Michezo

Sherehe za ‘kuudhi’ zamletea Bellingham balaa Ujerumani

Na CHRIS ADUNGO July 6th, 2024 2 min read

FOWADI matata wa Uingereza, Jude Bellingham, huenda akaepuka marufuku na badala yake akatozwa faini tu baada ya kuibuka kwa video za jinsi anavyosherehekea mabao yake.

Nyota huyo wa Real Madrid alijipata pabaya wiki hii kwa kufanya kitendo kinachodaiwa kuwa cha kuudhi, akisherehekea bao la ushindi alilofungia Uingereza dhidi ya Slovakia kwenye mechi ya 16-bora dimba la Euro nchini Ujerumani.

Video zilisambazwa mitandaoni zikimuonyesha Bellingham akishika sikio lake la kushoto huku ameuweka mkono wa kulia mbele ya fupanyonga, kutoa ishara ya mtu anayeshiriki ngono.

Ishara hiyo ilikuwa jibu la dharau kwa mashabiki wa Slovakia waliopoteza pambano hilo 2-1.

Tukio hilo lilichochea vinara wa mashindano hayo ya Euro kutangaza kuwa Bellingham atajutia matendo yake.

Kulingana na gazeti la Bild nchini Ujerumani, ishara hiyo huenda ikachochea waandalizi wa Euro kumpiga faini ya “mamilioni kidogo” na kumruhusu awakilishe Uingereza katika mechi zilizosalia.

Hata hivyo, Shirikisho la Soka la Uingereza (FA) limechomoa video ambazo linapania kutumia kumtetea Bellingham. Kwa mujibu wa FA, ishara hiyo haikuwa ya matusi ila ya kusherehekea tu ushindi na imezoeleka sana katika soka ya Uhispania.

Si mara ya kwanza kwa Bellingham kugonga vichwa vya habari kwa matendo yenye utata tangu ajiunge na Real baada ya kuagana na Borussia Dortmund.

Mnamo Aprili mwaka huu, aliondoka ugani mwishoni mwa mechi ya El Classico dhidi ya Barcelona akiwa ameshika sehemu zake za siri.

Alidai wakati huo kwamba alikuwa akihisi maumivu kwenye sehemu zake za siri baada ya kuumia paja akiwa uwanjani.

Kulingana na gazeti la Bild nchini Ujerumani, ishara aliyoitoa dhidi ya Slovakia huenda ikachochea waandalizi wa Euro kumpiga faini ya “mamilioni kidogo” na kumruhusu kuwakilisha Uingereza katika michuano yote mingine iliyosalia kwenye fainali za Euro mwaka huu.

Uingereza wataavana na Uswisi kwenye robo-fainali mjini Dusseldorf, leo.

Mnamo 2019, kocha wa Atletico Madrid, Diego Simeone, alitozwa faini ya Sh2.8 milioni kwa kutoa ishara sawa na kile ambacho Bellingham anatuhumiwa kufanya.

Simeone alifanya hivyo baada ya kuongoza kikosi chake kupepeta Juventus 2-0 katika mkondo wa kwanza wa hatua ya 16-bora ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) nchini Uhispania. Ishara hiyo imewahi pia kumweka supastaa Cristiano Ronaldo pabaya nchini Uhispania, Italia na Saudi Arabia.