Makala

SHERIA: Marufuku ya kuasili watoto si kwa raia wa Kenya

September 21st, 2019 2 min read

Na BENSON MATHEKA

FLORENCE Aketch, msomaji kutoka Kisumu anauliza ikiwa uamuzi wa Baraza la Mawaziri wiki jana wa kuzuia wageni kuasili watoto kutoka nchini utaathiri raia pia.

Anataka pia nifafanue kuhusu uamuzi huo na athari zake kwa wale wanaotaka kuasili watoto.

Kulingana na msomaji huyu, uamuzi huo ni pigo kwa wale waliokuwa wameanza utaratibu wa kuasili watoto hasa wasiokuwa na uwezo wa kupata watoto.

Kwanza, ningetaka kueleza kuwa kile ambacho Baraza la Mawaziri lilifanya ni kupinga marufuku raia wa kigeni pekee kuasili watoto wanaozaliwa na wazazi wa humu nchini na wala sio kuzuia Wakenya kuasili watoto.

Hii ilikuwa ni kuzuia ulanguzi wa watoto ambao raia wa kigeni wamekuwa wakiendesha kupitia mpango huu.

Kote ulimwenguni, walanguzi wa watoto wamekuwa wakitumia sheria za kuasili watoto za mataifa ya Afrika, nchi za bara Asia na ya Kusini mwa Amerika kuendeleza uhalifu huu kinyume na sheria za kimataifa.

Hivyo basi, kumekuwa na malalamiko kuhusu suala hili huku visa vya wizi wa watoto vikiongezeka na kuhusishwa na uasili wa watoto.

Kwa raia wa Kenya, kuna sheria wanazopaswa kufuata kuasili watoto ikiwa ni pamoja na kupata idhini ya mahakama baada ya uchunguzi wa kina kufanywa na idara zinazohusika.

Idara hizi ni lazima ziandae ripoti ambayo huwa inawasilishwa mahakamani kabla ya kufanya uamuzi wa kukubalia mtu kuchukua mtoto asiye wake na kumlea kama wake.

Ni muhimu kuelewa kuwa tofauti na raia wa kigeni, ni rahisi kufuatilia mtoto anayeasiliwa na raia wa Kenya ili kujua hali yake. Hii ndio sababu Baraza la Mawaziri liliagiza Shirika la Kushughulikia Maslahi ya watoto (CWSK) kulainisha shughuli zake.

Kwa hivyo, uamuzi wa Baraza la Mawaziri wa kupiga marufuku raia wa kigeni kuasili watoto unalenga kukabiliana na ulanguzi wa watoto wanaouzwa katika mataifa ya kigeni na watu wanaowachukua wakidai wanataka kuwalea.

Ulanguzi wa watoto ni uhalifu kote ulimwenguni na adhabu yake huwa kali kwa wanaopatikana na hatia.