriki kuonyesha umahiri wao kazini.

Hata hivyo, katika maadhimisho ya Jamhuri Dei mwaka huu, 2020, Makala ya 57, ambayo yamefanyika leo Jumamosi, Desemba 12, katika uwanja wa Nyayo, Nairobi ndege za vikosi vingine vya usalama zimeshiriki.

Ndege ya Kikosi cha Polisi, ya Shirika la Huduma za Wanyamapori Nchini (KWS) na ya Shirika la Misitu (KFS) zimejumuishwa katika maadhimisho hayo, kuonyesha uweledi na umahiri kazini.

“Ndege za wanajeshi ndizo zimekuwa zikionekana katika hafla za kitaifa. Kwa mara ya kwanza, ndege ya Kikosi cha Polisi, Shirika la Huduma za Wanyamapori na Shirika la Misitu zimeshiriki,” ametangaza Warrant Officer 1, Gibson Mwandawiro wakati akieleza aina ya ndege zilizopita angani kama ilivyo desturi ya sherehe za maadhimisho ya siku za kitaifa.

Bw Mwandawiro ni afisa wa kijeshi, na ambaye amehudumu kwa muda mrefu kama Mfawidhi wa hafla za kitaifa nchini.

Kwenye maadhimisho ya siku za kitaifa, baada ya Rais kukagua gwaride la heshima la vikosi jumuishi vya wanajeshi, Kama Amiri Jeshi Mkuu wa Kenya, maafisa wanapoondoka uwanjani, ndege za KDF hupita angani na mbele ya Rais kuonyesha umahiri wao.

Jamhuri Dei 2020, Rais Uhuru Kenyatta ameongoza taifa katika maadhimisho.