Habari

Sherehe za Mwaka Mpya zafana Mombasa

January 1st, 2020 1 min read

Na MISHI GONGO

MAELFU ya watu kutoka sehemu mbalimbali za nchi wamemiminika katika ufuo wa Bahari Hindi wa umma wa Jomo Kenyatta maarufu Pirates mjini Mombasa kwa sikukuu ya Mwaka Mpya.

Watu hao ambao wengi wemetoka maeneo ya bara walifika maeneo hayo kupiga mbizi na kuonja mapochopocho ya Pwani.

Japo Mombasa ina fuo nyingi za bahari watu wengi hupendelea kutembea Pirates kwa sababu ya ukubwa na vyakula vya kipwani vinavyouzwa sehemu hiyo.

Wakenya na wageni wafurahia maji ya Bahari Hindi huku wengine wakipunga upepo katika ufuo wa Jomo Kenyatta, Mombasa mnamo Jabuari 1, 2019. Picha/ Kevin Odit

Bi Margaret Owino ambaye alikuwa ameandamana na wanawe wanne, amesifu mji wa Mombasa kwa kuwa na mandhari ya kuvutia.

“Hii ni mara yangu ya kwanza kuona bahari na nimefurahia sana. Ninatarajia kurudi tena likizo ijayo,” amesema Bi Owino.

Mwenzake Bi Ruth Njenga amesema hewa safi na mandhari mazuri baharini humpa utulivu na kumpunguzia msongo wa mawazo.

“Kwetu hakuna bahari na ndiyo maana huwa nafurahia sana kuja kupunga upepo wa kutoka baharini kila ninapozuru jiji la Mombasa. Wataalamu husema kuwa eneo hili ni ‘dawa’ kwa watu wenye msongo wa mawazo,” akasema Bi Njenga.

Wenyeji wa Pwani ya Kenya huamini kuwa maji ya bahari ni dawa inayotibu maradhi mbalimbali yakiwemo ya macho, matatizo ya ngozi, mipasuko kwenye visigino, mapunye ya uso na kadhalika.

Bw Juma Bashir mfanyabiashara katika ufuo wa bahari hiyo anasema watu wengi wanaozuru bahari huoga na maji yake kama tiba.

“Maji na mchanga wa bahari hutumika kama tiba miongoni mwa watu na hata wengine huamini kuoga kutumia maji haya hutoa nuksi na kuondoa mkasa,” ameeleza Bw Bashir.