Sheria kali zatungwa kwa Gredi 7

Sheria kali zatungwa kwa Gredi 7

NA WANDERI KAMAU

SERIKALI jana Jumanne ilitoa masharti makali ambayo yatazingatiwa katika ufundishaji wa wanafunzi wa Gredi 7 katika Shule za Sekondari ya Msingi (JSS).

Kulingana na masharti hayo, masomo ya Kiingereza na Hisabati yatakuwa yakifunzwa kila siku katika shule hizo.

Kando na hayo, walimu watahitajika kuwafunza wanafunzi masomo yanayohusiana na michezo kabla ya wanafunzi kula chakula cha mchana.

Wanafunzi watakuwa wakisoma jumla ya masomo 12.

Masomo tendaji kama vile Somo la Kilimo yatakuwa yakifunzwa mara mbili kwa wiki. Masomo tendaji yanajumuisha Kilimo, Sayansi ya Pamoja, Sayansi ya Masuala ya Kompyuta, Sayansi ya Nyumbani na Sanaa.

Kinyume na hali ilivyo katika mfumo wa elimu wa sasa, shule hizo zitakuwa na vipindi vya kuwapa wanafunzi mwongozo kuhusu taaluma ambazo wangetaka kusomea katika maisha yao ya baadaye.

Kwa sasa, mfumo wa elimu uliopo haujajumuisha vipindi vya kuwapa wanafunzi mwongozo kuhusu mustakabali wao kitaaluma.

Ni hali ambayo imetajwa kuchangia wanafunzi wengi kutofanya maamuzi yafaayo ya kitaaluma chini ya mfumo wa elimu wa 8.4.4.

Masharti hayo ni baadhi ya mapendekezo ambayo yametolewa na Jopokazi Maalum lililobuniwa na Rais William Ruto, Septemba 2022, kulainisha Mfumo wa Elimu ya Umilisi na Utendaji (CBC).

Jopo hilo linaongozwa na Profesa Raphael Munavu, na linawajumuisha wanachama 42, wengi wao wakiwa wadau na wataalamu wa elimu kutoka viwango tofauti.

Kwenye masharti hayo, shule pia zitajumuisha wawakilishi kutoka vitengo mbalimbali kwenye utengenezaji wa ratiba zao za masomo ili kuhakikisha kuwa kila idara imejumuishwa.

Mbali na hayo, majina ya shule za msingi ambako shule za sekondari za msingi zitabuniwa yatabadilishwa.

Kwa mfano, shule inayoitwa Shule ya Msingi ya Mwendapole itabadilishwa jina na kuwa Shule ya Msingi na Upili ya Mwendapole.

Kwa mujibu wa masharti hayo, uongozi wa shule hizo utakuwa na usemi mkubwa katika uendeshaji wake.

Uongozi huo ndio utakaoamua aina ya sare ambazo wanafunzi watakuwa wakivalia.

Pia, utabuni Sajili Maalum ya Kusuluhisha Malalamishi. Wizara ilisema kuwa hatua hiyo inalenga kuhakikisha malalamishi yanayoibuka katika uendeshaji wa shule hizo, ikizingatiwa zitakuwa zikiendesha mfumo mpya wa elimu.

“Lengo letu ni kuweka mikakati yote ifaayo kuhakikisha masuala yote yatakayoibuka yatasuluhishwa kwa njia itakayowashirikisha wadau wote na kwa namna ambayo haitaathiri uendeshaji wa shule hizo,” akasema Waziri wa Elimu, Ezekiel Machogu alipokuwa akitangaza matokeo ya Mthani wa Kidato cha Nne (KCSE) wiki iliyopita.

Wazazi pia watakuwa na usemi mkubwa, kwani shule zote zitahitajika kubuni vyama maalum vya wazazi ili kuwashirikisha pia katika uendeshaji wake.

  • Tags

You can share this post!

Magoha, msomi aliyejituma kwa yote aliyoyafanya

TUSIJE TUKASAHAU: Majangili waendelea kuhangaisha Wakenya...

T L