Habari

Sheria kuhusu viazi kuunganisha wadau

August 15th, 2019 2 min read

Na SAMUEL BAYA

WADAU wote katika sekta ya kilimo cha viazi sasa watalazimika kuingia katika miungano wanapofanya shughuli zao.

Kulingana na sheria mpya zinazolinda kilimo cha viazi, inataka kubuniwe vituo maalumu ambako wakulima wa viazi watakuwa wakipeleka mazao yao kwa wanunuzi, hivyo basi kuwatoa nje madalali ambao wamekuwa wakiingia mashambani kununua viazi hivyo.

“Lengo la sheria hizi mpya ni kutoa mwongozo na kuimairhsa mapato katika kilimo cha viazi, kupanua mawazo ya jinsi ambavyo kinaweza kutumika kuendelea maisha mema ya mkulima na wale washika dau wote wanaounganishwa na kilimo hicho,” kinasema mojawapo ya vifungu vya sheria hiyo ambavyo Taifa Leo ilibahatika kuviona.

Hapo jana, afisa mkuu wa kilimo katika serikali ya kaunti Bw Joel Kibet alisema hakuna msamaha wala muda wa kupoteza zaidi na wakulima sasa lazima watiii sheria hiyi mpya.

Sheria hiyio mpya vile vile inazitaka serikali za kaunti kuhakikisha kwamba viazi ambavyo vinauziwa wananchi ni bora kiafya na ni vya thamani ambayo inaweza kufaidi mkulima pamoja na wahusika wengine.

“sheria hii pia inalenga kuhakikisha kwamba viazi vinatolewa kutoka mashambani vikiwa bgora, visafirishwe kwa njia salama zaidi hadi katika masoko na kuwafikia wanunuzi. Kwa sababu hiyo pia uzani wa viazi kufikishwa sokoni ni kilo hamsini na wala sio zaidi,” kinasema kifungu chengine katika sheria hizo mpya.

Kwenye mahojiano na Taifa Leo Bw Kibet alisema mambo yatabadilika sana katika sekta hiyo na wakulima wengi watanufaika.

“Kila anayekuza viazi sasa lazima asajiliwe na serikali ya kaunti na kupatiwa cheti. Vile vile watakuwa wanaeleza kama wanakuzia wapi viazi vyao na tunashukuru kwamba tayari baadhi ya wakuzaji wa viazi wameanza kukubali mwito huo na wanaendelea kufanya kama sheria inavyosema,” akasema Bw Kibet.

Vile vile Bw Kibet alisema kuwa kulingana na sheria hiyo mpya, miungano mikubwa ya wakulima itakuwa na uwezo wa kutoa vyeti kwa miungano midogo ya wakulima na kwamba hakutakuwa na usajili wa miugano miwili katika kila kipande kimoja cha ardhi, hatua ambayo inalenga kuangamiza matatizo ya kupigania ardhi za kilimo cha viazi.

“Sheria imewahusisha mitambo ya kutengeneza bidhaa za viazi, wale wanaotafutia soko viazi pamoja na madalali kwamba ni lazima wasajiliwe na serikali ya kaunti ili wajulikane shughuli zao rasmi,” akasema Bw Kibet.

Hata hivyo mmoja wa madalali wa Francis Njuguna alilaumu serikali kutokana na sheria hiyo mpya akisema iliharakishwa. Alisema wao kama washika dau wakuu katika biashara hiyo hawakuhusishwa mbali na wakulima.

“Nimekuwa katika biashara hii kwa muda mrefu lakini sheria hizi mpya zinatutatiza. Hakukuwa na hamsisho la kutosha ila kila kitu kiliharakishwa,” akasema Bw Njuguna.

Alitaja mfano wa kupunguza gunia la viazi kutoka kilo 110 hadi kilo 50 kuwa mateso kwao.

“Lile gunia kubwa limekuwa likiuzwa kwa Sh1,300 na lina faida. Sasa lile gunia dogo la kilo hamsini litakosa bei mwafaka sokoni,” akasema Bw Njuguna.