Makala

SHERIA BARABARANI: Hatia za trafiki zitakazowatupa seli abiria wengi bila taarifa

November 13th, 2018 2 min read

Na BENSON MATHEKA

SERIKALI inapoendelea kutekeleza sheria za trafiki, huenda abiria wakajipata matatani hata kuliko madereva iwapo watakiuka sheria zinazowahusu.

Kulingana na sheria hizo, abiria wanafaa kudumisha utulivu ndani ya magari ya uchukuzi wa umma na hawafai kutumia lugha ya matusi au kuzua fujo.

Sheria ya trafiki ya Kenya inayoendelea kutekelezwa inasema ni makosa kwa abiria yeyote kuingia ndani ya gari la uchukuzi wa umma kupitia kwa dirisha au eneo lolote lisiloruhisiwa.

“Hakuna abiria anayepaswa kuingia au kushuka kutoka garini kupitia eneo tofauti isipokuwa milango iliyowekwa,” inaeleza sheria ya trafiki.

Sheria pia inasema ni makosa kwa abiria yeyote kuzuia au kujaribu kuzuia abiria wengine kuingia au kushuka kutoka katika gari la uchukuzi wa umma.

Hii ni sawa na abiria kuingia na kukatalia ndani ya gari la uchukuzi wa umma licha ya kutakiwa kutofanya hivyo na mtu aliyeruhusiwa iwapo gari hilo litakuwa limejaa.

Makosa mengine ambayo abiria huwa wanafanya ni kuketi katika maeneo yasiyofaa ndani ya matatu au kuhusika na kitendo chochote kinachofanya matatu kusababisha majeraha au kukosesha watu wengine utulivu.

Abiria hafai kuhusika na kitendo chochote kinachoweza kumfanya dereva kukosa kuzingatia usukani gari likiwa kwenye mwendo. Hivyo basi, ni makosa kwa abiria kumsemeza dereva akiwa kwenye usukani isipokuwa iwe inafaa kuzungumza naye.

Kulingana na sheria za trafiki za Kenya, abiria hafai kutoa ishara kwa dereva ambayo anaweza kuichukulia kuwa imetoka kwa kondakta. Hii ni kumaanisha kuwa abiria wanaogonga mabati au vyuma garini kutaka dereva awashushe huwa wamevunja sheria.

Aidha, sheria inaeleza kuwa abiria hafai kutema mate au kuchafua kwa njia yoyote gari la uchukuzi wa umma. “Abiria hafai kutema mate, kuharibu makusudi au kuchafua sehemu yoyote ya matatu,” inaeleza sheria.

Aidha, inapiga marufuku abiria kusambaza karatasi au vifaa vyovyote vya matangazo akiwa ndani ya gari la uchukuzi wa umma kwani huko ni kuendeleze uchuuzi wa bidhaa kwa abiria.

Sheria inalinda abiria dhidi ya kelele za wenzao kwa kusema kwamba hakuna mtu anayefaa kuudhi wasafari wakiwa ndani ya matatu kwa kutumia vifaa vyovyote au kuungana na watu wengine kutoa sauti kubwa kwa kuimba, kupiga kelele au vinginevyo.

Wanaozoea kunywa maji ya chupa au juisi na kuzirusha nje ya matatu chupa huwa wanakiuka sheria na wanaweza kushtakiwa.

Makosa mengine ni kuvuta sigara wakiwa ndani ya matatu, kuchafua viti au mavazi ya abiria wengine au kubeba mizigo mingi inayotatiza abiria wengine ndani ya matatu. Ni makosa kubeba wanyama katika magari yanayobeba watu.

Kulingana na sheria, kila abiria anafaa kupewa risiti akilipa nauli na kuhifadhi tiketi. Ni makosa kwa mtu kujaribu au kutumia tiketi ya mtu mwingine au ambayo imefutika au maandishi kubadilishwa au kupanda matatu akiwa mlevi.

“Mtu yeyote hafai kupanda au kujaribu kupanda matatu akiwa mlevi au ikiwa amepanda akatae kushuka,” inaeleza sheria.

Sheria za trafiki za Kenya pia zinasema kila abiria ni lazima awe na tiketi ya nauli ya safari yake. Ni makosa kushuka gari likitembea au kushukia eneo lisiloruhusiwa katika barabara za mijini.

Katika safari, kila abiria anafaa kufunga mkanda wa usalama, kumaanisha mtu hafai kupanda gari ambako hataweza kuketi vyema kuweza kufunga mkanda.