Sheria maalum zawekwa kudhibiti sekta ya ujenzi Kiambu

Sheria maalum zawekwa kudhibiti sekta ya ujenzi Kiambu

Na LAWRENCE ONGARO

KUFUATIA kuporomoka kwa jumba moja eneo la Kinoo, Kaunti ya Kiambu hivi majuzi, Gavana James Nyoro na maafisa wakuu wa serikali wameweka mikakati na utaratibu wa kufuatiliwa na wajenzi.

Gavana Nyoro, kamishna wa Kiambu, Bw Wilson Wanyanga, na wasimamizi wa ujenzi wakiwemo wahandisi wa majumba, wametoa mwelekeo kwa wajenzi wote.

Baadhi ya mambo yaliyoafikiwa ni kwamba serikali ya kaunti na wahandisi wakuu wa majumba ni lazima watoe mwelekeo kwa jumba lolote litakalotarajiwa kujengwa katika eneo lolote la kaunti.

Wakati huo pia kaunti hiyo itaweka kituo kimoja kitakachojumuisha mipango ya ujenzi, mipango ya kuanzisha ujenzi wowote, ukaguzi, na ununuzi wa vifaa vyote ni miongoni mwa masuala yatakayojadiliwa kwa pamoja kwenye kituo hicho.

Wakati huo pia wakuu hao walikubaliana ya kwamba kutakuwepo na kamati ya watu walioteuliwa watakaofanya ukaguzi kamili wa jinsi jumba lolote linavyojengwa kuona kama limepitia sheria zote zinazostahili za ujenzi, na pia kukagua lile halijapita matakwa ya kibali cha ujenzi.

“Huu ni utaratibu wa kuweka mambo sawa ili wanaotarajia kujenga majumba ya kisasa wawe na mipango na wapate kibali kutoka kwa wahusika,” alisema Dkt Nyoro.

Wakati huo pia ilipitishwa ya kwamba ni sharti gavana ajulishwe kwa maandishi mipango yote ya ujenzi inayoendeshwa, na yeyote atakayejenga bila kupata idhini maalum atalazimishwa kubomoa jumba lake kwa gharama yake mwenyewe.

Kulingana na mipango hiyo, kutakuwepo na tovuti maalum itakayokuwa na majina ya wahandisi waliohitimu kuendesha ujenzi wa majumba na kwa hivyo mwananchi yeyote anayetaka kujenga ni sharti apitie kwenye tovuti hiyo.

Wakati wa mkutano huo, wakuu hao wote kwa kauli moja walikubaliana ya kuwa sheria zote zilizosajiliwa zitatekelezwa mara moja ili kukabiliana na wahandisi laghai ambao lengo lao kuu ni kujilimbikizia fedha nyingi bila kijali ubora wa majumba wanayojenga bila mpango.

You can share this post!

Nice waadhibiwa vikali baada ya mashabiki kuzua vurugu...

ULIMBWENDE: Njia rahisi za kutunza ngozi yako wikendi